Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Albamu 10 Bongo zenye majina magumu, maana yake!

Muktasari:

  • Hata hivyo, baadhi ya albamu na EP kutoka kwa wanamuziki hao, zimepewa majina ambayo maana yake imefichwa kiasi kwamba si rahisi kwa shabiki wa kawaida kuweza kung'amua maana iliyokusudiwa.

Tangu kuimarika kwa njia za kuuza muziki mtandaoni (digital streaming), wanamuziki wengi nchini hasa wale wa Bongofleva wamefululiza kuachia Albamu pamoja na Extended Playlist (EP) kwa ajili ya mashabiki na hatimaye kutengeneza fedha.

Hata hivyo, baadhi ya albamu na EP kutoka kwa wanamuziki hao, zimepewa majina ambayo maana yake imefichwa kiasi kwamba si rahisi kwa shabiki wa kawaida kuweza kung'amua maana iliyokusudiwa.

Kwa mfano, Professor Jay ana albamu inaitwa Machozi Jasho na Damu (2001), Ray C ana albamu, Mapenzi Yangu (2003), hizi albamu majina yake yanatoa picha ya moja kwa moja ni kitu gani kinazungumziwa ndani yake.

Lakini vipi unaposikia Young Lunya ametoa albamu inaitwa Mbuzi (2022), Marioo ametoa EP inaitwa MMMCXII (2026) au Lady Jaydee na albamu yake iitwayo 20 (2021), hapo unapata picha gani?, sasa ngoja tukupe picha halisi kama ifuatavyo.


1. Marioo - MMMCXII

Ikiwa ni EP ya kwanza kwa Marioo baada ya kuachia albamu mbili, mwanamuziki huyo wa Bad Nation Label aliamua kuipa jina la namba za kirumi ambazo zimebeba maana kubwa katika maisha yake.

MMMCXII ni namba za kirumi ambapo kwa namba za kawaida zinasomeka 3112, namba hizi zinawakilisha tarehe ya kuzaliwa Marioo ambayo ni 31/12/1995, hivyo EP hiyo inawakilisha kuzaliwa kwake.


2. Young Killer - Super Nyota

Rapa Young Killer Msodoki aliamua kuipa albamu yake ya kwanza jina la Super Nyota  (2022), jina ambalo linawakilisha ushindi ulioleta mafanikio makubwa katika safari yake ya muziki, hivyo ni kama alirudisha shukrani.

Young Killer alishinda shindano la Fiesta Super Nyota 2012, na ndipo akapata dili la kurekodi ngoma yake, Dear Gambe (2012) iliyomtoa kimuziki, na kushinda Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) kama Msanii Bora Chipukizi 2013.


3. Abigail Chams - 5

Takribani mwaka mmoja baada ya kusaini RockStar Africa na Sony Music, Abigail Chams aliachia EP yake ya kwanza akiipa jina la 5 (2023), jina ambalo linawakilisha familia yake pamoja na tarehe yake ya kuzaliwa.

5 inawakilisha familia yao yenye watu watano, yaani baba, mama na watoto watatu, vilevile 5 hiyo inawakilisha mwezi (Mei) aliyozaliwa Abigail Chams - 7/5/2003, akiwa mtoto wa mwisho katika familia.


4. Young Lunya - Mbuzi

Rapa Young Lunya amekuwa akiita Mbuzi, jina ambalo ni tafsiri ya neno la Kiingereza 'Goat', lakini hapa likitumika kwa muktadha wa kutambulisha ubora wa muda wote, yaani the Greatest of All Time (G.O.A.T).

Hivyo kuipa albamu yake jina la Mbuzi (2024), lengo lake ni kujitambulisha kama msanii bora wa muda wote, na alifanya hivyo baada ya kutoa wimbo unaokwenda kwa jina hilo pia ulioshinda tuzo mbili za TMA.


5. Lulu Diva - The 4 Some

Mwimbaji Lulu Diva aliipa EP yake ya kwanza jina la The 4 Some (2020), neno la Kiingereza ambalo linamaanisha kundi la watu wanne wanaofanya jambo fulani kwa pamoja.

Sababu ya kuiita The 4 Some, ni kwamba ilijumuisha wasanii wanne - yeye Lulu Diva, na wale aliowashirikisha ambao ni Fid Q, Eddy Kenzo wa Uganda, na Khaligraph Jones wa Kenya, hivyo ni watu wanne walioshirikiana katika EP hiyo.


6. Izzo Bizness - The Capricorn

Rapa Izzo Bizness aliyetoka chini ya MJ Records, aliipa EP yake ya kwanza jina la The Capricorn (2021) kwa sababu ndio nyota yake kulingana na tarehe yake ya kuzaliwa ambayo ni Desemba 25.

Ikumbukwe watu waliozaliwa kati ya Desemba 22 hadi Januari 19, katika masuala ya nyota (unajimu) wapo kundi la Capricorn (Mbuzi), hivyo EP hiyo ya Izzo Bizness ilibeba maana ya kipindi alichozaliwa yeye.


7. Rosa Ree - Goddess

 Albamu yake inaitwa Goddess (2022), neno la Kiingereza lenye maana ya 'mungu mwanamke' aliyetajwa katika hadithi za zamani, ila kwa sasa hutumika kumuelezea mwanamke mwenye nguvu ya ushawishi, kujiamini na hata mrembo.

Hivyo Rosa Ree ambaye katika nyimbo zake nyingi amesikika akijiita Goddess, kujipitia albamu hiyo alitaka kujielezea kama mwanamke mwenye nguvu ambaye haogopi kusema anachokiamini, na anayepambana kufikia malengo.


8. One The Incredible - R.A.P

Rapa One The Incredible aliyetoka chini ya M-Lab, aliamua kuipa albamu yake ya pili jina la R.A.P (2014), jina ambalo linasomeka kama 'Rap' lakini kwake lina maana tofauti kabisa.

Kwa One The Incredible, R.A.P ni ufupisho wa maneno - Representing Africa Popote, akiwa na maana kuwa muziki wake hasa hiyo inawakilisha bara la Afrika kila mahali.


9. Lady Jaydee - 20

Kwa sasa akiwa tayari na albamu 10, Lady Jaydee aliamua albamu yake ya nane kuipa jina la utofauti kidogo ambalo ni 20 (2021) ambalo lilikuwa linasadifu miaka yake 20 katika muziki.

Albamu hiyo ilipangwa kutolewa mwaka 2020 ambapo Lady Jaydee alikuwa akihadhimisha miaka 20 katika muziki ila kutokana na mlipuko wa virusi vya Corona ikasogezwa mbele na kuja kutolewa 2021.


10. Nikki Mbishi - Plata O Plomo

Kati ya albamu takribani 10 alizotoa Nikki Mbishi, kuna moja inaitwa Plata O Plomo (2025), msemo wa Kihispania unaomaanisha 'fedha au risasi', na mara nyingi ulitumika katika matukio ya uhalifu yenye mnyororo mrefu wa rushwa.

Lugha rahisi, Plata O Plomo ni kitendo cha mtu kulazimishwa kuchagua kati ya kukubali ofa fulani au kuuawa, sasa Nikki Mbishi alitumia msemo huo katika albamu yake ikielezea mfumo wa sanaa na maisha kwa ujumla ulivyo katili.