Mke wa Babu Seya ataka Watanzania kuwaombea maisha mema

Muktasari:

Jana Jumamosi Septemba 7, 2019 katibu tawala Wilaya ya Muheza, Desderia Haule alifunga ndoa na mwanamuziki Nguza Viking ‘Babu Seya’ katika Kanisa Katoliki Sinza, jijini Dar es Salaam.

Muheza. Jana Jumamosi Septemba 7, 2019 katibu tawala Wilaya ya Muheza, Desderia Haule alifunga ndoa na mwanamuziki Nguza Viking ‘Babu Seya’ katika Kanisa Katoliki Sinza, jijini Dar es Salaam.

Picha za wanandoa hao wakiwa kanisani na baadaye ukumbini ziliibua mjadala mitandaoni lakini leo Jumapili Septemba 8, 2019, Desderia akizungumza na Mwananchi amewataka Watanzania kuwaombea kwa kuwa wamekabidhi maisha yao kwa Mungu.

Amesema si vyema kuhoji lini walianza mahusiano, walikutana wapi, “Watuombee maisha mema na mume wangu. Tumeamua kuyasalimisha maisha yetu kwa Mungu. Tunashukuru ndoa yetu ilifanyika kwa amani na utulivu wa hali ya juu.”

Amebainisha kuwa ndoa haitakuwa kikwazo katika kutekeleza majukumu yake, itamfanya aongeze juhudi zaidi.

Kwa upande wake Nguza amemshukuru Rais wa Tanzania, John Magufuli kwa mema aliyomtendea kwa kuwa ndoa hiyo imetokana na huruma za kiongozi mkuu huyo wa nchi.

“Kwanza namshukuru Mungu kwa kuniwezesha kufunga ndoa hii na pili. Namshukuru Rais Magufuli kwa kunitoa gerezani mimi na mwanangu (Papii Kocha). Kama si  yeye tungefia huko na ndoa hii isingefungwa,” amesema Nguza.

Amesema mkewe ataishi kwenye kituo chake cha kazi wilayani Muheza, yeye muda mwingi atakuwa Dar es Salaam katika shughuli zake za muziki.

Amebainisha kuwa atakuwa akimfuata mkewe wilayani humo, “Kuna muda nitakuwa nakaa kwa mke wangu Muheza. Niwaombe shemeji zangu wa Muheza mniandalie machungwa na mafenesi huko lakini muda mwingi nitautumia huku Dar es Salaam kwenye shughuli zangu za muziki.”

Babu Seya na mwanaye Johnson Nguza ‘Papii Kocha’ walikuwa wakitumikia kifungo cha maisha jela na waliachiwa kwa msamaha wa Rais alioutoa Desemba 9,2017 wakati wa maadhimisho ya miaka 56 ya Uhuru wa Tanganyika.

Walikuwa wakishikiliwa katika Gereza la Ukonga na walikuwa miongoni mwa wafungwa 8,157 wakiwemo wa vifungo vya maisha na waliohukumiwa kunyongwa hadi kufa waliopata msamaha wa Rais.

Wawili hao walikaa gerezani kwa takriban miaka 13 na miezi minne baada ya kutiwa hatiani na kuhukumiwa adhabu hiyo kwa kosa la kubaka na kulawiti watoto 10 waliokuwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Mashujaa iliyopo Sinza, Dar es Salaam.