Wakulima, wafugaji wapatiwa mbadala uhakiki wa viuatilifu

Wednesday February 26 2020

Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Mawasiliano

Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Mawasiliano TTCL, Kezia Katamboi (kulia), akibadilishana mkataba na Kaimu Mkurugeni Mkuu wa Taasisi ya utafiti wa viuatilifu vya Kudhibiti visumbufu katika Ukanda wa Kitropiki (TPRI), Dk Margaret Mollel baada ya kusaini mkataba kwa ajili ya maandalizi ya kutoa huduma ya T- Hakiki.     

By Ephrahimu Bahemu, Mwananchi

Dar es Salaam. Katika kudhibiti viuatilifu feki, Taasisi ya Utafiti wa Viuatilifu Ukanda wa Tropiki (TPRI) na  Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL Corporation), zimeingia makubaliano ya maandalizi ya uzinduzi wa mfumo wa kuvihakiki kwa kutumia simu za mkononi.

Mfumo huo uliopewa jina la ‘T–Hakiki’, utamuwezesha mkulima kupata taarifa ya kiuatilifu kilichosajiliwa na kwa matumizi sahihi ili kuleta tija katika kilimo

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Jumatano Februari 26, 2020 wakati wa kusaini mkataba, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TTCL Corporation, Kezia Katamboi anasema baada ya makubaliano hayo, utoaji wa huduma hiyo unatarajiwa kuanza mwezi ujao ikiwa ni baada ya kukamilisha baadhi ya taratibu zinazotakiwa.

Anasema hatua hiyo ni kubwa katika kulinda bidhaa za kilimo na ufugaji kwani itahakikisha  wakulima na wafugaji wanapata mavuno yanayostahili.

“Kwa kupitia mfumo huu ambao utatumia mawasiliano ya TTCL Corporation utakuwa suluhisho ya kuondoa viuatilifu feki sokoni na kuongeza kasi ya matumizi ya viuatilifu sahihi vya kilimo na ufugaji kwa kuwa mtandao wa TTCL Corporation umeenea nchi nzima hivyo wakulima wote nchi nzima watanufaika na mradi huu.

Mkurugenzi wa Biashara wa Quincewood ambayo ayenasimamia mfumo huo, Fatma Fernandes anasema sekta ya kilimo ni muhimili wa maendeleo ya uchumi.

Advertisement

“Sekta hii inachangia kiasi cha nusu ya pato la Taifa, robo tatu ya bidhaa zinazouzwa nje ya Nchi na chanzo cha chakula pamoja na utoaji wa fursa za ajira zaidi ya asilimia 75 ya Watanzania.

“Kilimo kina uhusiano na sekta zisizo kuwa za kilimo kupitia uhusiano wa usafishaji kwenda kwenye usindikaji wa mazao ya kilimo, matumizi  ya ndani, uuzaji nje ya Nchi na uzalishaji wa  malighafi kwa ajili ya  viwanda vyetu.

Mkuu wa Taasisi ya Utafiti na Udhibiti wa Viuatilifu katika Ukanda wa Kitropikia, Dk Margaret Mollel anasema huduma ya “T-Hakiki” itamuwezesha mkulima kupata  taarifa kuhusu viuatilifu  vilivyosajiliwa na vyenye ubora unaotakiwa  kwa kutumia hapo alipo kwenye sehemu yake ya kilimo.

 

“Pia itamwezesha kujua matumizi sahihi ya viuatilifu kulingana na visumbufu lengwa kwa kuwasiliana na mamlaka ya TPRI pamoja na wamiliki wa viuatilifu na kutoa taarifa sahihi kwa TPRI kuhusu viuatilifu ambavyo havina ubora kwa ajili ya ufuatiliaji na kuchukua hatua,” alisema.

Ubunifu wa huduma hiyo pia utaisaidia TPRI kutapa taarifa na ufuatiliaji wa urahisi wa viuatilifu wakati vikiwa sokoni pamoja na taarifa kutoka kwa mkulima yaani mtumiaji wa mwisho

“Pia TPRI kama mdhibiti wa viuatilifu, T-Hakiki itafanya ufuatiliaji moja kwa moja bila hata kumshirikisha mtengenezaji au muingizaji wa kiuatilifu baada ya kupata taarifa kutoka kwa mkulima moja kwa moja juu kiualitifu husika endapo kitakuwa hakifanyi kazi iliyokusudiwa.

Advertisement