Wapinzani wataka Uchaguzi Mkuu uitishwe upya

Saturday October 31 2020
nyinginepic

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe

Dar es Salaam. Vyama vya ACT Wazalendo na Chadema vimepinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu katika ngazi ya udiwani, ubunge, uwakilishi na urais na kutaka urudiwe.

Vyama hivyo vimetoa tamko lao leo Jumamosi Oktoba 31 2020, ikiwa ni muda mfupi tangu Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imtangaze John Magufuli wa CCM kuwa mshindi wa kiti cha urais wa Jamhuri ya Muungano, na siku kadhaa baaya chombo kama hicho Zanzibar kumtangaza Dk Hussein Mwinyi kua rais wa visiwa hivyo.

Pia tamko hilo limekuja baada ya matokeo ya ubunge kuonyesha kuwa kati ya viti 256, ACT Wazalendo imeshinda viti vinne, CUF vitatu na Chadema kimoja.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati akisoma msimamo wa vyama hivyo, mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema kilichofanyika Oktoba 28 hakina sifa ya kuitwa Uchaguzi Mkuu.

Kutokana na hilo alitaka uchaguzi mkuu kuitishwa upya haraka iwezekanavyo jambo litakaloenda sambamba na kuvunjwa kwa NEC na ZEC na kuunda tume huru za uchaguzi zitakazosimamia uchaguzi huo.

 “Sambamba na hilo tunaomba pia kuwachukulia hatua waliohusika kuharibu mchakato mzima wa uchaguzi mkuu,” alisema Mbowe ambaye amepoteza ubunge wa Hai.

Advertisement

“Sisi kwa umoja wetu tutaendelea kupigania haki za uchaguzi ulio huru, haki na wenye heshima.”

Waraka huo uliosomwa na Mbowe umesainiwa na viongozi wakuu wa chama akiwemo yeye ambaye ni mwenyekiti wa Chadema na Tundu Lissu aliyegombea urais kwa tiketi ya chama hicho.

Pia umesainiwa na Zitto Kabwe ambaye ni kiongozi wa chama ACT-Wazalendo ambaye pia alimsainia Maalim Seif Sharif Hamad ambaye alikuwa mgombea wa chama hicho kwa upande wa Zanzibar aliyeshindwa kufika kwa kile kilichobainishwa kuwa ni sababu za kiusalama.

Advertisement