KALAMU HURU: Waziri anapoomba msamaha kwa Rais, kwa wananchi kumchagua mpinzani

Wednesday October 9 2019

 

By Elias Msuya

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Michezo na Wasanii, Juliana Shonza ameibua mjadala baada ya kumwomba msamaha Rais John Magufuli kwa sababu wananchi walichagua Mbunge wa upinzani na kuahidi kuwa kosa hilo halitarudiwa tena katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

Alitoa kauli hiyo Oktoba 6, wakati Rais Magufuli akiwa njiani kuelekea mkoani Rukwa akiwa katika jimbo la Momba mkoani Songwe.

Jimbo la Momba linashikiliwa na David Silinde wa Chadema. Pengine kwa kujikomba na kujipendekeza mbele ya Rais, Shonza akaona aibu kumweleza kuwa jimbo hilo ni la upinzani, hivyo akaomba msamaha.

Kwa maana nyingine Shinza hakumbuki kwamba Katiba ya Jamhuri ya Muungano inaitambua Tanzania kuwa inafuata mfumo wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa na ndiyo maana kuna sheria na kanuni zinazosimamia mfumo huo.

Wananchi wametumia haki yao ya kidemokrasia kumchagua mchunge wa chama wanachokitaka, halafu mtu mwingine anakuja kuomba msamaha kwa chaguo la wananchi?

Ingeeleweka kama Shonza angekuwa anajieleza ndani ya kikao cha chama chao ambacho hutumika kupanga mikakati ya ushindi. Lakini anapoomba msamaha mbele ya Rais ambaye ni kiongozi wa wananchi wote, anataka kuelewekaje kama siyo kuonyesha ubaguzi wa kisiasa?

Advertisement

Rais magufuli ambaye mara kwa mara amekuwa akisema maendeleo hayana chama, alipaswa kumkemea pale pale kwa sababu yeye ndiyo mlinzi wa Katiba ya nchi inayotambua mfumo wa vyama vingi.

Tatizo linalojionyesha ni kwamba baadhi ya viongozi wanashindwa kumtofautisha Rais na Mwenyekiti wa CCM. Pamoja na kwamba anavaa kofia mbili, lakini Rais anapokuwa kwenye ziara za kiserikali ni kiongozi wa wote.

Wananchi wana haki ya kudai maendeleo kwa Serikali na kwa Rais hata kama walichagua mbunge au diwani wa chama kingine, kwa sababu huyo ni Rais wa wote.

Wananchi hao hata kama ni wapinzani ndiyo wanaiolipa kodi na kodi hiyo ndiyo inatumika kugharamia miradi ya maendeleo. Siyo fedha ya Rais wala siyo ya CCM.

Wananchi wanalipa kodi ya mishahara, wanalipia kodi ya ongezeko la thamani, wanalipia ushuru wa mazao, wanalipia michango mingi tu ambayo inachukuliwa na Serikali. Watakuwa na kosa gani wakidai maji, umeme, barabara na afya?

Siyo kazi ya Mbunge kugharamia miradi hiyo, bali kazi ya Mbunge ni kwenda kuwasemea bungeni. Bajeti ikipitishwa Serikali ndiyo inayotekeleza.

Kitendo cha Waziri Shonza kumwomba msamaha rais ni dalili kwamba hata mfumo wenyewe wa vyama vingi ni kosa la jinai.

Ni bahati mbaya sana kwamba hata mfumo wenywe unavurugwa tu kwa makusudi. Kumekuwa na vitendo vinavyotafsiriwa kuwa ni vya kubagua watu kutokana na ufuasi wao wa vyama, huku vyombo vya Dola vikionekana kuipendelea CCM na kunyanyasa vyama vya upinzani.

Ni wajibu wa viongozi wa Serikali kuiheshimu Katiba ya Jamhuri ya Muungano inayotambua mfumo wa vyama vingi na kuheshimu uamuzi wa wananchi katika kuchagua viongozi wao.

Advertisement