Watano wakamatwa kwa tuhuma za kumuua mwanajeshi Tabora

Mkuu wa Polisi wa wilaya ya Tabora OCD, George Bagiyemu akizungumzia kuhusu ulinzi shirikishi leo mjini Tabora. Picha na Robert Kakwesi.

Muktasari:

Kuuawa kwa askari JWTZ,watu watano wanashikiliwa na Jeshi la Polisi hadi sasa ambao wanaendelea kuhojiwa na Polisi mjini Tabora.

Tabora. Kutokana na kuuawa askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) usiku wa kuamkia juzi jumla ya watu watano wamekamatwa wakituhumiwa kuhusika na mauaji hayo.
Mwanajeshi huyo, Samwel Machugu (28) aliuawa na watu wanaodhaniwa vibaka wakati akienda nyumbani kwake baada ya kushiriki ulinzi shirikishi.
Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Komanya Kitwala amesema watuhumiwa waliokamatwa wanaendelea na mahojiano kabla ya hatua zaidi kuchukuliwa kwa jalada lao kupelekwa ofisi ya Mkurugenzi Mashtaka (DPP).
Aliwataka wananchi kutulia kwa vile Jeshi la Polisi Wilaya ya Tabora lipo imara na waendelee na majukumu yao huku wakijiepusha na ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya corona kwa kufuata maelekezo yanayotolewa na wataalamu.
Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Tabora (OCD), Goerge Bagiyemu amesema wameviimarisha vikundi vya ulinzi shirikishi ambavyo mwanzoni vililegalega na kuvipatia tochi kwa ajili ya kuvisaidia katika shughuli za ulinzi.
Amesema washiriki wa vikundi wamefanyiwa uchunguzi wa kina ili wasiwepo watu wenye lengo baya kwa kutumia nafasi hiyo kufanya vitendo kinyume na sheria.
Mwanajeshi Samwel Machugu aliagwa jana Jumanne Machi 31 na jioni kusafirishwa kwenda Tarime mkoani Mara kwa maziko.
Marehemu aliajiriwa mwaka 2015 na amefariki akiacha mtoto wa miezi sita na mke ambaye wameishi naye kwa miezi minne tangu wafunge ndoa mwezi Novemba mwaka jana.