Met Gala 2026, Beyoncé atinga baada ya miaka 10
Muktasari:
- Kwa zaidi ya muongo mmoja, mashabiki wa mitindo walikuwa wakijiuliza lini malkia wa muziki na mitindo angerudi kwenye tukio hilo kubwa. Mara ya mwisho Beyoncé kuhudhuria ilikuwa mwaka 2016. Jana usiku, baada ya miaka 10, hatimaye alirudi.
Marekani. Usiku wa jana Mei 4,2026 dunia ya mitindo ilishuhudia maajabu mengi yaliyotokea Metropolitan Museum of Art jijini New York City.Baada ya nyota wakubwa wa burudani kutoka na mavazi ya aina yake katika tukio la kila mwaka la Met Gala. Hatahivyo jina lililotawala katika tukio hilo ni Beyoncé.
Kwa zaidi ya muongo mmoja, mashabiki wa mitindo walikuwa wakijiuliza lini malkia wa muziki na mitindo angerudi kwenye tukio hilo kubwa. Mara ya mwisho Beyoncé kuhudhuria ilikuwa mwaka 2016. Jana usiku, baada ya miaka 10, hatimaye alirudi.
Beyonce alifika akiwa ameambatana na mume wake Jay‑Z pamoja na binti yao Blue Ivy Carter, jambo lililofanya tukio hilo kuwa la kihistoria zaidi. Wengi walishangaa kuona Blue Ivy akiingia kwenye tukio hilo kubwa akiwa bado binti mdogo, lakini akiwa na ujasiri wa kutosha.
Beyoncé pia alikuwa mmoja wa wenyeji (co-chair) wa gala hiyo pamoja na Nicole Kidman, Venus Williams, na mhariri mkuu wa Vogue Anna Wintour.
Mavazi yaliyoshangaza
Mara tu Beyoncé alipofika kwenye ngazi za Met, kamera zote zilielekezwa kwake. Alivaa gauni maalum lililobuniwa na mbunifu maarufu Olivier Rousteing. Gauni hilo lilikuwa na muundo wa mifupa ya binadamu uliotengenezwa kwa mawe ya kung’aa juu ya kitambaa chepesi cha rangi ya ngozi, likionekana kama “skeleton ya almasi”.
Muonekano huo uliambatana na taji linalong’aa, nywele za rangi ya dhahabu zilizoteremka mgongoni, na joho refu lenye manyoya lililobebwa na wasaidizi kadhaa nyuma yake.
Ni wazi kuwa mavazi hayo yamefuata kikamilifu theme ya mwaka huu “Fashion Is Art”, ambayo ililenga kuonyesha uhusiano kati ya mwili wa binadamu na sanaa ya mavazi.
Nyota wengine waliovutia usiku huo
Usiku huo pia ulihudhuriwa na mastaa wenye majina makubwa katika burudani na mitindo. Miongoni mwa waliovutia walikuwa, Blake Lively aliyefika na gauni la kifalme lililofanana na ile mitindo ya karne ya 18.
Aidha Rihanna, kama kawaida yake aliwasili akiwa amechelewa kidogo lakini alivutia kwa vazi lake lenye vito. Kim Kardashian aliyekuwa alivalia bodysuit ya rangi ya machungwa.
Kwa upande wa Janelle Monáe aliwashangaza wengi kwa gauni lake la futuristic lililochanganywa na nyaya za umeme likiwakilisha teknolojia katika mitindo.
Ikumbukwe kuwa Met Gala haihusishi tu mavazi bali ni tukio la kuchangisha fedha kwa ajili ya taasisi ya mavazi ya jumba la makumbusho. Mwaka huu tukio hilo lilifanikiwa kukusanya takribani dola milioni 42, huku tiketi moja ikifikia hadi dola 100,000.