'All I Want for Christmas Is You' yamlipa Mariah Carey kila mwaka
Muktasari:
- Wimbo huo umekuwa kama alama ya msimu kwenye sikukuu ya Krismasi duniani kote, kutokana na kuhitajika kwake kila ifikapo Desemba. Kutokana na uhitaji huo 'All I Want for Christmas Is You' umekuwa ukimwingizia mamilioni ya dola kila mwaka mwimbaji huyo.
Marekani. Kawaida Desemba ni mwezi unaopambwa kwa mapambo na nyimbo mbalimbali zinazolenga sikukuu ya Krismasi ambayo hufanyika duniani kote kila ifikapo tarehe 25. Kati ya nyimbo ambazo huupamba mwezi huo ni 'All I Want for Christmas Is You' wa mwanamuziki wa Marekani Mariah Carey.
Wimbo huo umekuwa kama alama ya msimu kwenye sikukuu ya Krismasi duniani kote, kutokana na kuhitajika kwake kila ifikapo Desemba. Kutokana na uhitaji huo 'All I Want for Christmas Is You' umekuwa ukimwingizia mamilioni ya dola kila mwaka mwimbaji huyo.
'All I Want for Christmas Is You' uliotolewa kwa mara ya kwanza miaka 30 iliyopita, kutoka kwenye albamu yake ya nne na albamu yake ya kwanza ya Krismasi, iliyoitwa 'Merry Christmas', uliongoza kwenye Chati ya Singles ya Uingereza kwa mara ya kwanza Desemba 11,2020, ikiwa ni miaka 26 baada ya kutolewa kwake. Hata hivyo, ulirudi tena katika nafasi ya kwanza kwa wiki moja mwaka 2022.
Mariah Carey anapata mamilioni ya dola kila mwaka kutokana na wimbo wake huo kupigwa duniani kote. Mwaka 2017, gazeti la 'The Economist' liliripoti kuwa mwimbaji huyu alipata dola 60 milioni kutokana na wimbo huo, kati ya mwaka 1994 na 2016, na kwa wastani alikuwa akipata dola 2.6 milioni kwa mwaka.
Mwaka 2022, Billboard ilikadiria kuwa Mariah Carey alipata dola milioni 5.3 kutokana na toleo la rekodi kuu la wimbo huo na dola milioni 3.2 kutokana na mirahaba ya uchapishaji, jumla ikiwa ni dola milioni 8.5.
'All I Want for Christmas Is You' ni wimbo unaoongoza kwa mauzo mengi zaidi kwa Mariah Carey katika historia yake. Wimbo huu umeshauzwa zaidi ya nakala 16 milioni na unakadiriwa kuingiza dola milioni 100 katika malipo ya haki za kipekee kufikia mwaka 2023. Pia ni wimbo wa Krismasi unaosikilizwa zaidi nchini Uingereza, umesikilizwa YouTube zaidi ya mara milioni 700.