Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Lameck Ditto aidai Multchoice fidia ya Sh6 bilioni

Muktasari:

  • Adai imetumia wimbo wake wa Nchi Yangu kwenye biashara bila idhini yakea

Dar es Salaam. Mwanamuziki, Lameck Ditto ameiomba Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, iamuru kampuni ya Multichoice Tanzania Limited imlipe fidia ya Sh6 bilioni kwa kutumia wimbo wa Nchi Yangu, aliodai ni wake; kwenye matangazo yao ya biashara bila ridhaa yake.

Ditto ambaye jina lake halisi ni Dotto Bernard Bwakeya, pia ameiomba Mahakama iamuru alipwe Sh200 milioni kama fidia ya madhara ya jumla, pamoja na riba ya asilimia 25 tangu siku alipofungua shauri hilo mpaka litakapomalizika.

Akitoa ushahidi wake, Ditto amewasilisha vielelezo tisa katika kesi hiyo, huku akitoa ushahidi wake kwa saa sita mbele ya jaji Hamidu Mwanga, akiilalamikia kampuni hiyo kutumia wimbo huo kwenye matangazo yao ya biashara kipindi cha kampeni ya Afcon 2019.

Katika ushahidi wake akiongozwa na wakili wake, Elizabeth Mlemeta, Ditto amedai MultiChoice imempora fursa ya kunufaika na kazi yake kupitia wimbo huo.

‘Wakati wanautumia, na mimi ilikuwa niutumie kwenye kampeni ya Kibanda Umiza ya kampuni ya Betika, ikashindikana,” alisema Ditto akiwasilisha vielezo vya ushahidi wake.

Miongoni mwa vielelezo alivyoviwasilisha kuthibitisha madai yake kuwa yeye ndiyo mmiliki wa wimbo huo ni mawasiliano ya barua pepe (email) ambayo amedai alifowadiwa na Emmilian Mallya, aliyekuwa mratibu wa Tamasha la Urithi ambayo ilionyesha ushiriki wa wimbo wake huo kwenye tamasha hilo.

"Mheshimiwa jaji, huu ni wimbo wangu na mimi ndiye mmiliki, niliutunga wa kwanza nikaimba mwenyewe, nikaombwa nitunge wa pili kwa ajili la urithi ambao umeimbwa na wengi," amedai Ditto wakati akitoa ushahidi wake.

Awali, Wakili anayeiwakilisha MultiChoice, Mlano Mlekano amedai walitumia wimbo wa Nchi Yangu, lakini si huo unaolalamikiwa na mdai.

Pia Ditto aliwasilisha flash disc yenye sauti (audio) na video za matangazo anayolalamikia na nyimbo hiyo ambayo alidai ndiye mmiliki halali.

Kabla ya Mahakama kupokea kielelezo hicho, wakili wa Multi Choice Tanzania Limited, Mlekano alihoji uhalali wa video hizo kama si za kutengenezwa.

Hata hivyo, wakili wa Ditto alidai ni halali na endapo links za matangazo hayo hazijafutwa, Mahakama iridhie waangalie kwenye google.  Jaji Mwanga aliliridhia ombi hilo na video hiyo ilipochezwa, ikafunguka na kumuonyesha mchezaji wa zamani wa Simba na Yanga, Akida Makunda akihamasisha Afcon huku kukiwa na matangazo ya DSTV na katika (background) ulisikika wimbo wa Nchi Yangu.

Baada ya kuchezeshwa kwa video hiyo, wakili Mlekano alionekana akicheka, huku akiwa hajazungumza lolote na Mahakama kupokea kielelezo hicho.

Baadhi ya vielelezo vingine vilivyowasilishwa mahakamani hapo ni nakala za mawasiliano kwa njia ya whatsapp na barua pepe kati yake na mratibu wa Tamasha la Urithi.

Kesi hiyo iliendelea jana kwa mashaidi wa Ditto kutoa ushahidi wao.

Nje ya Mahakama

Wakili wa Ditto, Elizabeth Mlemeta alieleza kuwa upande wa mdai una mashahidi watano.

"Leo (juzi), shahidi mmoja ambaye ni Ditto ametoa ushahidi, upande wetu tuna mashahidi watano ambao wataendelea kutoa ushahidi, tuko hatua nyingine za kisheria ambazo zinaendelea,” ameeleza.