Prime
Alikiba alivyoruka kiunzi kilichowashinda wengi!
Muktasari:
- Wimbo Mahaba, kwa ujumbe wa kutafakarisha kuhusu mapenzi, unasimulia hadithi ya maisha ya uhusiano, ukionyesha zaidi matokeo ya hadithi hiyo na kusisitiza kwamba hakuna haja ya kuogopa kuingia kwenye mapenzi, hivyo kuwa huru kupenda.
Dar es Salaam. Mwimbaji wa Bongofleva kutokea Kings Music, Alikiba kupitia wimbo wake maarufu, Mahaba (2023), amefanikiwa kuruka kiunzi ambacho kimewashinda wasanii wengi wa muziki licha ya jitihada kubwa wanazofanya.
Wimbo Mahaba, kwa ujumbe wa kutafakarisha kuhusu mapenzi, unasimulia hadithi ya maisha ya uhusiano, ukionyesha zaidi matokeo ya hadithi hiyo na kusisitiza kwamba hakuna haja ya kuogopa kuingia kwenye mapenzi, hivyo kuwa huru kupenda.
Alikiba, mshindi wa MTV EMAs 2016, alitayarisha wimbo huo chini ya usimamizi wa Yogo Beats ambaye alishiriki pakubwa katika albamu yake ya tatu, Only One King (2021), huku video ikiongozwa na Bless Dollar.
Mahaba ni wimbo ulioshinda tuzo ya Muziki Tanzania (TMA) kama Wimbo Bora wa Bongofleva 2023 ikizibwaga nyimbo nyingine kali kama Yatapita (Diamond Platnumz), Baridi (Jay Melody), Honey (Zuchu) na Single Again (Harmonize).
Mradi huu ulikuja takribani miaka minne tangu Alikiba kuachana na RockStar Africa na Sony Music, lebo alizofanya nazo kazi kwa miaka mingi na kwa mafanikio makubwa akishinda tuzo mbalimbali za kimataifa.
Kati ya tuzo alizoshinda ni pamoja na All Africa Music Awards (AFRIMA) 2017 kama Wimbo Bora wa Kushirikiana Afrika (Aje) ft. M.I (Mr. Incredible), pia alishinda MTV Europe Music Awards (EMAs) 2016 kama Msanii Bora Afrika.
Ushirikiano wa Alikiba na RockStar Africa ulianza kuonekana katika wimbo wake, Mwana (2014) uliyotarisha na Man Water kutokea Combination Sound huku mwanamuziki huyo akirejea katika kile alichotaja kama kiti chake cha Ufalme wa muziki.
Hadi anaachana na RockStar Africa na Sony Music, video ya wimbo ‘Mwana’ iliyofanyika kwa Godfather wa Afrika Kusini, ndio ilikuwa namba moja YouTube kwa Alikiba, mshindi mara 18 wa TMA.
Ila kwa sasa video ya wimbo ‘Mahaba’ ndio namba moja ikiwa imetazamwa zaidi ya mara milioni 45 ndani ya miaka miwili, huku ‘Mwana’ ikiwa na milioni 42, namba ilizokusanya kwa miaka 10.
Kitambo tu ‘Mahaba’ ilionekana kuja kushika namba kwani ndani ya miezi minane baada ya kuachiwa kwake, ilitazamwa mara milioni 18 na kushika nafasi ya tatu katika orodha ya nyimbo za Alikiba zenye mafanikio YouTube.
Tunasema Alikiba ameruka kiunzi kilichowashinda wengi kwa sababu ni wasanii wachache wanaoweza kutengeneza nyimbo au wimbo wenye namba kubwa katika majukwaa ya kidijitali baada ya kuachana na lebo zilizowafanyia mambo makubwa.
Mathalani, tangu Harmonize ameondoka WCB Wasafi mwishoni mwa 2019 na kuanzisha lebo yake, Konde Music Worldwide, ameshindwa kutengeneza nyimbo kubwa YouTube kama Kwangwaru, Happy Birthday na Bado.
Hadi sasa nyimbo hizo ndio zimetazamwa zaidi (most viewed) YouTube kwa upande wake, hivyo katika miaka yake sita nje ya WCB Wasafi ameshindwa kutoa video ilizofanya vizuri kama hizo!
Ikumbukwe video ya wimbo, Kwangwaru (2018), akimshirikisha Diamond Platnumz, ndio iliyofanya vizuri zaidi YouTube ikiwa imetazamwa zaidi ya mara milioni 130, kisha ikafuata Happy Birthday (2017) yenye milioni 57.
Akiwa na lebo yake, Konde Music, video ya Harmonize yenye mafanikio makubwa YouTube ni ya wimbo, Single Again (2023), hii imetazamwa mara milioni 39, na ndio wimbo wake uliopata namba kubwa tangu ameondoka WCB Wasafi.
Kitu kama hicho hakipo kwa Harmonize pekee, bali kwa wasanii wengi walioachana na lebo zao kwa muda sasa, baadhi yao ni Country Wizzy (Konde Music), Rayvanny (WCB Wasafi), Angela (Konde Music), Cheed (Kings Music), Killy (Konde Music) n.k.
Ila kwa Alikiba ameshaufunga ukurasa huo huku video ya wimbo wake ‘Utu’ kutoka katika albamu, Only One King (2021), ikipanda kwa kasi ambapo sasa inaikaribia ‘Mwana’ na huwenda isichukua muda mrefu kuja kushika nafasi ya pili.
Ikumbukwe Alikiba alivuma katika Bongofleva baada ya kuachia albamu yake, Cinderella (2007) chini ya G Records, kisha zikafuata - Ali K4Real (2009) na Only One King (2021), pamoja na Extended Playlist (EP) moja, Starter (2024).
Alikiba, mwandishi wa kibao cha Dully Sykes, Zali (2024), anatajwa na mkongwe huyo kama Mfalme wa Bongofleva kwa sababu ni msanii wa kwanza ambaye alikuwa bado hajatoka lakini akamuomba amshirikishe katika wimbo wakati tayari Dully alikuwa msanii mkubwa wakati huo.