Yanga yaifuata Pyramids na tumaini jipya Cairo

Muktasari:

Licha ya Yanga kuondoka na matumaini ya kupindua matokeo ugenini, lakini rekodi zinaonyesha miamba hiyo ya Tanzania haijawahi kushinda Misri.

Dar es Salaam. Nahodha msaidizi wa Yanga, Juma Abdul amesema kupoteza nyumbani dhidi ya Pyramid hakujawakatisha tamaa katika mchezo wao wa marudiano utakaofanyika Jumapili jijini Cairo.

Yanga inakwenda Misri katika mchezo wake wa marudiano wa kusaka kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika ikiwa na kumbukumbu ya kufungwa mabao 2-1 na Pyramids katika mechi iliyofanyika Mwanza siku nne zilizopita.

Akizungumza Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, nahodha msaidizi Abdul amesema mpira ni dakika 90 na wanatambua mchezo utakuwa mgumu, lakini wana imani ya kushinda baada ya kujua kilichowafanya wapoteze nyumbani.

"Ukweli mechi itakuwa ngumu, lakini tutapambana kadri tutakavyoweza kuhakikisha ushindi tunaupata kama wao walitushinda kwetu na sisi tunaweza kuwafunga kwao."

"Tunajua wapinzani wetu ni wazuri eneo gani na wanamapungufu eneo lipi, tutajitolea kwa kadri tutakavyoweza kuhakikisha tunaiwakilisha Tanzania kwa ushindi."

"Faida nyingine tutakayoipata wakijiamini kupita kiasi basi itaturahisishia sisi kupata matokeo kirahisi tuna morali ya kutosha kuhakikisha tunafanya kitu katika mechi hiyo," alisema Abdul.

Kipa wa timu hiyo, Metacha Mnata alisema wanakwenda na akili ya ushindi licha ya kwamba walipoteza mchezo wa nyumbani.

Metacha alisema Pyramid si timu ya kubeza hivyo watakwenda kucheza kwa umakini na kutorudia makosa waliyofanya Uwanja wa CCM Kirumba yajirudie Cairo.

"Tumejipanga kwenda kuiwakilisha Tanzania kwa ushindi kwani sisi ndio tumebakia katika mashindano ya kimataifa, mchezo utakuwa mgumu ila tutajituma kwa kadri tuwezavyo kupata ushindi."

"Dua za Watanzania ni muhimu ila na sisi kwa upande wetu tutakwenda kujitolea kwa nguvu zetu zote," alisema Mechata.

Yanga ndio timu pekee ya Tanzania iliobaki kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, baada ya Simba kutolewa hatua ya awali na UD Songo ligi ya Mabingwa, KMC AS Kigali ya Rwanda na Azam FC ikitolewa na Triangle FC ya Zimbabwe.