Watanzania 30 waliorejeshwa kutoka Afrika Kusini wahukumiwa kifungo, kulipa faini

Muktasari:

Watanzania 30 waliorejeshwa nchini kutoka Afrika Kusini wamehukumiwa kifungo au kulipa faini baada ya kutiwa hatiani kwa shtaka la kuondoka Tanzania kinyume na sheria ya uhamiaji.

Dar es salaam. Watanzania 30 waliorejeshwa nchini kutoka Afrika Kusini wamehukumiwa kifungo au kulipa faini baada ya kutiwa hatiani kwa shtaka la kuondoka Tanzania kinyume na sheria ya uhamiaji.

Washtakiwa hao wamesomewa mashtaka yao leo Alhamisi Januari 23, 2020 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na mahakimu wawili tofauti.

Mbele ya Hakimu Mkazi mwandamizi, Agustina Mbando wakili wa Serikali, Godfrey Ngwijo amedai washtakiwa 16 waliondoka Tanzania kinyume  na kanuni za uhamiaji namba 20 (3) (a)  G.N namba 657 ya mwaka 1997 na kufanyiwa marekebisho mwaka 2016.

Amesema kuwa Januari 21, 2020 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) walikutwa wakiwa wametoka nje ya nchi bila kufuata utaratibu kupita mipaka isiyojulikana.

Washtakiwa wote 16 walikubali mashtaka yao na upande wa mashtaka kuwasomea maelezo ya awali kwamba katika tarehe zisizofahamika waliondoka Tanzania kwenda Afrika Kusini bila kufuata utaratibu.

Ngwijo amedai katika tarehe hizo, washtakiwa walikamatwa Afrika Kusini na kuletwa Tanzania, walipofika JNIA walipelekwa ofisi ya Mkoa wa Dar es Salaam kuchukuliwa maelezo.

Amewataja washtakiwa hao kuwa ni Omary Kaulu, Dominic Fabric, Sefu Mohammed, Hamad Hashiri, Asbawi Omar, Abdala Hamad, Razan Ally,

Wengine ni Moosa Salimu, Mawki Ally, Daniel Joshua, Amari Abduli, Abdullah Ramadhan, Mohammed Tuwa, Aziz Mohammed, Rajabu Shamanism na Adam Seifu.

Akiwasomea hukumu,  Hakimu Mmbando amesema kutokana na makosa hayo kujirudia kila mshtakiwa atatakiwa kutumikia kifungo cha miezi sita jela au kulipa faini ya Sh300,000.

Kabla ya kutolewa adhabu hiyo wakili wa Serikali, Godfrey Ngwijo aliiomba mahakama hiyo kutoka adhabu kali kwa washtakiwa kwa sababu utaratibu wa kutoka nje ya nchi unafahamika.

Washitakiwa hao waliiomba mahakama kuwapunguzia adhabu kutokana na kuwa wamekaa gerezani walipokuwa Afrika Kusini.

Mbele ya Hakimu Mkazi mwandamizi, Salum Ally washtakiwa wengine 14 walihukumiwa kutumikia kifungo cha miezi 18 jela  au kulipa faini ya Sh50,000 baada ya kukiri kosa hilo.

Washtakiwa hao ni  Adam Luzz, Suleiman Saidi, Kapaya Fredric, Semboko Abubakari, Mambosasa Francis, Juma Muhina, Chale Othoman, Salehe Iddy, Mohammed Kassim, Hassan Ally, Boban Abed, Abdul Kessy, John Joseph na Mawazo Frank.

Baadhi ya washtakiwa wamelipa faini na kuondoka mahakamani hapo na baadhi walishindwa na kupelekwa gerezani.