Aisee! Asap Rock na Drake jino kwa jino

Muktasari:

Baada ya Drake kutaja neno “anti” katika mistari yake ndipo wengi wakatambua kuwa mlengwa ni Rihanna ambaye albamu yake ya mwisho kutoa inaitwa “ANTI” iliyotoka Januari 2016 baada ya kumaliza mkataba wake na Def Jam Recording.

Hatimaye rapa Asap Rocky ameingilia kati na kujibu maneno ya shombo yaliyotolewa na Drake mwaka uliopita yaliyokuwa yakimlenga mpenzi na mzazi mwenziye Rihanna, ambaye wamejaliwa kupata  watoto wawili, RZA na Riot. 

Katika albamu yake ya Drake, ‘For All the Dogs’ (2023), kupitia wimbo wa ‘Fear of Heights’ anasikika akimchana mwanamke ambaye anadai penzi lao kipindi cha nyuma lilikuwa la kawaida sana, kwa kifupi hakuwa na maajabu yoyote.

Baada ya Drake kutaja neno “anti” katika mistari yake ndipo wengi wakatambua kuwa mlengwa ni Rihanna ambaye albamu yake ya mwisho kutoa inaitwa “ANTI” iliyotoka Januari 2016 baada ya kumaliza mkataba wake na Def Jam Recording.

Utakumbuka wawili hao mwaka 2009 walitajwa kuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi na mwaka uliofuatia Rihanna akampa shavu Drake katika wimbo wake ‘What’s My Name’, naye Drake akamshirikisha mwimbaji huyo wa Visiwa vya Barbados katika wimbo wake, ‘Take  Care’ (2012).

Hata hivyo, Rihanna katika mahojiano na Vanity Fair mwaka 2015 alikana kuwa na uhusiano na Drake baada ya kuonekana pamoja maeneo mbalimbali ikiwemo katika ziara za kimuziki, Rihanna alidai mpenzi wake wa mwisho alikuwa ni Chris Brown.

Sasa Asap Rocky amejibu kauli ya Drake kupitia wimbo alioshirikishwa na Kid Cudi ‘Wow’ kutoka katika albamu mpya, Insano (2024) iliyokutanisha wakali wengine kama Travis Scott na Lil Yachty.

Katika wimbo huo wa dakika nne, Rocky ametoa maneno makali kwa Drake na kudai hamsumbui na kutaka athibitishe kama ni kweli alitoka na Rihanna, huku akidai ana dawa ya tumbo baada ya mwaka uliopita Drake kueleza kusumbuliwa na tumbo.

Ikumbukwe ukaribu wa Rihanna na Asap Rocky ulianza kuonekana hadharani mwaka 2012 walipotumbuiza remix ya wimbo ‘Love It’ katika tuzo za MTV VMA, baadaye Rocky akaonekana katika video ya wimbo wa Rihanna, Fashion Killa (2013).

Desemba 2019 wakapita pamoja katika zulia jekundi la British Fashion Awards, na kufika Novemba 2020 wakathibitisha wao ni wapenzi na kwenda mapumzikoni katika visiwa vya Barbados ambako wote wamezaliwa huko. Mtoto wao wa kwanza alizaliwa Mei 2022 na wa pili Agosti 2023.