Wananchi wampongeza Nape kwa kuomba msamaha

Wednesday September 11 2019

By Aurea Simtowe, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Watu wa kada mbalimbali wamempongeza mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye kwa uamuzi wake wa kumuomba msamaha Rais wa Tanzania, John Magufuli.

Jana Jumanne Septemba 11, 2019 mbunge huyo alikwenda Ikulu Dar es Salaam kumuomba radhi Magufuli kwa yaliyotokea, ikiwa ni siku chache baada ya wanachama wengine wawili kufanya hivyo.

Wametoa maoni hayo kutokana na swali lililoulizwa na Mwananchi na kuwekwa katika mitandao yake ya kijamii lililosema, “Uamuzi wa mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye kumuomba msamaha Rais Magufuli una maanisha nini.”

Hatua ya Nape kuomba msamaha imekuja takribani siku 53 tangu kusambaa kwa sauti inayofanana na ya waziri huyo wa zamani wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ikizungumza na wanasiasa wengine kuhusu barua ya makatibu wakuu wastaafu wa CCM, Yusuf Makamba na Abdulrahman Kinana kwa uongozi wa chama hicho wakilalamikia kuchafuliwa na mtu wanayedai anakingiwa kifua.

Mbunge huyo wa Mtama alikana kuzungumzia sauti hizo alipohojiwa na kituo cha televisheni, akisema kuna jinai ndani yake.

Wakijibu swali hilo Wilbrodus Maugo aliandika, “Hongera Nape kuomba radhi sio udhaifu ni uungwana kwani hakuna binadamu asiyekosea, hongera kwa hatua hiyo mmakonde.”

Advertisement

Barry_berrry aliandika, “Ina maana ya kuimarisha umoja katika Chama na kujiimarisha kimbinu na kimikakati wakati tukielekea Uchaguzi Mkuu 2020.”

Adam_mjomba amesema ni kosa gani alilifanya Nape huku akisema kama wameamua kutangaza msamaha watangaze na makosa.

“Kwani Nape amekosea nini kwa Magufuli, kama wameamua kutangaza msamaha basi waamue kutuambia na makosa waliofanyiana ndio maana ya ukweli na uwazi,” amesema.

Ngalisoi_laizer16 amesema, “Ina maanisha kuwa Nape amesoma alama za nyakati vizuri na alifaulu vizuri maana asingeenda kuomba msamaha 2020 angefyekelewa mbali na ubunge ungebaki historia kwake.”

luluvibes_amesema, “Nape kutokuwa na msimamo kwa kile anachokiamini. Na labda Nape ana tabia za umbea na uzushi

Kulya_lio ameandika, “Kuomba kwake msamaha ni tendo jema la unyenyekevu hasa kwa mtu mwenye Mamlaka kubwa zaidi yake. Amefanya jambo la maana kupatana naye,”

mrishokamdogo_a.k.a_mbilwa ameandika “Amefanya jambo sahihi, huyo ni mkuu wa nchi na mwakilishi wa mwananchi, kumkashifu alikua ametukosea wananchi hivyo kumuomba radhi inamaanisha amekubali kuwa alitukosea wananchi na ni jambo bora kabisa yeye kufanya hivyo.”

ibrahim Jamesir amesema, “Bado kunakosekana wanasiasa wakweli wanaoweza kusimamia wanachokiamini na other side hatuna wanasiasa wanaovumilia ukweli mchungu.”

Shaibuklassic amesema, “Ni nidhamu ya woga waliyonayo watu wa CCM hakuna kubwa hapo.”

Advertisement