Wasomi wachambua staili ya Magufuli jukwaani

Monday October 21 2019

 

By Waandishi Wetu, Mwananchi [email protected]

Dar/mikoani. Ziara ya kikazi ya siku nne ya Rais John Magufuli katika Mkoa wa Lindi imeacha mtikisiko huku baadhi ya wasomi wakitaka watendaji wa chini kujifunza kasi ya bosi wao huyo katika utendaji kazi.

Ziara hiyo ilishuhudia mkuu wa wilaya ya Nachingwea, Rukia Muwango na mkurugenzi wa wilaya hiyo, Bakari Bakari wakitenguliwa.

Dk Richard Mbunda, ambaye ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), amesema licha ya kuwepo kwa dosari anazoziona kwa baadhi ya maamuzi ya papo kwa hapo majukwaani, watendaji wanapaswa kumsoma bosi wao.

Katika ziara yake mkoani Lindi, Rais alifanya maamuzi ya papo kwa hapo na wakati mwingine kutumia maneno makali kufikisha ujumbe kwa watendaji wa Serikali, akionyesha kutoridhishwa na utendaji wao wa kazi.

Akiwa Chukuku, Rais Magufuli alimuondoa Kamanda wa Mkoa wa Mtwara wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), RBC Stephen Mafipa kwa kukosekana kwake mkutanoni.

Wananchi walimueleza Rais kuhusu madai yao kuhusu fedha wanazowadai viongozi wa Chama cha Msingi cha Mazao (Amcos) wanaotuhumiwa kutoweka na fedha hizo za wakulima.

Advertisement

Baada ya kupata malalamiko hayo, Rais Magufuli alimuita Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Blasius Chatanda, ambaye alieleza kuwa wanawatafuta watuhumiwa, jibu ambalo halikumfurahisha na kumuita RBC Mafipa.

Hata hivyo, kamanda huyo hakuwepo eneo hilo, hali ambayo ilimuudhi Rais na kumpigia simu mkurugenzi mkuu wa Takukuru, Brigedia Jenerali John Mbungo na kumuelekeza kumuondoa kamanda huyo katika wadhifa wake huo.

Katika ziara hizo, Rais aliwashukia wakurugenzi na watendaji wengine kila alipobaini tatizo likiwamo la matumizi mbaya ya fedha ambazo zililengwa kwenye miradi ya maendeleo hasa maji.

Wasomi wachambua utendaji

Dk Mbunda alisema ziara za Rais zinasaidia kuwakumbusha watendaji wake kama kuna vitu hawakusimamia ipasavyo na pia kutuma ujumbe kwa watendaji wengine nchini.

“ Nature’ (asili) ya Rais Magufuli anapenda kuona kazi zinafanyika na watendaji wake wanawajibika kutekeleza majukumu yao ipasavyo. Rais anataka matokeo kwa wakati,” aliongeza Dk Mbunda.

“Nchi hii ina sera nzuri kwenye makaratasi, lakini utekelezaji tunakuwa nyuma sana. Tumepata mtu anayehimiza uwajibikaji kama Rais Magufuli ndio maana tunamwona kiongozi wa tofauti,” alisema. Hata hivyo, alisema kuna baadhi ya maamuzi ya Rais aliyochukua yanazua shaka na kutolea mfano kutumbuliwa kwa Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Mtwara katika mkutano wa hadhara.

“Tunaona Rais alitangaza amemwondoa kwenye nafasi yake, kimsingi hapa kuna tatizo kwa sababu aliyeondolewa hakupewa nafasi ya kujitetea.”

“Ziara za Rais ni nzuri lakini pale maamuzi yanapofanyika kama yale ya kumuondoa kamanda wa Takukuru ni vizuri sheria, taratibu na kanuni zikafuatwa pamoja na haki ya kusikilizwa ikazingatiwa,” alitahadharisha Dk Mbunda.

Shalom Muzo ambaye ni mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Chuo Kikuu cha Jomo Kenyatta jijini Nairobi, Kenya, alisema watendaji wengi bado hawajamuelewa Rais Magufuli.

Muzo alisema kwa mtendaji yeyote anayepata woga wa kujieleza pale Rais anapofika kwenye eneo lake ni kwamba hatoshi.

“Rais Magufuli anafanya mambo mazuri sana katika nchi ya Tanzania lakini bado kunaonekana kuna walakini kwenye watendaji wake aliowachagua na hii ndio maana amekuwa akiwabadili kula uchao.

Mwanafunzi huyo alisema Rais anatakiwa kuongeza kasi katika yale anayofanya ili watu wabadilike na kwamba anayeshindwa kuwajibika basi ni bora akakaa pembeni.

Muzo ametaka ziara za Rais zisiwatie watu woga bali wanatakiwa wajifunze na kuwajibika ili kuepuka kudhalilika kama ilivyotokea kwa watendaji wengi hivi karibuni.

Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Kukuza Utawala Bora na Uwazi Tanzania (IGT), Edwin Soko alisema kuna baadhi ya wanaoteuliwa wameshindwa kuonyesha kwamba wanaweza kuzitumikia nafasi zao.

Soko ambaye pia ni mchambuzi wa siasa na utawala bora, alisema bado kuna kazi ya ziada kuweza kupata watendaji wenye uwezo.

Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (Sua), Rose Kicheleri alisema changamoto kubwa ni uwajibikaji kwa baadhi ya watendaji wakati mwingine wakurugenzi wanaweza kuwa wanafanya kazi nzuri na kubwa lakini watendaji wake wa chini wakawaangusha.

Alisema wakati mwingine wanalazimika kuwajibika kwa makosa ambayo yamefanywa na watendaji ama wa juu au wale wa chini lakini kulingana na mfumo inakuwa ngumu kumjua aliyefanya kosa hilo.

Alisema kiuhalisia Watanzania hawana utamaduni wa kujituma kufanya kazi na hutokea mara nyingi kiongozi kufanya kazi za wale anaowasimamia.

“Mambo ni `very complex’ (magumu sana) hasa kwenye halmashauri, kuna watu wanafanya kazi kwa woga, pia kuna `lack of accountability’ (kukosekana uwajibikaji) au mtu kutojua anawajibika kwa nani hivyo inakuwa rahisi kutenda makosa halafu akayabeba mtu mwingine,” alisema Kicheleri.

Pia alisema mambo mengine ambayo yanaweza kuwafanya waonekane sio watendaji wazuri ni kutokana na kutokuwapo uwazi katika masuala ya fedha matokeo yake kukwamisha miradi kukamilika kwa muda unaotakiwa.

Alisema pia kuna changamoto ya kiutawala kutokana na kuwepo kwa mianya ya kisheria inayotoa nafasi kwa watu kufanya mambo kinyume na taratibu.

Dk Kicheleri alifafanua kuwa jambo jingine linalosumbua utendaji kazi ni maamuzi ya kisiasa kuingilia masuala ya kiutendaji na kisomi. “Maamuzi ya kisiasa yanawaweka watendaji katika mazingira magumu, naamini wateule wengi ni watu wenye elimu ya kutosha, sema tu mfumo wetu wa kiutawala bado una shida,” alisema Dk Kicheleri.

“Ukimwangalia Rais unaona kabisa alivyo na nia njema na nchi hii, na kila anachokiongea unaona kinatoka moyoni na ana dhamira ya kweli lakini bado kuna mambo ya utawala hayajakaa sawa, hata sheria bado zinatoa mianya ya rushwa,” alisema Kicheleri.

Imeandikwa na Herieth Makweta (Dar), Janeth Joseph (Moshi) na Jesse Mikofu (Mwanza).

Advertisement