Wamiliki wa mabasi Mwanza walia uchache wa abiria

Muktasari:

  • Wakati jitihada za kudhibiti kusambaa ugonjwa wa corona, wafanyabiashara wa  mabasi jijini Mwanza wamelia mabasi kuondoka stendi yakiwa matupu huku wengine wakiyaegesha baada ya kukosa wasafiri.

Mwanza. Wakati jitihada za kudhibiti kusambaa ugonjwa wa corona nchini Tanzania zikiendelea, wafanyabiashara wa  mabasi jijini Mwanza wamelia mabasi kuondoka kituoni yakiwa matupu huku wengine wakiyaegesha baada ya kukosa wasafiri.

Mwenyekiti wa Kampuni za mabasi Kanda ya ziwa, Rogers Malaki akizungumza na Mwananchi leo Jumamosi Aprili 4,2020 amesema asilimia kubwa ya mabasi yameegeshwa kwenye yadi.

“Sasa hivi tunatoa huduma kama huduma lakini hatuzalishi faida, maana hata wanaojitokeza huwezi kuwaacha kuwasafirisha,” amesema Malaki

“Kwa sasa mfano gari inatoka Mwanza kwenda Iringa inaondoka na abiria 15 wakati ina siti 54, utaona mfanyabiashara kwa sasa anatumia akiba iliyopo ndani kutoa huduma kwa wananchi, hakuna anachoingiza.”

Amesema wafanyabiashara wengi wanaanza kukata tamaa na kuyapaki mabasi ndani kulingana na uwezo wa mtu mwenyewe, “lakini tunazidi kuwasisitiza wasikate tamaa waendelee kutoa huduma maana uchumi wa nchi utayumba.”

Amesema wameiomba serikali ijaribu kuongea na taasisi za fedha ambazo ziliwakopesha ili ziweze kuwavumilia kwa kipindi hiki cha janga la corona maana kwa hali  ilivyo sasa madeni yanaweza kukwama kulipika.

“Sawa mtu atalipa kwa awamu sasa hivi na hali ikiendelea kwa miezi mingine miwili hata ile akiba itaisha na kimsingi mtaji wake wote utaisha hivyo benki itakuja kuuza mali zake zote na kumfilisi,” amesema Malaki

Wakala wa kampuni ya mabasi ya Happy Nation, Lushinge Lushinge amesema “kwa sasa wanaosafiri ni wale wenye shughuli muhimu tu lakini kwa kweli wengi hawasafiri biashara imeyumba.

“Kampuni iliyokuwa na mabasi matatu yanatoka kila siku stendi kwasasa imebakiza basi moja tu nalo unakuta lina abiria 20, huwezi kuacha kuwasafirisha lakini kiukweli hali tete.”