Watu 13 wakamatwa kwa kukwepa karantini

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Albert Chalamila ,(katikati) akiangalia moja ya vitakasa mikono kati 150 vilivyotolewa na Wizara ya Afya  kilichoshikwa na Balozi wa Kampeni ya kitaifa ya "Mikono salama,Nyumba Salama,Tanzania Salama, " iliyoanza Leo mkoani Mbeya, Mrisho Mpoto, (kushoto,)  wa kwanza kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Usafi na Mazingira kutoka Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia, Wazee  na Watoto, Anyitike Mwakitalima. Picha na Hawa Mathias.

Muktasari:

  • Raia 13 wa kigeni wadakwa Mbeya baada ya kubainika kutaka kukwepa kuhifadhiwa kwenye karantini

Mbeya. Serikali mkoani Mbeya imewakamata raia 13 walioingia nchini kupitia mipaka ya nchi jirani kutaka kukwepa kuhifadhiwa kwenye karantini kwa siku 14 kwa ajili ya kupimwa afya zao kama wanaweza kuwa na viashiria vya maambukizi ya virusi vya corona.


Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila amesema hayo leo Aprili 6, 2020 wakati akipokea vitakasa mikono 150 kutoka Wizara ya Afya ikiwa ni siku ya kwanza ya kuanza kampeni ya kitaifa ya kuhamasisha jamii kunawa mikono kwa maji tiririka.


Amesema Serikali imejipanga kikamilifu katika mipaka yote ya nchi jirani na za Malawi na Zambia na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe(SIA) kwa kuhakikisha raia wote wanaiongia wanakaa karantini siku kwa 14.


"Nimebaini kuna kamchezo kanafanywa sasa kama kiongozi wa Serikali nitapambana kuhakikisha hakuna raia anayeingia bila kukaa karantini atakayebainika atawekwa mahabusu kwani tayari tumetengeneza maeneo ya kuwahifadhi kwa siku 14,"amesema.


Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Usafi na Mazingira Wizara ya Afya, Anyitike Mwakitalima amesema wizara imenzisha kampeni hiyo lengo ni kuwafikisha wananchi elimu ya kujikinga na ugonjwa wa corona.