Wanaodaiwa kumtapeli kiwanja Malecela wafikishwa mahakamani, wakosa dhamana

Thursday February 14 2019

 

By Habel Chidawali, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Diwani wa Makole (CCM), Abel Shauri na wenzake watatu wanaokabiliwa na kesi ya kughushi kiwanja cha Waziri Mkuu wa zamani,  John Malecela wamefikishwa mahakamani na kusomewa mashitaka nane.

Washtakiwa hao walikamatwa mwishoni mwa Januari 2019 wakidaiwa kughushi nyaraka na kuuza kiwanja cha Malecela namba 26 kitalu J kilichopo mtaa wa Area D, jijini Dodoma.

Watuhumiwa wengine ni Jackson Ndahani, Shaban Msovela na Elias Stephen.

Washtakiwa hao wamesomewa mashtaka yao leo Alhamisi Februari 14, 2019 mbele ya hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama ya Dodoma, Godfrey Pius, ikielezwa kuwa wametenda kosa hilo kati ya Juni na Agosti 2018 katika mtaa wa Area D.

 

Mwendesha mashtaka wa Serikali,  Lina Magoma ameieleza mahakama kuwa washitakiwa walighushi nyaraka na kubadili jina katika kiwanja kilichokuwa na jina la John S. Malecela chenye ofa namba CDA/ED/LA-15/53243 ya Februari 16, 2010.

Advertisement

Amesema makosa hayo yanaangukia kifungu namba 333 na 335 (b) na 337 vya kanuni ya adhabu sura ya 16 ambapo walimuuzia Godfrey Gao kiwanja walichojua sio mali yao.

Wakili huyo amezitaja kesi nyingine zinazowakabili zenye uhusiano na utapeli ni DOM/IR/1744/2019, DOM/IR/1662/2019 na DOM/R/CIA/PE/14/2017 ambapo zote zinahusiana na utapeli na kujipatia pesa kwa udanganyifu.

Hoja ya wakili wa utetezi, Francis Stephen kuwa wateja wake wapewe dhamana itatolewa uamuzi kesho Februari 15,2019 watakapopelekwa mahakamani kwa ajili ya uamuzi mdogo wa dhamana.


Advertisement