Ajirusha akiwa uchi kwenye kundi la simba

Monday May 23 2016

Franco Luis akishambuliwa na simba kabla ya

Franco Luis akishambuliwa na simba kabla ya kuokolewa na askari wa bustani ya wanyama.  Picha na Dailymail 

Chile. Ukistaajabu ya Mussa utayaona ya Firauni,  kijana mmoja aliyefahamika kwa jina la Franco Luis ameshambuliwa na kundi la simba baada ya kujirusha ndani ya bustani ya wanyama hao akiwa uchi.

Luis  aliwaacha mdomo wazi watu waliofurika kwenye bustani hiyo ya Santiago  mwishoni mwa wiki ambao wengi waliambatana na  familia zao.

Kwa mujibu wa gazeti la Daily Mail la Uingereza, kijana huyo mwenye miaka 20, alikimbizwa hospitali baada ya walinzi wa bustani hiyo kumuokoa kwa  kuwaua simba wawili waliokuwa wanamshambulia.

Uongozi wa bustani hiyo ulithibitisha tukio hilo na kudai kwamba kijana huyo alishambuliwa akiwa uchi wa mnyama baada kuvunja uzio na kuingia kwenye kundi hilo.

Mkurugenzi wa Santiago Alejandra Montalva alisema walijua kijana huyo aliingia  kwenye bustani hiyo kama wateja wa kawaida wanavyolipa tiketi  kwa lengo  la kutembelea hapo.

‘‘Baada ya kufanya malipo kama mteja wa kawaida kijana huyo hakupita kwenye njia inayotumiwa na wateja bali aliezua paa la simba hao na kutumbukia ndani na kuanza kushambuliwa,’’ alisema

Advertisement

Alisema ni kitendo cha kushangaza kwani kila mtu alishikwa na bumbuwazi baada ya kumuona kijana huyo akijirusha kwenye kundi hilo la simba na kuanza kupigana nao.

Alisema askari wa bustani hiyo walitumia nguvu za ziada kuhakikisha wanaokoa maisha ya kijana huyo, ambaye hawajafahamu fika kama alikuwa na akili timamu.

 Atoa sababu

 Kwa upande wake kijana huyo alisema alifanya kitendo hicho cha kustaajabisha kila mtu kutokana na ufunuo alioshushiwa na  Mungu.

Shuhuda

Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Cynthia Vasquez alisema  baada ya Luis kujirusha ndani ya bustani hiyo, simba waliokuwa ndani hawakumdhuru kwanza.

“Cha kushangaza simba hao walianza kucheza naye,”alisema Vasquez

 Vasquez ambaye alikuwa miongoni mwa wageni waliotembelea bustani hiyo, alisema baada ya dakika chache   Lius alisikika akipiga kelele. “Walianza kumrarua...alipiga kelele aliita jina la Yesu,”alisema.                       

Alisema kelele hizo ziliwavuta watu wengi ambao walifika kushuhudia tukio hilo.

Vasquez alisema walinzi waliofika kuokoa maisha ya Luis walilazimika kufyatua risasi juu ili kuwatawanya watu. “Waliingia baada ya kuwaua simba hao na kumtoa Luis ambaye alikuwa ameshajeruhiwa vibaya,” alisema.

Baba aongea

Baba mzazi wa Luis alisema  alishaanga kusikia watu wanapiga kelele na alipofika katika eneo la tukio alimkuta kijana wake akiwa amejeruhiwa vibaya na simba.

Advertisement