Miaka 13 bila uwepo wa Dk Remmy Ongala, muziki wake bado unapendwa
Muktasari:
- Usiku wa tarehe 12 Disemba 2010, katika hospitali ya Regency ya mjini Dar es Salaam, Ramadhani Mtoro Ongala, aliyejulikana zaidi kwa jina la Dokta Remmy alifariki wakati madaktari wakijitahidi kuokoa maisha yake.
Novemba 26, 2023 nikiwa na bendi yangu nilishiriki katika Tamasha la Muziki la Ongala la mwaka 2023 ( Ongala Music Festival 2023). kabla sijapanda jukwaani kutumbuiza nilirudisha kumbukumbu nyuma miaka mingi nilipoanza kumfahamu Dr Remmy Ongala.
Ilikuwa mwaka 1984, binamu yangu marehemu Andy Swebe, ambaye alikuwa mpiga gitaa la bezi wa Orchestra Makassy alinifuata na kuniomba nijiunge na bendi hiyo, wakati huo ilikuwa muda mfupi baada ya kuiacha Orchestra Mambo Bado. Nilipokweenda mazoezi, Kinondoni Moscow nyumbani kwa Mzee Makassy ndipo nilipokutana uso kwa uso na Dr Remmy, alikuwa ni mtu aliyependa sana utani hivyo ilichukua muda mfupi sana kumzoea.
Jambo ambalo sitalisahau katika kipindi hicho ni mkutano ambao nadhani ni moja ya sababu zilizomfanya Remmy aiache Orchestra Makassy na kurudi tena Super Matimila. Katika mkataba wake na Makassy, Remmy alitakiwa kuimba kwa saa mbili katika kila onyesho, katika kikao hicho wanamuziki walilalamika kuwa nyimbo alizokuwa anaimba Remmy zilikuwa ndefu mno, hivyo anaishia kuimba chache katika saa alizopewa, ulikuwa ubishani mkali sana, siku chache baadaye Remmy aliiacha Makassy na kurudi Super Matimila.
Mwaka 1995, nikiwa na wadau kadhaa tuliamua kuanzisha kampuni ya kusambaza kaseti za wanamuziki wa Tanzania, ilikuwa ni jitihada ya kujaribu kupigana na biashara haramu ya kaseti ili wanamuziki wa Tanzania japo wapate chochote kutokana na jasho lao.
Na ndipo tukasambaza albamu ya Dr Remmy iliyoitwa ‘Kilio Cha Samaki’. Baada ya hapo kila tulipokutana hatukuwa wageni tena, na nilihudhuria maonyesho mengi ya Super Matimila na mara nyingine kushiriki kupiga gitaa jukwaani. Kila ikifika Desemba huwa nakumbuka sana matukio ya mwezi huu mwaka 2010.
Desemba ya mwaka 2010 ulituachia masikitiko makubwa katika tasnia ya muziki Tanzania. Wanamuziki wawili maarufu walifariki katika kipindi cha siku chache. Usiku wa tarehe 12 Disemba 2010, katika hospitali ya Regency ya mjini Dar es Salaam, Ramadhani Mtoro Ongala, aliyejulikana zaidi kwa jina la Dokta Remmy alifariki wakati madaktari wakijitahidi kuokoa maisha yake.
Dk Remmy alipata umaarufu mkubwa nchini baada ya kujiunga na kundi la Orchestra Makassy mara baada ya kuingia nchini akitokea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Dk Remmy aliyejitaambulisha kuwa alikuwa mpwa wa Mzee Makassy, baada ya kufanya kazi nzuri akiwa na Orchestra Makassy akahamia kundi la Orchestra Super Matimila lililokuwa na makazi yake Songea.
Baada ya kukaa kwa muda katika kundi la Super Matimila ambalo kwa wakati huo lilikuwa na wanamuziki wengine mahiri akiwemo Mosese Fan Fan aliyewahi kupiga muziki katika kundi la TP OK Jazz la Franco, walikuweko pia waimbaji mahiri kina Skassy Kasambula na Kasaloo Kyanga, pia walikuwepo wapiga magitaa wengine waliobobea kama Hamza Kalala na Omari Makuka na alikuweko pia mpiga ‘drums’ mwenye uzoefu Abuu Semhando.
Dk Remmy alirudi tena Orchestra Makassy akisindikizana na Mosese Fan Fan, ni katika kipindi hicho ndipo nami nilibahatika kujiunga na bendi hiyo.
Safari ya Dk Remmy haikuwa imeisha kwani alirudi tena Super Matimila, lakini safari hii alidumu kwa muda mrefu sana na bendi hiyo iliyokuwa ikipiga mtindo walioutambulisha kuwa ni Bongo Beat. Hatimaye aliacha muziki wa dansi na kuanza kuimba wa injili na alikuwa katika muziki huu mpaka mauti yalipomkuta.
Dk Remmy alizikwa makaburi ya Sinza, jirani na mtaa uliopewa jina lake ‘Sinza kwa Remmy’. Mkesha wa siku ya mazishi ya Dk Remmy wanamuziki mbalimbali walikusanyika nyumbani kwake na kukesha wakipiga muziki wa dansi kusherehekea maisha ya mwenzao.
Katika hali ya kusikitisha na kushangaza, siku mbili baada ya mazishi ya Dk Remmy, Desemba 18, 2010, Abuu Semhando, mwanamuziki mwingine ambaye aliwahi kuwa na Dk Remmy kwenye kundi la Orchestra Super Matimila na pia ndiye aliyekuwa akiendesha pikipiki iliyoongoza msafara wa mazishi ya Dk Remmy, alipata ajali ya kugongwa na gari.
Semhando alipata ajali hiyo akiwa anatoka kwenye onyesho ya bendi yake akiwa anaendesha pikipiki. Kama saa tisa ya usiku, kiongozi wa bendi ya African Stars, Louiza Nyoni alinipigia simu na kunitaarifu kuwa Abuu amepata ajali maeneo ya Mbezi Tanki Bovu, nilichukua usafiri na kujaribu kuwahi, nikakuta Polisi wameshabeba pikipiki yake kwenye gari lao na gari iliyomgonga Abuu ikiwa pembeni kwenye mtaro.
Abou Semhando aliyejulikana kwa pia kwa jina la Lokasa au Baba Diana, alikuwa mpiga drums wa miaka mingi, kati ya bendi alizowahi kuzipigia ni pamoja na Sola TV, Super Matimila, Vijana Jazz Band, Diamond Sound na African Stars. Maiti ya Abuu ilisafirishwa na alienda kuzikwa kwao Kibanda, Muheza. Mungu awalaze pema wanamuziki hawa.