Alichofanya Wizkid ni kumvua nguo Fela Kuti
Muktasari:
- Kauli hiyo imekuwa gumzo kutokana na heshima ya Kuti kwenye muziki wa Afrobeat nchini Nigeria. Kwani Kuti ndiye mwanzilishi wa aina hiyo ya muziki, ambao ni mchanganyiko wa midundo ya Yoruba, Jazz, Highlife na Funk.
Nigeria. Mwanamuziki wa Nigeria Wizkid amezua gumzo baada ya kudai yeye ni mkubwa zaidi kimuziki kuliko gwiji wa Afrobeat, Fela Kuti.
Kauli hiyo imekuwa gumzo kutokana na heshima ya Kuti kwenye muziki wa Afrobeat nchini Nigeria. Kwani Kuti ndiye mwanzilishi wa aina hiyo ya muziki, ambao ni mchanganyiko wa midundo ya Yoruba, Jazz, Highlife na Funk.
Kupitia jumbe mbalimbali za Wizkid alimshambulia Seun Kuti, mtoto wa Fela, akimuita mjinga akiwa na umri wa miaka 40.
"Mimi ni Big Wiz, kila siku nazidi kuwa mkubwa kuliko baba yako. Unataka kufanya nini?" Ameandika Wizkid
Utakumbuka ugomvi kati ya staa wa muziki Wizkid na Seun Kuti, ulianza baada ya baadhi ya mashabiki wa Wizkid kumlinganisha msanii huyo na Fela Kuti. Wakimtaja Wizkid kama “Fela mpya” kutokana na mafanikio yake makubwa kimataifa.
Kauli hizo hazikumpendeza Seun Kuti, ambaye alikemea vikali ulinganisho huo akisema ni kukosa heshima kwa baba yake aliyekuwa zaidi ya msanii, bali pia mwanaharakati na sauti ya mapambano kwa jamii barani Afrika.
Kauli za Seun Kuti dhidi ya mashabiki wa Wizkid ndizo zilizosababisha mvutano, hadi Wizkid mwenyewe kuamua kuingilia kati. Kupitia mitandao ya kijamii, Wizkid alijibu kwa maneno makali na ya kejeli. Na hapo ndipo baadhi wa mashabiki wakaona Wiz amevuka mipaka
Mchango wa Fela Kuti
Jina lake halisi ni Olufela Olusegun Oludotun Ransome-Kuti. Mwanamuziki mahiri raia wa Nigeria. Alizaliwa Oktoba 15, 1938 na kufariki dunia Agosti 2, 1997.
Kumbukumbu za muziki, zinaonyesha Kuti ndiye mwanzilishi wa mtindo uliotamba miaka ya sabini na kujulikana kama Afrobeat.
Mbali na kuimba, Kuti alikuwa mwandishi mzuri wa tungo, ambapo sehemu kubwa ya nyimbo zake aliandika mashairi mwenyewe, pia alikuwa mtayarishaji muziki.
Katika masuala ya kijamii, Kuti alishiriki kwenye jukwaa la wanaharakati wa kudai haki za binadamu na alishiriki kwenye mambo ya siasa, hii ni kutokana na uwezo na kujiamini katika kuongea.
Mama yake Kuti, Funmilayo Ransome alikuwa kinara kwenye kikundi cha wanaharakati wa kike waliokuwa wakipinga ukoloni wakati huo, wakati baba yake alikuwa mwalimu, ambapo baadaye aliweka rekodi alipochaguliwa kuwa Rais wa kwanza wa Chama cha Waalimu Nigeria.
Ndugu zake wa kiume, Beko Ransome-Kuti na Olikoye Ransome-Kuti, walisomea fani ya udaktari na walikuwa maarufu sana nchini Nigeria. kindugu, Fela alikuwa binamu wa kwanza wa mwandishi na mshindi wa tuzo ya Nobel, Wole Soyinka.
Mwaka 1958, Fela alipelekwa Uingereza kwa ajili ya masomo ya udaktari wa dawa, lakini cha kushangaza akaachana na fani hiyo na kuamua kusomea muziki.
Akiwa London kwenye chuo cha muziki cha Trinity College, alianzisha bendi iliyojulikana kama Koola Lobitos iliyokuwa ikipiga mtindo wa Jazz na highlife.
Mwaka 1960, Fela alifunga ndoa na mke wa kwanza, Remilekun (Remi) Taylor, na mwaka 1963 alirudi Nigeria na kuunda upya kundi la Koola Lobitos.
Akiwa nchini Ghana mwaka, 1967 Kuti aliutambulisha kwa mara ya kwanza muziki wake katika midundo ya Afrobeat, na baadaye mwaka 1969, Fela alikwenda kufanya shoo Los Angeles, Marekani alikokaa kwa miezi 10.
Aliporejea Nigeria alibadilisha jina la bendi yake na kuiita Africa ‘70, hatua iliyokwenda sambamba na kubadilisha maudhui kutoka muziki wa mapenzi na kuwa muziki wa mambo ya kijamii.
Mafanikio yake makubwa yalimwezesha kufungua studio ya kurekodi muziki, huku pia akifungua klabu ya usiku iliyokuja kuwa maarufu kwenye hoteli ya Empire na kuipa jina la Afro-Spot, na kisha kuibadili jina na kuwa Afrika Shrine.
Muziki wa Fela uliendelea kupanuka katika jamii nyingi za Nigeria na Afrika kwa jumla, huku pia wakati mwingine akiimba kwa lugha ya Kiingereza kwa lengo la kupata mashabiki wengi.
Fela anakumbukwa pia kwa tabia yake ya kupenda wanawake, ambapo mwaka 1978, alioa wanawake 27 kwa mara moja katika sherehe ya kimila ya watu wa Yoruba.
Sehemu kubwa ya wanawake ni wasanii wa muziki kutoka katika bendi yake iliyoibadilisha jina na kuiita Misri 80. Wanamuziki hao ni waimbaji, wacheza shoo na watayarishaji.
Mwaka 1984, Serikali ya Rais Muhammadu Buhari, ilimfunga jela Kuti baada ya kupatikana na hatia ya matumizi mabaya ya fedha kutoka shirika la kutetea haki za binadamu.
Baada ya kutumikia kifungo chake jela, aliamua kuwapa talaka wake zake 12 kwa mara moja, akisema hakuwa tena na sababu ya kuendelea na imani yake ya kuishi na wanawake wengi.
Baadhi ya nyimbo alizopata kupiga ni pamoja na Zombie ulioleta mvutano mkubwa na Serikali kiasi hata cha kupigwa na kujeruhiwa, huku studio na vifaa vya bendi yeke vikiharibiwa kabisa na askari enzi za utawala wa Rais Olusegun Obasanjo.
Agosti 1997, Olikoye Ransome-Kuti, kaka wa Fela aliyekuwa mwanaharakati wa ugonjwa wa Ukimwi na Waziri wa zamani wa Afya, Nigeria alitangaza hadharani kuwa, mdogo wake (Fela Kuti), amefariki dunia kutokana na ugonjwa wa Ukimwi.
Mazishi ya Kuti yalijaza watu zaidi ya milioni moja. Alizikwa katika eneo la Shrine. Baadhi ya nyimbo zake ni International Thief Thief,Je’ Nwi Temi, Jeun Ko Ku, Keep Nigeria One, Lady, Mattress, My Lady Frustration, Onidodo, Viva Nigeria na Zombie.