Walimu waeleza mafanikio ya Tehama kufundisha wanafunzi

Muktasari:

Walimu 400 wa shule za sekondari Mikoa ya Pwani na Morogoro wameeleza mafanikio ya kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) kufundisha wanafunzi.

Dar es Salaam. Walimu 400 wa shule za sekondari Mikoa ya Pwani na Morogoro wameeleza mafanikio ya kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) kufundisha wanafunzi.

Wakizungumza wakati wa mafunzo hayo yaliyofanyika Kibaha mkoani Pwani  baadhi ya walimu hao wamesema tangu walipoanza kutumia teknolojia hiyo miaka miwili iliyopita, kiwango cha ufaulu wa masomo wanayofundisha kwenye shule zao kimeongezeka.

Walimu hao wamejifunza na kuanza kutumia Tehama baada ya shirika la Global e-Schools and Community Initiative kupitia mradi wake wa matumizi ya teknolojia kujifunza na kufundishia wa African Digital Schools Initiative (ADSI)  kuwekeza kwenye sekta ya elimu.

Mwalimu wa Shule ya Sekondari Chalinze, Salagea Joel amesema matokeo ya kidato cha nne yaliyotoka mwaka 2019, yanaonyesha kuwa wanafunzi 28 wa shule hiyo walipata alama A katika somo la Fizikia baada ya kuanza kufundisha kwa kutumia teknolojia hiyo.

“Mwaka juzi tulikuwa na A 10 tu, hii inaonyesha wanafunzi wanaweza kujifunza vizuri zaidi na kuelewa ikiwa matumizi ya chaki yatapungua,” amesema.

Mwalimu wa hesabu  Shule ya Sekondari Bagamoyo, Violet Msuya amesema wanafunzi wanaojifunza kwa kutumia teknolojia hiyo huelewa haraka kwa sababu huwa wanajifunza kwa kusikia na kuona.

“Changamoto kubwa ni vifaa tu lakini kama tutawekeza hali itakuwa nzuri zaidi, wanafunzi wataweza kusoma vizuri,” amesema Msuya.

Awali mthibiti ubora wa Shule katika Wilaya ya Kibaha, Neema Materu alikiri kuwa matumizi ya Tehama kwenye kujifunzia yanachangia katika kuongeza ubora wa elimu shuleni.

 “Mkakati wetu ni kuendeleza jambo hili kwenye shule zetu na kwa hatua ya awali, walimu waliopewa mafunzo na wameanza kutumia Tehama watakuwa chachu kwa wenzao kujifunza,” amesema Materu.

Mratibu wa shirika hilo Mkoa wa Pwani, Bahati Mussa amesema ni rahisi wanafunzi wanaohitimu masomo kuingia kwenye ushindani wa soko la ajira ikiwa ufundishaji wa teknolojia ya Tehama utawekezwa.

“Siku hizi sio kama zamani, dunia inakimbia imebadilika sana, hawahitajiki makarani ila wataalamu mbalimbali wanaoweza kuendesha mitambo. Watawezaje kama aina ya ufundishaji itakuwa ya chaki, tunaweza kuwekeza kwenye matumizi ya Tehama,” amesema Mussa.

Mratibu wa shirika hilo nchini Tanzania, Joyce Msola amesema wanatarajia kuona kasi ya matumizi ya Tehama shuleni inaongezeka baada ya shule 40 za mkoa wa Pwani na Morogoro kuanza kuitumia.