Waziri Ndalichako awataka wanasayansi kubadilishana mbinu

Waziri wa Elimu nchini Tanzania, Profesa Joyce Ndalichako

Muktasari:

Waziri wa Elimu nchini Tanzania, Profesa Joyce Ndalichako amewataka wanasayansi duniani kubadilishana mbinu za utafiti wa teknolojia na ubunifu kuboresha uchumi wa Tanzania.

Dar es Salaam. Waziri wa Elimu nchini Tanzania, Profesa Joyce Ndalichako amewataka wanasayansi duniani kubadilishana mbinu za utafiti wa teknolojia na ubunifu kuboresha uchumi wa Tanzania.

Ametoa kauli hiyo jana Jumatatu Novemba 11, 2019 jijini Dar es Salaam wakati akifungua mkutano  wa mwaka wa baraza la udhamini wa sayansi Afrika, kuahidi kuwa  Serikali itaendelea kufadhili miradi ya utafiti wa sayansi nchini.

“Kwanza kuwe na kubadilishana wataalamu wa utafiti wa sayansi, wabadilishane matokeo ya utafiti wa sayansi na machapisho na kuwe na semina na mafunzo ya teknolojia.”

 “Sayasi na teknolojia ndio chanzo cha ukuaji wa uchumi kwa kuwa ndio chanzo cha kuongezeka kwa uzalishaji na ushindani wa biashara na ndio chanzo cha ajira,” amesema Profesa Ndalichako.

Ameongeza, “utafiti wa kisayansi una nafasi kubwa katika maendeleo ya jamii na uchumi katika jamii yoyote.”

“Serikali itaendelea kufadhili miradi ya utafiti na ubunifu wa sayansi kupitia mfuko wa utafiti wa sayansi na teknolojia unaosimamiwa na Tume ya Sayansi na Teknolojia (Cosetch).”

Mkurugezi wa Costech, Dk Amos Nungu amesema baraza hilo lina lengo la kuimarisha uwekezaji katika sayansi kwa nchi za Jangwa la Sahara ikiwa ni pamoja na kufadhili utafiti na kusaidia kuweka sera zitakazoleta maendeleo ya uchumi.

Mkakati huo unafadhiliwa na Shirika la kimataifa la Maendeleo la Uingereza (DFID); Shirika la Maendeleo la kimataifa la Canada (IDRC), taasisi ya Taifa ya Utafiti ya Afrika Kusini (NRF) na Shirika la kimataifa la Maendeleo la Sweden (Sida).

Mkutano huo unahusisha washiriki kutoka nchi 15 ambazo ni Botswana, Burkina Faso, Ivory Coast, Ethiopia, Ghana, Kenya, Malawi, Namibia, Msumbiji, Rwanda, Senegal, Tanzania, Uganda, Zambia na Zimbabwe.

Pia wawakilishi kutoka Guinea, Sweden, Ujerumani, Marekani, Uingereza, Brazil, India, Japan na Ufaransa nao walishiriki mkutano huo.