Binti wa Jay Z, Blue Ivy avunja sheria Met Gala 2026
Muktasari:
Binti wa mastaa wakubwa wa muziki Beyonce na Jay Z, Blue alivunja sheria ya hafla hiyo, sheria ambayo inawataka wageni wote wawe wamefikisha umri wa miaka 18, huku binti huyo akihudhuria katika hafla hiyo akiwa na miaka 14.
Marekani. Wki hii nchi ya Marekani ilisimama kufuatia na tukio kubwa linalosubiriwa kwa hamu kila mwaka la Met Gala ambapo mastaa mbalimbali kutoka pande zote za dunia walifanikiwa kuhudhuria huku mitoko yao ikivutia macho ya wengi.
Hafla hiyo ilifanyika mapema wiki hii Jumatatu iliyopita usiku wa Mei 4, jijini New York katika jumba la makumbusho la The Metropolitan Museum of Art, huku dhimira kuu ya mwaka huu ikiwa ni ‘Costume Art/ Fashion is Art’.
Staa ambaye ametikisa katika hafla hiyo ni mwanamuziki Beyonce ambaye baada ya miaka 10 kutoonekana katika hafla hiyo, alitinga katika onyesho hilo akiwa na binti yake mwenye umri wa miaka 14, Blue Ivy pamoja na mumewe Jay Z huku akivalia gauni la kung’aa lililobuniwa na Olivier Rousteing.
Utakumbuka mara ya mwisho Queen Bey kuonekana katika Met Gala ilikuwa ni 2016 ambapo alipata katika ngazi za The Metropolitan Museum of Art akiwa na mume wake Jay Z.
Hata hivyo inaelezwa kuwa hakukuwa na sababu ya msingi ya kutoonekana katika maonyesho hayo makubwa yanayotikisa dunia huku baadhi ya vyombo vya habari vikidai kuwa ni kutokana na 2017 kujifungua mapacha wake ambao ni Rumi na Siri pamoja na kuwa na ratiba ngumi.
Mbali na msanii huyo mastaa wengine waliotikisa ni pamoja na mwanamuziki na mfanyabiashara Rihanna ambaye aliambatana na mumewe, na kama kawaida yake aliendeleza tamaduni ya kuchelewa katika hafla hiyo kama ilivyo kawaida yake. Staa huyo alivalia gauni lenye kung’aa lililonakshiwa na stone za gold huku mumewe akitupia koti la pinki likitajwa kuwa ni heshima kwa watoto wake wa kike.
Ukiachana na wapendanao hao staa mwingine aliyebaruza ni mtayarishaji wa filamu kutoka nchini India, Karan Johar ambaye vazi lake huwenda likawa bora zaidi kwani limetejwa kutumia takribani saa 5600 (ambayo ni siku 86) huku likitengenezwa na mafundi zaidi ya 50.
Staa mwingine aliyewashangaza mashabiki ni msanii wa muziki kutoka Puerto Rico, Bad Bunny ambaye alipanda katika ngazi za The Metropolitan Museum of Art akiwa na mwonekano wa kizee. Alipozungumza na Vogue staa huyo ameeleza kuwa kilichomsukuma kutoka na mwonekano huo ni kutokana na kupendelea kufanya vitu tofauti katika maisha yake.
Hata hivyo baadhi ya media zinaeleza kuwa sababu kubwa iliyopelekea kuchagua mwonekano huo ni baada ya kuvutiwa na mwonekano wa msanii mwenzake The Weeknd alioutumia katika albamu ya ‘Dawn Fm’ ambapo alitumia taswira ya mtu mzee.
Mastaa wengine waliohudhuria katika halfa hiyo ni pamoja na Nicole Kidman, Venus Williams, Zoë Kravitz, Sabrina Carpenter, Doja Cat, Gwendoline Christie, Alex Consani, Misty Copeland, Elizabeth Debicki, Lena Dunham, Paloma Elsesser, LISA, Chloe Malle, Sam Smith, Teyana Taylor, Lauren Wasser, Anna Weyant, A’ja Wilson, Yseult, Adut Akech, Angela Bassett, Sinéad Burke, Rebecca Hall, Aimee Mullins, Amy Sherald, Chase Sui Wonders, Manish Malhotra, Isha Ambani, Karan Johar, Natasha Poonawalla na Ananya Birla.
Mtoto wa Beyonce, Blue Ivy kuvunja sheria
Binti wa mastaa wakubwa wa muziki Beyonce na Jay Z, Blue alivunja sheria ya hafla hiyo, sheria ambayo inawataka wageni wote wawe wamefikisha umri wa miaka 18, huku binti huyo akihudhuria katika hafla hiyo akiwa na miaka 14.
Jambo hilo limezua gumzo katika mitandao ya kijamii mashabiki wakidai kuwa sheria za hafla hiyo hazifuatwi kabisa baadhi wakilikashifu kuwa halina mvuto kama zamani. Hata hivyo mashabiki pia wamemnanga Blue baada ya kutinga Met Gala akiwa amevalia miwani jambo ambalo lilionekana kama amedharau wageni waalikwa.
Si Blue tuu ambaye ametinga Met Gala akiwa na umri mdogo miaka ya nyuma wapo mastaa ambao waliwahi kuhudhulia wakiwa na umri mdogo akiwamo Elle Fanning mwaka 2011 alipokuwa na miaka 13, Hailee Steinfeld miaka 14, Willow Smith na Jaden Smith mwaka 2016 walihudhuriwa wakiwa na miaka 15 na 17.
Sheria za Met Gala
Katika hafla hiyo zipo sheria 8 ambazo zimekuwa zikitiliwa mikazo ambazo ni; sheria namba moja ni lazima uwe na umri wa miaka 18 na kuendelea, Lazima uwe umealikwa rasmi, mavazi lazima yaendane na theme (mfano mwaka huu theme ilikuwa ni Costume Art), hauruhusiwi kuingia na simu wala kupiga selfi wakati wa hafla.
Lakini pia orodha ya wageni lazima ithibitishwe na Anna Wintour, hauruhusiwa kuvuta sigara, bangi wala shisha, wageni lazima kuingia kwa mpangilio maalum kulingana na mahusiano pamoja na umaarufu, hauruhusiwi kuingia na chakula ama kula vyakula vinavyoweza kuwachefua wengine kama vitunguu na parsley.
Met Gala ni nini?
Met Gala ni tukio la mitindo linalofanyika kila mwaka Jumatatu ya kwanza ya mwezi Mei, lengo kuu la tukio hilo likiwa ni kukusanya fedha kwa ajili ya jumba la makumbusho la The Costume Institute. Ambapo mapato yake husaidia maonesho, machapisho, ununuzi wa vitu vipya pamoja na uendeshaji wa kila siku katika makumbusho hiyo.