Watanzania waishio Afrika Kusini wazungumzia machungu ya corona

Saturday March 28 2020

 

By Elizabeth Edward, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Baadhi ya watanzania  waishio  nchini Afrika Kusini  wamesema hatua ambayo nchi hiyo inapitia kwa sasa ni mbaya kiuchumi na hawatamani kuona Tanzania ifike huko.

Kauli hiyo  imekuja siku moja baada ya kuanza kutekelezwa kwa agizo la shughuli zote kufungwa kwa muda wa siku 21 na watu kutakiwa kukaa  nyumbani ili kupunguza kasi ya kusambaa kwa virusi vya corona.

Agizo hilo lililotolewa Machi 24,2020 na Rais wa nchi hiyo Cyril Ramaphosa limeanza kutekelezwa jioni ya Machi 26,2020 wakati maambukizi yalifikia watu 927 ambapo ndani ya saa 24 waliambukizwa watu 218.

Mmoja wa Watanzania hao Rahim Mohamed alisema mchana wa Alhamisi sehemu mbalimbali za huduma zilifurika watu wakijaribu kununua mahitaji ya muhimu kabla ya kuanza kwa agizo hilo.

“Kiukweli sio jambo zuri watu wanajaribu kukusanya mahitaji, matokeo yake foleni inakuwa kubwa kwa kifupi naweza kusema hatuko sawa. Wapo wanaohofia kupoteza vibarua vyao.”

“Ukiacha hayo licha ya lockdown kuja kipindi ambacho watu wamepata mshahara lakini wapo wengi wanaotegemea shughuli za kila siku, kazi za vibarua na wapo wanaofanya kazi kwa masaa zote hizo zimesitishwa,” alisema Rahim anayeishi katika kitongoji cha Midrand mjini Johansburg.

Advertisement

Alisema kamwe hatamani kuona Tanzania imefikia hatua hiyo kwa kuwa ina athari kubwa na inaweza kusababisha watu wengi kuwa na maisha magumu.

“Nasisitiza Watanzania wenzangu wachukue tahadhari, huu ugonjwa upo ninachokishuhudia huku nisingetamani kuona kinafika Tanzania.

“Najua maisha yetu ya kubangaiza ni lazima watu watoke ndiyo wapate kula sasa shughuli zote zikisimamishwa itakuwa balaa, Afrika kusini kidogo wana uwezo lakini bado wanalia,” alisema Rahim.

Kwa upande wake Jaffary Abdul anayeishi mjini Durban alisema wasiwasi mkubwa ni kwa wale ambao vipato vyao  vinatokana  na kufanya kazi kila siku.

Alisema changamoto kubwa aliyonayo ni kuhakikisha anaweza kujibana katika siku hizo ili akiba aliyonayo iweze kufika siku 21 zilizotangazwa na serikali.

“Maisha ya huku hayana tofauti na nyumbani Tanzania wengi tunategemea tutoke ndio tupate riziki sasa hii lockdown ya siku 21 ni balaa.”

“Hatuna budi kumuomba  Mungu atuepushie hali hii isidumu kwa muda mrefu, huko nje ni polisi na wanajeshi ndio wapo kuhakikisha hakuna anayetoka bila sababu ya msingi,” alisema Abdul.

Afrika Kusini iliyotangaza mgonjwa wa kwanza wa corona Machi 5, 2020  inaongoza orodha ya nchi za Afrika zenye maambukizi mengi ikiziacha  kwa mbali Misri yenye wagonjwa 456 na Algeria yenye wagonjwa 367.

Misri ilikuwa nchi ya kwanza Afrika kuwa na mgonjwa mwenye virusi vya corona aliyetangazwa Februari 14, ikifuatiwa na Algeria ambayo mgonjwa wake wa kwanza alibainika Februari 25.

 

Advertisement