Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

2024 tutegemee muziki wa 'Akili Bandia'

Muktasari:

  • Teknolojia hii ya ‘multi track’ ilianzisha aina mpya ya mfumo wa muziki ambayo baada ya kukutana na teknolojia ya kidijitali ikaboreshwa hata vyombo vinapigwa na kurekodiwa kiteknolojia. Na ndipo tulipo sasa. 

Muziki wa bendi umekuwepo katika jamii yetu kwa  takribani miaka 95 sasa. Muziki wa aina hii ulianza katika enzi ya utawala wa Wajerumani. Ilikuwa katika zama hizi utamaduni wa kuwa na miji ulianza kusambaa,  watu wa kutoka makabila mbalimbali wakaanza kuishi pamoja.

Kwa kuwa walitoka katika makabila yenye utamaduni tofauti, watu hawa walianza kutengeneza utamaduni wao mpya wa ‘mjini’, kati ya mambo mapya waliyoanzisha yalikuwa muziki mpya. Ulikuwa ni waliouiga kutoka muziki wa  kijeshi wa watawala wao. Wakauita Beni Ngoma. 

Huu ukawa ndio muziki wa kwanza wa ‘kisasa’. Hata neno ‘muziki’ lilianza kutumika wakati huo, kwani lilitokana na neno la Kijerumani ‘muzik’.
Masalia ya Beni Ngoma yanaonekana wazi mpaka leo kwenye  ngoma za  kiasili za Mganda na Malipenenga, ambazo ni maarufu katika kabila la Wamanda.

Wachezaji wa muziki huo huvaa sare na huwa kunakuwa na muongozaji kama ilivyo katika bendi za kijeshi, pia ngoma hizo hutumia vifaa vinavyojaribu kupata sauti za vyombo kama saksafoni na tarumbeta za jeshi.

 Ulipoingia utawala wa Muingereza, wakaiga  teknolojia mpya hasa gramafoni. Hiki kilikuwa chombo cha kupigia santuri. Muziki mpya sasa ukaanza kusikika, wakati huohuo Waingereza wakaanzisha utamaduni wa kuwa na klabu za starehe, ambako wanachama wakaanza kushindana kucheza nyimbo zilizokuwa zikipigwa kwenye santuri, kukawa na mashindano hata kati ya klabu za miji mbalimbali.

Zilikuwepo maarufu kama  Noverty Dancing Club ya Tanga na New Generation Dancing Club ya Dar es Salaam. Katika klabu hizo za starehe pia kukawa mwanzo wa vikundi vya muziki ambavyo awali viliiga muziki uliosikika katika santuri.

Kati ya bendi za awali za mfumo huu ni  YMCA Social Orchestra na Dar es salaam Social Orchestra. Bendi hizi za mwanzo ziliitwa Social Orchestra, zilifanya shughuli ya muziki  kama burudani baada ya kazi.

Na kwa miaka mingi makao makuu ya bendi yaliendelea kuitwa klabu, utamaduni unaoendelea katika muziki wa taarabu mpaka leo.

Katika miaka ya michache kabla  na baada ya uhuru,kulitokea wimbi la kuunda bendi za muziki na kuzipa majina kutokana na maeneo ambayo waanzilishi wanatokea, mfano Rufiji Jazz Band, Kilwa Jazz Band na hata Western Jazz band.
Western Jazz band ilijiita jina hilo kwani waanzilishi walitoka katika Jimbo la Magharibi, awali nchi yetu iligawanywa katika majimbo manane na si mikoa kama siku hizi. Majimbo hayo yalikuwa ni Southern Highlands Province, Western Province, West Lake Province, Central Province, Northern Province, Eastern Province, Southern Province na Lake Province.

Kwa kuwa bendi za wakati huu zilikuwa katika mfumo wa  klabu, wanamuziki waliotakiwa katika bendi, walitafutiwa ajira au kutafutiwa sehemu za kuishi.

Walisaidiwa  na wanachama wa klabu ikiwemo malazi, chakula na hata posho kwa wale ambao ajira haikupatikana, mazoezi ya bendi yalifanyika kilabuni jioni baada ya saa za kazi.

Ujio wa wanamuziki  kutoka Congo mwanzoni mwa miaka ya 60, ulibadilisha mfumo wa bendi hizi.

Bendi za Congo ziliingiza utamaduni wa wanamuziki kuendesha maisha kutokana na kupiga muziki na nyingine zikaiga mfumo huo, ambao kimsingi ndio upo mpaka leo.

Wanamuziki waliokuwa na vikundi  lakini hawakuwa na vyombo waliweza kuwashawishi wenye fedha kuingia katika biashara hiyo, kwa kununua vyombo na kuanzisha bendi.

Mfumo huu uliendelea na baadaye idara za Serikali, kampuni  na mashirika ya umma nayo yakaanzisha bendi zao.
Kukawa na bendi zilizoanzishwa kwa malengo tofauti na si kufanya biashara.

Mashirika ya umma yalianzisha ili kutangaza bidhaa zake na kuburudisha watumishi wa mashirika hayo, na pia kuburudisha umma.

Idara za Serikali zilianzisha  kwa ajili ya kutoa burudani kwa wafanyakazi na wananchi kwa ujumla. Kwa upande mwingine kuongezeka kwa bendi kulisaidia wanamuziki wengi kupata kipato cha uhakika.

Bendi nyingine zilikuwa ni zile ambazo wanamuziki walijikusanya na kukusanya vifaa wenyewe, hivyo kujiajiri.

Bendi chache sana siku hizi ambazo ni mali ya wanamuziki wenyewe, nyingi ni ajira ya namna moja au nyingine kutoka kwa mwenye vyombo, japo wanamuziki hujitangaza kama vile wameanzisha kundi lao binafsi.

Miaka ya mwishoni mwa 80, kuliingia teknolojia iliyowezesha mtu mmoja kurekodi vyombo mbalimbali, kuimba na wimbo ukaonekana kama vile umepigwa na bendi.

Teknolojia hii ya ‘multi track’ ilianzisha aina mpya ya mfumo wa muziki ambayo baada ya kukutana na teknolojia ya kidijitali ikaboreshwa hata vyombo vinapigwa na kurekodiwa kiteknolojia. Na ndipo tulipo sasa. 
Ugunduzi wa taaluma mpya ya Artificial Intelligence (AI), unamuwezesha mtu yoyote kutengeneza hata albamu na kuamrisha teknolojia hiyo iige sauti ya muimbaji maarufu na kupata santuri nzuri.

Hakika 2024 tunaingia katika dunia nyingine kimuziki, naamini AI itatuandalia muziki kutoka ule wa asili.