Wakili akwamisha kesi ya bomba la mafuta

Muktasari:

Kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili mfanyakazi mstaafu wa Shirika la Mafuta Tanzania na Zambia (Tazama), Samwel Nyakirang'ani (63) na wenzake 11 imeshindwa kuendelea kutokana na wakili anayeendesha kesi hiyo kuwa mgonjwa

Dar es Salaam. Kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili mfanyakazi mstaafu wa Shirika la Mafuta Tanzania na Zambia (Tazama), Samwel Nyakirang'ani (63) na wenzake 11 imeshindwa kuendelea kwa kuwa wakili anayeendesha kesi hiyo ni mgonjwa.

Hayo yameelezwa na Hakimu Mkazi Mkuu ,Thomas Simba, leo Januari 30, 2019 baada ya wakili wa Serikali Faraji Nguka kueleza kesi hiyo imekuja kwa ajili ya kutajwa na upelelezi haujakamilika

Hakimu Simba amedai kuwa asubuhi aliwasiliana na wakili husika na kumweleza kuwa ni mgonjwa anaelekea hospital hivyo.

"Naona tuahirishe kwa siku chache ili tuipange tarehe za karibu kwa kuwa asubuhi nimewasiliana na wakili wa Serikali anayeendesha kesi hii akasema ni mgonjwa na anaelekea hospitali," ameeleza Hakimu Simba

Baada ya maelezo hayo, Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi Februari 7,2019 kesi hiyo itakapotajwa tena.

Nyakirang’anyi na wenzake wanakabiliwa na mashtaka matatu likiwemo la kujiunganishia isivyo halali bomba la mafuta, mali ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA).

Washtakiwa wengine katika kesi  hiyo ni Nyangi Mataro (54) mwalimu wa Shule ya Msingi Ufukoni na mkazi wa Kisiwani Mkajuni Kigamboni.

Mfanyabaishara, Farijia Ahmed (39) mkazi wa Soko Maziwa Kigamboni, Malaki Mathias (39) mkazi wa Magogoni, Kristomsi Angelus (25) mkazi wa Soko Maziwa,  Fundi Ujenzi Pamfili Nkoronko (40) mkazi wa Tungi Kasirati na Henry Fredrick (38) mkazi wa Tungi Kigamboni.

 

Wengine ni Audai Ismail (43) ambaye ni mkazi wa Kibaha, Chibony Emmanuel, Roman Abdon, Amina Shaban na Zubery Ally.

 

Kwa pamoja washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka matatu ya uhujumu uchumi kwa  kujiunganishia isivyo halali bomba la mafuta, kinyume cha sheria ya uhujumu uchumi.

 

Katika shtaka la kwanza, kati ya mwaka 2015 hadi Januari 8, 2018, eneo la Tungi Muungano, wilaya ya Kigamboni, washtakiwa wanadaiwa kujiunganishia bomba la mafuta ya dizeli lenye upana wa inchi moja kutoka katika bomba la upana wa inchi 24, bila kuwa na kibali kutoka TPA.

Katika shtaka la pili ambalo ni kuharibu miundombinu, inadaiwa siku hiyo ya tukio, washtakiwa walitoboa bomba  hilo ambalo lilikuwa likitumika kufirisha mafuta, mali ya  TPA.

Katika shtaka la tatu, washtakiwa waliharibu bomba la mafuta mazito (Crude oil) la upana wa inchi 28, ambalo lilikuwa likitumika kusafirisha mafuta ghafi, mali ya TPA.

dhamana.