Gabo Zigamba kuja na filamu yenye kisa cha kweli nchini
Muktasari:
- Tofauti na filamu nyingi zinazojikita katika masuala ya mapenzi, usaliti na migogoro ya kifamilia. Mwamwindi imeangazia maisha halisi ya Watanzania katika miaka ya mwanzo baada ya uhuru.
Msanii wa filamu za Bongo Movie, Gambo Zigamba, ameibuka na kazi tofauti na ilivyozoeleka katika tasnia ya filamu nchini baada ya kuachia filamu mpya ya Mwamwindi, inayotokana na moja ya visa vya kihistoria vilivyowahi kuibua mjadala nchini Tanzania enzi za Ujamaa na Kujitegemea.
Tofauti na filamu nyingi zinazojikita katika masuala ya mapenzi, usaliti na migogoro ya kifamilia. Mwamwindi imeangazia maisha halisi ya Watanzania katika miaka ya mwanzo baada ya uhuru, wakati Serikali chini ya Rais wa kwanza wa Tanzania, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ilipokuwa ikihamasisha wananchi kuishi na kufanya kazi katika vijiji vya ujamaa.
Filamu hiyo imepokelewa kwa hisia tofauti na wadau wa sanaa, huku wengi wakisifu hatua ya kuanza kuibua visa vya kweli vya kihistoria vilivyojenga taifa.
Wapo wanaoamini kuwa hatua hiyo inaweza kufungua ukurasa mpya katika tasnia ya filamu nchini kwa kuhamasisha waandishi na watayarishaji kugeukia historia yenye simulizi nyingi zenye mafunzo kwa jamii.
Kiini cha filamu hiyo ni simulizi ya Dk Wilbert Kleruu, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa na mmoja wa viongozi waliokuwa mstari wa mbele kutekeleza sera ya Ujamaa na Kujitegemea.
Dk Kleruu, ambaye alizaliwa mwaka 1929 huko Mwika mkoani Kilimanjaro, alikuwa miongoni mwa wasomi wachache wa Tanzania waliokuwa na Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Sayansi ya Siasa na Uchumi wa Kilimo, aliyopata nchini Marekani mwaka 1962.
Kutokana na uelewa wake mkubwa wa sera za maendeleo ya vijijini, aliaminiwa sana na Mwalimu Nyerere. Kabla ya kuhamishiwa Iringa, alifanya kazi mkoani Mtwara ambako alifanikiwa kuanzisha mamia ya vijiji vya ujamaa katika muda mfupi, jambo lililomjengea sifa kubwa serikalini.
Mwaka 1971 alipelekwa Iringa, mkoa uliokuwa na wakulima wakubwa waliomiliki maelfu ya ekari za mashamba pamoja na matrekta.
Serikali ilitaka wananchi hao wahamie katika mfumo wa vijiji vya ujamaa, jambo ambalo halikupokelewa kwa urahisi na baadhi yao.
Ni katika mazingira hayo ndipo simulizi ya Said Abdullah Mwamwindi inaanza.
Siku ya Krismasi, Desemba 25, 1971, Dk Kleruu alitumia siku yake kufanya kazi za kilimo katika Kijiji cha Ujamaa cha Ndolela. Alipokuwa akirejea Iringa mjini jioni, alikutana na Mwamwindi akiendelea kulima shamba lake kwa trekta katika eneo la Mkungugu.
Kwa mujibu wa simulizi za kihistoria, kulikuwa na mvutano wa maneno kati ya viongozi waliokuwa wakitetea sera za ujamaa na baadhi ya wakulima waliokuwa wakiamini katika mfumo wa kilimo binafsi.
Tukio lililofuata baadaye lilibadilika kuwa moja ya matukio yaliyotikisa Tanzania katika miaka ya mwanzo ya uhuru wake. Kifo cha Dk Kleruu kilisababisha mshtuko mkubwa nchini na kuibua mjadala mpana kuhusu utekelezaji wa sera za ujamaa, mamlaka ya serikali pamoja na uhusiano kati ya viongozi na wananchi.
Zaidi ya nusu karne baadaye, simulizi hiyo imefufuliwa kupitia filamu ya Mwamwindi, ikiwa si tu kama kazi ya burudani bali pia kama kumbukumbu ya historia ambayo wengi wa kizazi cha sasa hawajawahi kuisikia kwa undani.
Wadau wa sanaa wanaamini kuwa Tanzania ina hazina kubwa ya visa vya kweli vinavyoweza kutumika kutengeneza filamu za kiwango cha kimataifa.
Kutoka vita vya Kagera, harakati za uhuru, maisha ya viongozi wa kitaifa hadi matukio yaliyotikisa jamii katika vipindi tofauti vya historia, visa hivyo vinaweza kuwa darasa kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Kupitia Mwamwindi, Gambo amejaribu kuonyesha kuwa filamu si chombo cha burudani pekee, bali pia ni njia ya kuhifadhi historia, kuelimisha jamii na kufufua simulizi ambazo zingepotea katika kurasa za vitabu.