Wanasheria wapinga uamuzi wa Tz kujitoa Korti ya Afrika

Dar es Salaam. Hatua ya Tanzania kujiondoa kwenye itifaki inayowaruhusu wananchi na asasi za kiraia kuishtaki Serikali Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu (ACHPR) kwa ajili ya kutafakari, imepingwa na wanasheria na watetezi wa haki hizo.

Mbali na watetezi hao, Shirika la Kimataifa la Haki za binadamu (Amnesty International) nalo limelaumu uamuzi huo likisema utaathiri harakati za kulinda haki za binadamu.

Barua ya Serikali kwenda Tume ya Umoja wa Afrika iliyosainiwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi Novemba 21, 2019 na iliyothibitishwa na mkuu wa mawasiliano wa wizara hiyo, Emmanuel Buhohela, imeeleza nia ya Tanzania kujiondoa kwenye mahakama hiyo ili kutafakari suala hilo.

Inasema Serikali imechukua uamuzi huo kutokana na kupinga kuwemo kwa kifungu cha 34(6) cha itifaki cha uanzishwaji wa mahakama hiyo.

Inasema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeamua kujiondoa kutokana na kutozingatiwa wazo ililopeleka la kuomba kupitiwa kifungu cha 34(6) cha itifaki ya Mamlaka ya Afrika iliyoanzisha Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu.

“Uamuzi huu umefikiwa baada ya azimio hilo kutekelezwa kinyume na maoni yaliyotolewa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati lilipoletwa azimio hilo. Kwa hiyo hii ni taarifa rasmi ya kujitoa inayotolewa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” inasema sehemu ya taarifa hiyo, ambayo Wizara ya Mambo ya Nje imekiri kuwa ni yake.

Lakini uamuzi huo umekosolewa na wanasheria na watetezi wa haki za binadamu, akiwamo Onesmo Olengurumwa ambaye ni mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC).

“Ni pigo kubwa kwa sekta ya haki za binadamu kwa sababu ukizingatia mahakama zetu zilivyo, wamekuwa wakienda huko lakini hawapati haki,” alisema Olengurumwa.

Huku akitoa mifano ya baadhi ya kesi zilizopelekwa mahakama hiyo na Serikali kushinda, ikiwamo ya marehemu Mchungaji Chritopher Mtikila aliyekuwa akihoji haki ya mgombea binafsi. Olengurumwa alisema Watanzania wanaongoza kwa kupeleka kesi wakiamini watapata haki.

“Utakumbuka Mchungaji Mtikila alikwenda (Mahakama ya Afrika), akapewa haki. Sisi wenyewe tulikwenda kushtaki kuhusu sheria ya vyombo vya habari tukashinda. Mara nyingi kesi zinazokwenda kule zikiwa na haki tunashinda,” alisema.

Alisema licha ya Serikali kutokuwa na tabia ya kutekeleza hukumu za mahakama hiyo, “ile aibu tu ya Serikali kuona kwa nini kesi ishinde (mahakama za ndani), lakini inashindwa kule”. Kwa mfano kesi ya Mchungaji Mtikila Serikali haikutekeleza.

“Hukumu zile hazina nguvu sana, lakini inaonyesha kuna tatizo sehemu na huwa wakikaa kule Addis Ababa (Ethiopia) huwa wanaulizwa kwa nini hamtekelezi uamuzi wa mahakama? Hiyo ndiyo inawasumbua. Nadhani wanataka kuepuka hivyo vitu,” alisema.

Maoni kama hayo yametolewa pia na mwanasheria wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Fulgence Massawe, ambaye alisema ushindi wa kesi wanazopeleka ndiyo umeitisha Serikali.

“Sisi watetezi wa haki za binadamu huwa hatuamini katika kushindwa kesi, kwa kuwa hata tukishindwa tunakuwa tumepeleka ujumbe,” alisema.

“Kwa mfano tulipeleka kesi ya mgombea binafsi tukishirikiana na (Chama cha Wanasheria wa Tanganyika) TLS tukashinda na mpaka leo Tanzania haijatekeleza. Lakini wanajua kuwa wanatekeleza sheria mbovu.

“Mara nyingi Tanzania hatutekelezi hukumu za mahakama za kimataifa na hata za ndani. Uamuzi ule unaifunga nchi lakini hakuna utashi wa kisiasa.”

Massawe alisema mahakama hiyo iliyoanzishwa kutokana na Mkataba wa Haki za Binadamu (Banjul Charter) iliridhiwa na nchi 30 za Afrika huku nchi tisa zikitoa tamko la kukubali kifungu cha 34(6) cha itifaki kinachoruhusu watu binafsi na asasi za kiraia kupeleka mashitaka.

Alitaja baadhi ya kesi zilizopelekwa na watu binafsi na asasi za kiraia kuwa ni pamoja hukumu iliyofuta adhabu ya kifo ya lazima na hukumu ya kina Babu Seya ikisema hawakutendewa haki.

Alisema kesi nyingi zinazoendelea ni za wafungwa wa mauaji wanaoamini kuwa hawakutendewa haki, huku pia kukiwa na kesi za watetezi wa watu wenye ualbino wakidai kuwa Serikali haijachukua hatua za kutosha.

Kesi nyingine imefunguliwa na wakili Jebra Kambole akikosoa matokeo ya urais kutopingwa mahakamani.

Akizungumzia hatua ya Serikali, Kambole alisema amesikitishwa kwa kuwa mahakama ilikuwa kimbilio la Watanzania wengi.

“Mimi nimekuwa `disappointed’ (nimesikitishwa) na uamuzi wa Serikali kwa sababu katika kuheshimu haki za binadamu huwa tunakwenda mbele, lakini kwa kitendo hiki tunarudi nyuma sana kiasi kwamba tunaonekana hatuheshimu haki za binadamu,” alisema Kambole.

Hata hivyo, alisema licha ya Serikali kutaka kujiondoa kwenye kifungu hicho ilichokiridhia mwaka 2010, bado kuna mwaka mmoja mbele wa kuendelea na kesi zilizobaki.

“Sababu ninayoiona, Serikali inashindwa kesi nyingi sana kwa sababu mahakama hiyo ya Afrika iko huru. Inafanya uamuzi kwa mujibu wa sheria, haiingiliwi na mtu yoyote, kila jaji anatoka nchi yake,” alisema.

Kauli hiyo imeungwa mkono na wakili Harold Sungusia ambaye pia anasimamia kesi katika mahakama hiyo

“Mimi nina kesi zangu, nina wateja wangu pale tangu wakati ule wa Mchungaji Mtikila na kuna wastaafu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ninawatetea kule mahakamani. Lakini hilo kusudio la kujiondoa haliwezi kukamilika mpaka baada ya mwaka mmoja,” alisema.

“Ukizingatia kuwa hiyo mahakama iko kwetu na inatoa ushawishi katika ukanda wa Afrika Mashariki, ina fursa nyingi kuliko gharama tutakayoingia kwa kuivuruga hiyo mahakama. Ilitakiwa sisi Tanzania kwa kuwa mahakama iko kwetu tuitangaze kwa nchi nyingine ili zijiunge.”

Nchi jirani ya Rwanda pia imeyojitoa, huku pia Gambia ikiwa imejiunga hivi karibuni.

Mbali na wanasheria hao Shirika la Haki za Binadamu la Kimataifa (Amnesty International) limelaani hatua hiyo kupitia tamko lake juzi.

“Hatua hii ya Tanzania inazuia kabisa watu binafsi na asasi za kiraia kwenda moja kwa moja mahakamani ili kutafuta haki kutokana na ukiukwaji wa haki za binadamu. Hili ni jaribio la dhihaka la kuepuka uwajibikaji,” alisema Japhet Biegon, mratibu wa masuala ya utetezi barani Afrika wa shirika hilo.

Biogon alisema Tanzania ina idadi kubwa zaidi ya kesi zilizofunguliwa na watu binafsi na asasi za kiraia pamoja na hukumu zilizotolewa dhidi yake na Mahakama ya Afrika.