Erick Kabendera amuomba msamaha Rais

Muktasari:

  • Septemba 22, 2019 Rais wa Tanzania, John Magufuli alitoa ushauri kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kuwasamehe watuhumiwa wa uhujumu uchumi watakaokiri makosa na kukubali kulipa fedha na mali walizohujumu kuachiwa huru. Rais Magufuli alitoa siku saba kuanzia Septemba 23 hadi 29, 2019 kumwandikia barua DPP.
  • -Jana Jumatatu Septemba 30, 2019 DPP alisema hadi siku hizo zinamalizika watuhumiwa 467 waliokuwa wameandika barua ya kukiri makosa na kukubali kulipa Sh107.8 bilioni. Rais Magufuli ameongeza tena siku saba ili ambao walishindwa kufanya hivyo ndani ya muda wa awali kuomba kukiri, kulilpa na kusamehewa.

Dar es Salaam. Mwandishi wa habari nchini Tanzania, Erick Kabendera amemwomba radhi Rais na Serikali ya nchi hiyo akiomba kusamehewa kama kuna makosa ameyafanya.

Kabendera amesema hayo leo Jumanne Oktoba 1, 2019 jijini Dar es Salaam kupitia kwa wakili wake, Jebra Kambole.

Kambole amesema hayo muda mfupi baada ya kesi inayomkabili mwandishi huyo ya uhujumu uchumi na kutakatisha fedha Sh173.24 milioni kuahirishwa hadi Oktoba 11, 2019 kutokana na upelelezi kutokamilika.

“Sisi kama mawakili tunatoa ombi kwa Rais, kama Erick katika utendaji kazi wake kama kuna mahali alimkosea Rais au Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa niaba yake, familia yake, ndugu zake tumwombe radhi,” amesema Kambole

Katika kesi ya msingi,  mshtakiwa anadaiwa katika siku tofauti kati ya Januari 2015 na Julai 2019 jijini Dar es Salaam, alitoa msaada katika genge la uhalifu kwa nia ya kujipatia faida.

Katika shtaka la pili, inadaiwa siku na mahali hapo mshtakiwa bila kuwa na sababu za msingi kisheria alishindwa kulipa kodi ya Sh173.24 milioni ambayo ilitakiwa ilipwe kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Katika shtaka la utakatishaji fedha,  kati ya Januari 2015 na Julai 2019 ndani ya jiji na mkoa wa Dar es Salaam mshtakiwa alijipatia kiasi hicho cha Sh173.2 milioni wakati akizipokea alijua kuwa fedha hizo ni mazao ya makosa tangulizi ya kukwepa kodi na kujihusisha na genge la uhalifu.