Waliofariki ajali ya moto Morogoro wafikia 101

Friday August 23 2019

 

By Muyonga Jumanne, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Majeruhi mmoja kati ya 15 wa ajali ya moto mjini Morogoro waliolazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) amefariki leo Ijumaa Agosti 23, 2019.

Ajali hiyo ilitokea Agosti 10, 2019 katika mtaa wa Itingi, Msamvu barabara ya Morogoro-Dar es Salaam baada ya lori la mafuta kupinduka na kuwaka moto muda mfupi baada ya watu kuanza kuchota mafuta.

Tangu siku hiyo hadi Agosti 11, 2019 watu 100 waliripotiwa kufa huku wengine 15 wakiendelea na matibabu MNH na  leo amefariki mmoja na kufanya majeruhi hao kubakia 14

Mkuu wa kitengo cha mawasiliano ya umma wa MNH,  Aminiel Aligaesha amesema majeruhi 14  wapo chini ya uangalizi maalum.

Agosti 21, 2019 madaktari walisema sababu ya vifo hivyo ni kuungua kwa kiasi kikubwa na kuvuta moshi.

Hayo yalielezwa na madaktari bingwa wa upasuaji wanaowatibia majeruhi hao waliohamishiwa hapo kutoka Hospitali ya Mkoa wa Morogoro. Majeruhi walioletwa MNH kutoka Morogoro walikuwa 47 na sasa wamebaki 14 baada ya wengine 33 kufariki.

Advertisement

Dk Lauren Rwanyuma amesema majeruhi waliopelekwa MNH waliungua kwa zaidi ya asilimia 70 kiwango ambacho ni kikubwa zaidi kwa mwili kustahimili.

Amesema pamoja na kuungua kwa kiasi hicho majeruhi hao walivuta moshi mwingi ambao umeenda kuathiri sehemu za ndani za miili yao, ikiwemo figo na mapafu.

Dk Rwanyuma amesema licha ya madaktari kufanya jitihada kutibu majeraha na kuwaondoa kwenye hatari lakini athari walizopata kutokana na moto huo zilikuwa kubwa, kusababisha wapoteze maisha.

“Hata kama mtu ameungua kwa kiwango kikubwa kiasi gani jukumu la madaktari ni kuokoa maisha yake, wengi walikuja wameungua sana ila tulipambana na tunaendelea kupambana kuwanusuru waliobaki,” amesema Dk Rwanyuma.

Naye daktari bingwa wa upasuaji, Edwin Mrema amesema majeruhi hao pamoja na kuungua ngozi na kubaki wazi moshi waliovuta umeongeza hatari zaidi.

Advertisement