Sababu Gabo kuigiza safari ya kiongozi wa Kihehe
Muktasari:
- Filamu hiyo, imeibua mijadala miongoni mwa wadau wa sanaa na wapenzi wa filamu nchini, kutokana na kuwa na simulizi ya kweli ya historia inayohusisha kabila la Wahehe mkoani Iringa.
Dar es Salaam. Katika kipindi ambacho filamu nyingi zinajikita kwenye simulizi za mapenzi, migogoro ya kifamilia na maisha mwigizaji na mtayarishaji mkongwe wa filamu nchini, Gabo Zigamba, ameibuka na kazi tofauti inayolenga kufufua historia na utamaduni wa Watanzania kupitia filamu yake mpya ya Mwamwindi.
Filamu hiyo, imeibua mijadala miongoni mwa wadau wa sanaa na wapenzi wa filamu nchini, kutokana na kuwa na simulizi ya kweli ya historia inayohusisha kabila la Wahehe mkoani Iringa.
Akizungumza na mwananchi kuhusu kazi hiyo, Gabo amesema lengo kubwa la Mwamwindi si burudani pekee, bali kuwakumbusha Watanzania umuhimu wa kuzienzi simulizi za kale ambazo zimekuwa sehemu ya historia ya taifa.
"Filamu hii inazungumzia stori za kale, kuzikumbuka na kuzienzi. Mashabiki wana nafasi kubwa ya kujifunza kupitia uhalisia wa kwetu kwa sababu inakuza uzalendo. Mtu akijua historia ya nchi yake na yaliyotokea zamani, anapata nafasi ya kujifunza na kukuza imani ya utaifa," amesema.
Tofauti na filamu nyingi zinazotungwa kutokana na mawazo ya waandishi, Gabo amesema Mwamwindi imejengwa juu ya matukio halisi yaliyowahi kutokea.
Ameeleza kuwa kazi kubwa iliyofanyika ilikuwa kufanya utafiti wa kina ili kuhakikisha simulizi hiyo inawekwa katika mfumo wa filamu bila kupoteza ukweli wake wa kihistoria.
"Hadithi ya Mwamwindi sijaitunga. Ni hadithi ya kweli. Kilichofanyika ni kufanya utafiti na kisha kuiweka katika lugha ya filamu," amesema.
Kwa mujibu wa Gabo, mandhari kuu ya filamu hiyo ni mkoani Iringa. Huku ikibeba kwa kiasi kikubwa utamaduni wa kabila la Wahehe, jamii ambayo imekuwa na mchango mkubwa katika historia ya Tanzania.
Kupitia mavazi, lugha, desturi na mazingira yanayoonekana kwenye filamu hiyo, watazamaji wanapata fursa ya kujua historia na kujionea namna jamii hizo zilivyoishi katika nyakati tofauti.
Hata hivyo, kutengeneza filamu ya aina hiyo hakukuwa kazi rahisi.
Gabo amesema moja ya changamoto kubwa ilikuwa kurejesha mazingira ya zamani ili yaendane na kipindi ambacho simulizi hio inahusu.
"Changamoto ni kubwa sana, hasa kufanya kitu cha mwaka 1971 katika mazingira ya mwaka 2021 na kuweza kuonyesha uhalisia wake," amesema.
Licha ya juhudi kubwa zilizowekwa katika uzalishaji wake, Gabo amesema bado hajaridhishwa na mapokezi ya filamu hiyo.
Kwa mtazamo wake, simulizi kama hio ilipaswa kufika kwa Watanzania wengi zaidi kutokana na uzito wake wa kihistoria na kitaifa.
"Mapokezi bado ni madogo sana kulingana na aina ya simulizi yenyewe. Matarajio yangu yamefeli kwa sababu hii ni stori ya taifa, lakini mapokezi yake kwa sasa yako zaidi kwenye mitandao," amesema.
Kauli hiyo inaonyesha namna msanii huyo anavyotamani kuona kazi za kihistoria zikipata nafasi kubwa zaidi katika jamii, hususan katika kipindi ambacho vijana wengi wanatumia muda mwingi kwenye majukwaa ya kidijitali.
Gabo amesema bado kuna uwezekano wa kuendelezwa ikiwa mazingira yatakuwa mazuri.
"Kama nitapata fedha na idhini ya taifa, itaendelea," amesema.
Mbali na kuzungumzia Mwamwindi, Gabo pia alitoa ushauri kwa vijana wanaotamani kuingia katika tasnia ya filamu lakini wanaogopa changamoto.
Kwa mujibu wake, mafanikio hayawezi kupatikana bila kupitia magumu. Hivyo jambo muhimu ni kuendelea kuamini ndoto zao na kuwekeza katika elimu.
"Waendelee kuamini ndoto zao huku wakijifunza na kuzipalilia kwa elimu. Changamoto ndiyo ukuaji wenyewe, hivyo wasikate tamaa," alisema.
Akizungumzia mashabiki wake, Gabo amesema mchango wao umekuwa muhimu katika safari yake ya kisanii na ndiyo unaompa nguvu ya kuendelea kufanya kazi.
"Mategemeo yangu ni kwamba imani yao kwangu isipungue, kwa sababu inanijenga mno na kunipa dhamira ya kweli ya kuendelea kufanya kazi," amesema.
Kuhusu mipango yake ijayo baada ya Mwamwindi, msanii huyo alibaki kuwa mtu wa mafumbo, akisema si wakati wa kuweka wazi kila jambo.
"Silaha za vita hazitangazwi," amesema kwa kifupi.