Wananchi Buguruni walia kuuziwa samaki wanaovuliwa kwenye maji yenye kinyesi

Dar es Salaam. Wakazi wa Buguruni Mivinjeni wamesema kuna watu wasio waaminifu wamekuwa wakivua samaki katika mabwawa yanayohifadhi kinyesi na kwenda kuwauza katika masoko mbalimbali jijini hapa.

Walieleza hayo jana wakati ziara ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mussa Zungu alipowatembelea kujua changamoto zinazowakabili kwa kuwa wanaishi karibu na mabwawa matatu yanayotumika kuhifadhi majitaka yakiwemo ya kinyesi.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Buguruni Mivinjeni, Fadiga Legele alimwambia Zungu kuwa wakazi wa maeneo yanayozunguka mabwawa hayo wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo harufu kali inayotoka nyakati za usiku.

“Kipindi cha nyuma yalikuwa yanafanyiwa usafi na kuwekwa dawa lakini takriban miaka saba hawajafanya hivyo. Jambo jingine kuna watu wasio waaminifu wanavua samaki wakati wa usiku.

“Tumekuwa tukipata shida sana kuwakamata watu hawa wanaojishughulisha na uvuvi wa samaki aina ya perege. Kutokana na hali hali ya mabwawa haya tunaamini wananchi wanaokula samaki hawa wanakwenda kuathirika,” alisema Legele.

Mbali na hilo, mwenyekiti huyo alisema mtaa huo unakabiliwa na changamoto ya utiririshaji wa majitaka, licha ya kupeleka maombi ramsi kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa) kupelekewa mradi maalumu wa mifereji ili kuondoa changamoto hiyo.

Pili Pazi, mkazi mwingine wa eneo hilo aliungana na Legele akisema samaki hao si salama kwa afya ya binadamu na kwamba ukiwaona ni vigumu kubaini kama wamevuliwa katika mabwawa yanayohifadhi kinyesi eneo la Buguruni.

Mkurugenzi wa idara ya Majitaka Dawasa, Lydia Ndibalema alisema mabwawa hayo hayawekwi dawa bali ni mfumo unaojisafisha wenyewe kwa kutumia wadudu, lakini kinafofanyika, wanapunguza tope linapozidi ambalo linasababisha mfumo usifanye vizuri.

Kwa upande wake, Zungu aliagiza kuweka kwa dawa katika mabwawa hayo ili kuzuia uwezekano wa watu hao kuvua samaki katika eneo hilo.

“Kinga ni bora kuliko tiba, watu wanakuja wanachukua samaki na wanawapeleka sokono kuwauzia watu. Watu wanaugua Serikali inapata gharama ya kuwatibu.

“Watu wakipata ugonjwa wa matumbo Serikali inawatibu na imekuwa hodari, lakini gharama zinazidi kwa sasabu ya uzembe unaoonekana hapa. Mkiua samaki hawa na dawa hakuna atakayekuja kuvua hapa,” alisema Zungu.

Hata hivyo, Zungu alitumia nafasi hiyo kuupongeza uongozi na Serikali ya Mtaa wa Mivinjeni kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuwazuia watu wasivue samaki wanaopelekwa katika masoko.