2025 ni ndoa juu ya ndoa kwa Mastaa
Muktasari:
- Kwa takribani miaka sita nyuma baadhi ya mastaa waliamini kuwa kuingia katika ndoa au kutangaza uhusiano katika mitandao ya kijamiii kunaweza kusababisha kupoteza kabisa mashabiki. Lakini kwa miaka ya hivi karibuni hasa 2025 wasanii wakubwa Bongo wameonesha mabadiliko kwa kujitosa rasmi kwenye ndoa. Twende pamoja
Dar es Salaam. Tasnia ya burudani nchini kwa mwaka 2025 imeonekana kupiga hatua hasa katika mahusiano. Hii ni baada ya mastaa mbalimbali kuuaga usela na kuingia kwenye ndoa, jambo ambalo limekuwa likiibua mijadala katika mitandao ya kijamii.
Kwa takribani miaka sita nyuma baadhi ya mastaa waliamini kuwa kuingia katika ndoa au kutangaza uhusiano katika mitandao ya kijamiii kunaweza kusababisha kupoteza kabisa mashabiki. Lakini kwa miaka ya hivi karibuni hasa 2025 wasanii wakubwa Bongo wameonesha mabadiliko kwa kujitosa rasmi kwenye ndoa. Twende pamoja
Jux na Priscilia
Februari 7, 2025, mwanamuziki wa Bongo Fleva nchini Jux alifunga ndoa na mpenzi wake mfanyabiashara na mwigizaji kutoka Nigeria Priscilia.
Wawili hao walionekana kwa mara ya kwanza Julai 19, 2024 kwenye moja ya kumbi za starehe zilizopo jijini Dar es Salaam. Huku uhusiano huo ukiwekwa wazi katika mitandao ya kijamii Agosti mwaka huohuo baada ya Jux kupokelewa kwa shangwe ukweni Nigeria.
Hata hivyo baada ya kufunga ndoa na kufanya harusi kubwa Tanzania. Hekaheka za harusi yao zilihamia nchini Nigeria. Ambapo bridal Shower na sherehe kubwa ya kitamaduni.
Sherehe hiyo nchini Nigeria ilihudhuriwa na mastaa mbalimbali akiwemo Diamond, Nandy, Irene Poul, Ommy Dimpoz, Billnass, G Nako, D Voice na wengineo.
Hawakuishia hapo Aprili 19,2025 ilifanyika sherehe nyingine ya ‘white wedding’, sherehe ambayo ilizua gumzo katika mitandao ya kijamii. Baadhi ya mashabiki wakimnanga Jux kufunga ndoa ya kikristo. Jambo ambalo alikanusha kwenye moja ya mahojiano yake akieleza kuwa ilikuwa ni shererhe ya kawaida.
Sherehe ya mwisho ya ndoa yao waliimalizia Mei 28,2025 katika ukumbi wa Warehouse jijini Dar es Salaam. Katika hii pia walikusanya kijiji cha mastaa wakiwamo Lulu Diva, Aunty Ezekiel, Irene Uwoya, Jacqueline Wolper, Zuchu, Nandy, na wengine wengi.
Kwa upande wa Jux baada ya kufunga ndoa ameendelea kuvunja rekodi katika muziki akifanikiwa kupata ongezeko kubwa la mashabiki kutoka Nigeria. Wawili hao wamefanikiwa kupata mtoto wa kiume aitwaye Rakeem.
Mobetto na Aziz Ki
Baada ya kuzuka kwa uvumi wa muda mrefu hatimaye mashabiki walishuhudia picha na video mitandaoni zikimuonesha aliyekuwa mchezaji wa Yanga, Stephanie Aziz Ki akimvisha pete mwanamitindo Hamisa Mobetto.
Hata hivyo mambo yalinoga zaidi Februari 15, 2025 siku ambayo Aziz alitoa mahari kwa ajili ya kufunga ndoa na mwanamitindo huyo. Ikadaiwa kuwa alitoa mahari ya malori mawili ya ng’ombe pamoja na pesa Sh30 milioni.
Ndoa ya wawili hao ilizizima kwenye mitandao ya kijamii na kufanya mashabiki kuwazungumzia wao tu. Huku mastaa waalikwa wakigeuza harusi hiyo kama jukwaa la mitindo.
Februari 16, 2025 ndoa ya wawili hao ilifungishwa na Shekh Mkuu wa Dar es Salaam, Walid Alhad Omar na mashekh wengine katika msikiti uliopo Mbweni jijini Dar es Salaam.
Mabeste na Divashia
Mwanzoni mwa Machi kijiti kikamuangukia rapa na mtayarishaji wa muziki nchini, Mabeste ambaye alifunga ndoa na mchumba wake wa muda mrefu Divashia. Mabeste alithibitisha hilo kupitia ukurasa wake wa Instagram akionyesha furaha yake kwa kufunga ndoa na mpenzi wake.
“Hatimaye, subira imezaa heri! Nimebarikiwa kufunga ndoa na mwanamke mrembo, mwenye akili, na mwenye upendo wa dhati. Safari imekuwa ya thamani kila hatua,” aliandika Mabeste.
Utakumbuka, hii inakuwa ndoa ya pili kwa rapa huyo baada ya kuachana na mke wake wa kwanza Lisah Karl mwaka 2019, ambaye walibahatika kupata watoto wawili, Kendrick na Catelyn Mabeste.
Zuchu naDiamond
Taharuki ilianza usiku wa kuamkia Juni 3, 2025 ambapo mwanamuziki Diamond alichapisha picha za harusi huku akiachia ujumbe tata ambao uliacha maswali kwenye mitandao ya kijamiii. Hata hivyo Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam Walid Kawambwa akizungumza na mwananchi alithibitisha kuwafungisha ndoa ya wawili hao miezi kadhaa iliyopita.
“Kwanini watu wanapenda watu wengine wazini, Diamond na Zuchu ni kweli nimewafungisha ndoa mimi. Toka miezi mitano iliyopita, ila hilo swali lako unaloniuliza kuhusu wameachana mimi silifahamu. Sababu kama wangekuwa wameachana Diamond angekuja kuniambia mimi.
“Vile mlivyoona kwenye mitandao ni kweli ndoa wala sio kiki. Ila naona watu wengi wameshtushwa na hii habari, maana mmezoea kuwasema sema Diamond na Zuchu wazini kila kukicha sasa hili jambo la kheri lishangilieni na kuliombea kheri,” alisema Warid.
Aidha ndoa ya wawili hao imeendelea kudumu mpaka sasa lakini jambo la kushangaza ambalo wengi hujiuliza maswali ni wawili hao kutokufanya sherehe yoyote hadi leo.
Ibra Chinga na Hafsa
Baada ya kuwapo kwa tetesi katika mitandao ya kijamii kuhusu mwanamuziki wa Bongo Fleva nchini Ibrah kufunga ndoa na mrembo kutoka Burundi, hatimaye Chinga alithibitisha taarifa hiyo kwenye moja ya mahojiano yake baada ya kurudi Bongo.
Chinga aliweka wazi kuwa haikuwa kiki bali alifunga ndoa na mpenzi wake Hafsa Massud, ndoa ambayo ilifungwa Julai 18, 2025. Hata hivyo baada ya kulithibitisha hilo siku chache mbele kupitia ukurasa wa Instagram wa Hafsa alichapisha picha huku akiweka wazi kuwa yeye na mumewe wanatarajia kupata mtoto wao wa kwanza.
Afande Sele na Wema
Hata hivyo mwaka 2025 wakati ukielekea kuisha mwanamuziki wa Hip hop nchini, Seleman Msindi maarufu Afande Sele Desemba 6, 2025 alifunga ndoa na mwandishi wa Mwananchi Wema Makongoro.
Ndoa hiyo ya Serikali ilifungwa Morogoro mbele ya Ofisa Tawala kutoka Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Morogoro Mjini, Hilary Sagara.
Ikumbukwe Afande alimvisha pete mpenzi wake huyo Agosti 5,2025 huku akieleza kuwa ameamua kufanya hivyo kutimiza ahadi kwa mpenzi wake ambaye amekuwa naye kwa zaidi ya miaka miwili na nusu.