Zitto awachangia Chadema Sh2 milioni

Wednesday March 11 2020
pic act mchango

Dar es Salaam. Kiongozi wa Chama cha ACT -Wazalendo,  Zitto Kabwe ameichangia Chadema  Sh2 milioni ili zitumike kuwalipia faini viongozi wanane wa chama hicho.

Viongozi hao akiwemo mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe jana Jumanne Machi 10, 2020 walihukumiwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kulipa faini ya Sh350 milioni au kwenda jela miezi mitano baada ya kutiwa hatiani  katika mashtaka 12 kati ya 13 yaliyokuwa yakiwakabili.

Kutokana na jana jioni kushindwa kukamilisha taratibu za kulipa fedha hizo, walipelekwa katika gereza la Segerea, huku taratibu za kuwatoa zikifanywa na Chadema kuanza kuchangishana fedha kuwatoa.

Leo Jumatano Machi 11, 2020 Zitto aliyewahi kuwa naibu katibu mkuu wa Chadema kabla ya kufukuzwa, alifika makao makuu ya chama hicho mnamo saa 9 alasiri na kutoa mchango wake na kuondoka.

Mkurugenzi wa Itikadi, uhusiano na mambo ya nje wa Chadema, John Mrema amesema mbali ya kutoa fedha hizo,  Zitto ameahidi kuhamasisha wanachama wa ACT-Wazalendo  kuchangia Chadema.

Tangu jana Zitto aliandika kwenye ukursa wake wa Twitter akisisitiza kushirikiana na Chadema kuhamasisha wananchi kuchangia faini hiyo.

Advertisement

Akifafanua kuhusu michango hiyo Mrema amesema imetoka kwa watu mbalimbali bila kujali itikadi zao.

"Wapo wanachama, wapo watumishi wa umma, wengine ni wana CCM. Tutatoa idadi kamili ya wachangiaji lakini hatutatoa majina ili kulinda siri za wachangiaji," amesema Mrema.

Wakusanya 234 milioni

Akizungumza na waandishi wa habari leo Makamu Mwenyekiti wa Chadema Zanzibar, Said Issa Mohammed amesema hadi leo saa 8 mchana wamekusanya Sh234.6 milioni na kati ya fedha hizo Sh176.94 milioni  zimechangwa kwa simu, Sh52.74 milioni zimechangwa kupitia benki na Sh 4.7 milioni zimechangwa kama fedha taslim.

"Tulipotangaza jana kuchangia, mwitikio umekuwa mkubwa. Kuna wengine wameuza kuku zao, mayai, nyama. Tumepata jumla Sh234,469,000," amesema Mohammad
Amesema kati ya fedha hizo wametumia Sh100 milioni kulipa mahakamani na kupata code number ya washitakiwa
"Mawakili wetu wapo tumepata remove order ya kuwatoa wabunge wanawake. Halima Mdee gharama yake Sh40 milioni, Esther Matiko Sh30 milioni na Esther Bulaya Sh30 million," amesema

Advertisement