Watu 666 wajiua ndani ya miaka minne Tanzania

Muktasari:

Wengi wanaojiua hutaja sababu za kimapenzi, kuugua kwa muda mrefu bila kupata dalili ya kupona, maisha magumu na ugomvi wa familia.

Dar es Salaam. Watu 666 wamejiua kwa kipindi cha miezi sita ya mwaka tangu 2016 hadi 2019, Jeshi la Polisi Tanzania limeeleza.

Akizungumza na jana Jumanne Septemba 10, 2019 katikia redio ya Clouds FM ikiwa ni siku ya kupinga kujiua duniani, Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania, David Misime alisema kwa miaka minne Januari mpaka Juni, jumla ya watu waliojiua kwa sumu walikuwa 75, kwa kujinyonga walikuwa 367, kujipiga risasi watano na kwa kisu walikuwa 219.

“Tanzania kuna vitendo kama vivyo vya watu kujiua, takwimu zetu zinaonyesha tangu Januari 2016, watu waliojiua kwa sumu walikuwa 30, waliojinyonga 101, waliojiua kwa kujipiga risasi hawakuwepo na kwa kutumia kisu walikuwa 131,” alisema Misime  

Kwa mwaka 2017, waliojiua kwa kunywa sumu walikuwa 16, waliojinyonga walikuwa 71, waliojipiga risasi alikuwa mmoja na waliojiua kwa kisu walikuwa 88.

Kwa mwaka 2018 alisema waliojiua kwa kunywa sumu walikuwa 21, waliojinyonga 90 na waliojipiga risasi walikuwa wawili.

“Mwaka huu 2019 waliokunywa sumu inaweza kuwa dawa, sumu ya kuulia wadudu aya kuulia magugu na kadhalika, kuanzia Januari hadi Juni 8, kujinyonya 105, kujipiga risasi walikuwa wawili,” alisema.  

Akieleza sababu za watu kujiua, Misime alisema japo wengi huwa hawaachi sababu na wachache wanaoacha ujumbe hutaja sababu za kukataliwa kimapenzi, wengine wanasema wameugua muda mrefu na hawaonyeshi dalili za kupona na wengine hutaja sababu za maisha magumu.

“Wengine ni ugomvi wa kifamilia labda amedhulumiwa mali au ameambiwa jambo baya. Kama tungechukua hizi takwimu kwa mwaka mzima zingeonekana kama ni kubwa zaidi,” alisema.

Aliwataka wanajamii kuwasaidia watu kuachana na msongo wa mawazo kwa kuwapeleka kwa wataalamu wa saikolojia kupata ushauri.