Baada ya kusepa WCB, Mbosso ageuka mfalme wa kolabo
Muktasari:
- Ndivyo tunavyoweza kusema baada ya sauti yake kuendelea kusikika katika nyimbo za wasanii wakubwa wa Bongo Fleva, hali inayoonyesha kuwa bado ni mmoja wa waimbaji wanaohitajika zaidi nchini. Kwa kifupi, unaweza kusema amewateka mastaa hadi mashabiki.
Dar es Salaam. Huenda huu ukawa wakati ambao , Mbosso, anaufurahia zaidi tangu aanze safari yake kama msanii huru.
Ndivyo tunavyoweza kusema baada ya sauti yake kuendelea kusikika katika nyimbo za wasanii wakubwa wa Bongo Fleva, hali inayoonyesha kuwa bado ni mmoja wa waimbaji wanaohitajika zaidi nchini. Kwa kifupi, unaweza kusema amewateka mastaa hadi mashabiki.
Hivi karibuni, msanii wa Bongo Fleva, Jux ameachia wimbo wake mpya Kipepeo akiwa amemshirikisha Mbosso. Kabla ya hapo, tayari Mbosso ambaye jina lake halisi Mbwana Yusuph Kilungi alikuwa amesikika kwenye Leo ya Harmonize na Bhuju ya Alikiba, kolabo ambazo zimeendelea kumuweka kwenye mjadala mkubwa wa muziki wa Tanzania, huku akiwa na safari ndefu tangu kuanza kwake muziki 2013.
Baada ya kuitumikia WCB Wasafi kwa takribani miaka saba, Mbosso aliondoka rasmi kwenye lebo hiyo Februari 2025 na kuamua kuanza ukurasa mpya kupitia lebo yake ya Khan Music.
Hatua hiyo ilizua mjadala mkubwa miongoni mwa wadau wa muziki. Wapo walioamini angeendelea kufanya vizuri kutokana na kipaji chake, huku wengine wakisubiri kuona kama angeweza kuhimili ushindani akiwa nje ya moja ya lebo kubwa zaidi Afrika Mashariki.
Majibu ya maswali hayo hayakuchukua muda mrefu. Juni 12, 2025, Mbosso alizindua EP yake ya pili iliyopewa jina la Room Number 3, ikiwa ndiyo kazi yake ya kwanza tangu awe msanii huru.
Kupitia EP hiyo, Mbosso alionyesha alikuwa tayari kuandika historia mpya. Nyimbo zake zilianza kufanya vizuri kwenye majukwaa ya kidijitali, huku mashabiki wakionesha kuwa bado wana imani kubwa na muziki wake hata baada ya kuondoka WCB.
Baada ya uzinduzi wa Room Number 3, jambo moja lilianza kujitokeza wazi. Mbosso akaanza kuonekana mara kwa mara katika nyimbo za wasanii wakubwa wa Bongo Fleva.
Mwaka 2025 alishirikishwa na Harmonize kwenye wimbo wa Leo, kolabo iliyopokelewa vizuri na mashabiki.
Mwaka 2026 akafuata Alikiba kupitia wimbo wa Bhuju, kazi iliyounganisha sauti mbili ambazo mashabiki walikuwa wakisubiri kwa muda mrefu kuzisikia pamoja.
Na sasa, Mbosso ameungana na Jux kwenye Kipepeo, wimbo unaotarajiwa kuongeza rekodi nyingine ya mafanikio katika orodha ya kolabo zake.
Muendelezo huo unaonyesha wazi kuwa tangu aanze kujitegemea, Mbosso amekuwa mmoja wa wasanii wanaotafutwa zaidi linapokuja suala la kolabo.
Kwanini kila staa anamtaka?
Jibu linaonekana kuwa rahisi. Kwa miaka mingi Mbosso amejijengea sifa ya kuwa mmoja wa waimbaji bora wa kizazi chake. Ana uwezo mkubwa wa kuandika nyimbo za mapenzi, kuimba kwa hisia na kuendana na aina tofauti za muziki bila kupoteza utambulisho wake.
Tofauti na wasanii wengi, Mbosso ana uwezo wa kuingia kwenye wimbo wa msanii mwingine na kuongeza ubora bila kuifunika kazi ya mwenye wimbo. Hilo limekuwa moja ya sababu zinazowafanya wasanii wengi wakubwa kuendelea kumtafuta kufanya naye kazi.
Pia, hana migogoro mingi inayoweza kuathiri ushirikiano wake na wasanii wengine, jambo linalorahisisha kufanya kazi na karibu kila upande wa tasnia ya muziki.
Safari ya Mbosso ilianza mwaka 2013 alipojiunga na kundi la Yamoto Band chini ya usimamizi wa Mkubwa na Wanawe.
Akiwa pamoja na Aslay, Enock Bella na Beka Flavour, kundi hilo lilitoa nyimbo nyingi zilizotikisa Bongo Fleva kabla ya kuvunjika mwaka 2017.
Baada ya hapo, Diamond Platnumz alimsajili Mbosso ndani ya WCB Wasafi, hatua iliyomfungulia milango ya mafanikio makubwa zaidi.
Ndani ya WCB, Mbosso alitoa nyimbo nyingi zilizogeuka kuwa hits, zikiwemo Hodari, Nadekezwa, Tamba, Baikoko, Kiss Me, Yataniua, Shida, Maajabu na nyingine nyingi.
Mwaka 2021 alitoa albamu yake ya kwanza Definition of Love, huku mwaka 2022 akitoa EP ya Khan, kazi ambazo ziliendelea kuonyesha uwezo wake mkubwa wa kutengeneza muziki wenye ubora.
Tangu aanze kujulikana kupitia Yamoto Band, Mbosso anaendelea kuthibitisha kuwa mafanikio yake hayakutegemea lebo pekee, bali kipaji, sauti na ubora wa muziki wake.
Kolabo zake za hivi karibuni na Harmonize, Alikiba na sasa Jux zinaonyesha kuwa bado ni mmoja wa waimbaji wanaoaminiwa zaidi na mastaa wa Bongo Fleva.
Kama mwelekeo huu utaendelea, huenda Room Number 3 ikakumbukwa si tu kama EP iliyomrudisha Mbosso baada ya kuondoka WCB, bali kama kazi iliyofungua ukurasa mpya uliomfanya kuwa msanii anayegombewa na karibu kila staa mkubwa wa muziki wa Tanzania.