BET hawajasikia hata 'Single Again' ya Harmonize!
Muktasari:
- Wasanii wa Afrika waliochaguliwa ni Burna Boy, Ayra Starr, Tems, Seyi Vibes na Asake wote wakitokea Nigeria, pia kuna wenzao kutoka Afrika Kusini ambao ni Tyla, Focalistic na Tyler ICU.
Ndilo swali la wengi baada ya wiki iliyopita kutangazwa majina ya wanaowania tuzo za BET 2024 huku kukiwa hakuna msanii hata mmoja kutokea Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla aliyechomoza katika orodha hiyo.
Wasanii wa Afrika waliochaguliwa ni Burna Boy, Ayra Starr, Tems, Seyi Vibes na Asake wote wakitokea Nigeria, pia kuna wenzao kutoka Afrika Kusini ambao ni Tyla, Focalistic na Tyler ICU.
Drake ndiye msanii aliyetajwa kuwania vipengele vingi vya BET 2024 ambavyo ni saba, anafuatiwa na Rapa mwenzake waliofanya kazi pamoja chini ya Young Money Entertainment, Nicki Minaj anayewania sita.
Tuzo hizo zinazoandaliwa na Black Entertainment Television (BET) nchini Marekani tangu Juni 19, 2001 na kufanyika katika ukumbi wa Microsoft Theater huko Los Angeles, zinatarajiwa kutolewa hapo Juni 30 mwaka huu.
Msanii wa mwisho wa Bongofleva kuwania BET ni Diamond Platnumz ambaye 2021 alitajwa kipengele cha 'Best International Act' akichuana na Wizkid, Emicida, Headie, Aya Nakamura, Young T & Bugsey, Youssoupha na Burna Boy aliyeibuka mshindi.
Wasanii wa Bongofleva kutoswa tena katika tuzo hizo kumeendelea kuibua mijadala, mathalani aliyekuwa DJ wa Harmonize, Seven amehoji kwanini nyimbo kama 'Single Again' wake Harmonize na 'Enjoy' wa Jux hazijapata nafasi wakati zimefanya vizuri.
"Kwa hiyo hawa BET hata 'Single Again' hawajaiona kweli?, 'Enjoy' je?. Kama ni kuimba ngeli (Kiingereza) 'Single Again' si ngeli tupu mle. Let's go again inshallah next time." ameandika DJ Seven kupitia Insta Story.
Kwa mwaka uliopita 'Single Again' ni moja ya nyimbo za Bongofleva zilizofanya vizuri, Harmonize mara kadhaa amejigamba kuwa yeye ndiye msanii wa kwanza Bongo kuimba wimbo wote kwa lugha ngeni na bado ukafanya vizuri nchini na kimataifa.
Alitoa remix zake mbili, ya kwanza akimshirikisha Ruger wa Nigeria aliyetamba na wimbo wake, Bounce (2021), ya pili akiwa na Nkosazana Daughter kutokea Afrika Kusini.
Wimbo huo wenye 'streams' zaidi ya milioni 10 Spotify ukiwa wa kwanza Bongo kupata namba hizo ndani ya mwaka mmoja, baadhi ya mashabiki wanasema ili tambo za Harmonize ziwe na maana basi uchaguliwe kuwania Grammy au BET kitu ambacho umeshindwa.
Utakumbuka Rayvanny ndiye pekee Bongo aliyeshinda BET ambapo 2017 aliibuka mshindi kipengele cha 'Viewer’s Choice Best New International Act' akiwa ni msanii wa pili Afrika Mashariki baada ya Eddy Kenzo wa Uganda aliyeshinda 2015.
Mwaka 2010 ndipo BET walianza kujumuisha wasanii kutoka Afrika katika tuzo zao kupitia kipengele cha 'Best International Act; Africa' ambacho 2018 kilifanyiwa mabadiliko na kuwa 'Best International Act' kikihusisha wasanii wote kutoka nje ya Marekani.
Hadi sasa Wizkid na Burna Boy ndio wasanii vinara Afrika kushinda tuzo nyingi za BET ambapo kila mmoja ameshinda mara nne ila Wizkid kuna moja alishinda kupitia kolabo yake na Beyonce, Brown Skin Girl (2019) iliyoshinda kipengele cha HER Award 2020.
HER Award ni tuzo maalumu kwa nyimbo zinazotia moyo na kuwawezesha wanawake, ilianza kutolewa 2006 ikitambulika kama BET J Cool Like That, huku Beyonce na Mary J. Blige wakiwa ndio wasanii walioshinda mara nyingi kipengele hicho hadi sasa.
Je, wajua mshindi wa tuzo za BET anavyopatikana?, hawa hawatumii mfumo wa mashabiki kupiga kura ili kumpata mshindi bali kura zinapigwa na akademi yao (BET Awards Voting Academy) yenye watu 500 waliowachagua wao.
Akademi hii inajumuisha watu mbalimbali wenye uwelewa kutoka kwenye muziki, vyombo vya habari, bloga na hata mashabiki ambao hupita katika mchakato maalumu kabla ya kutambulika rasmi.
BET kupitia tovuti yao hutoa taarifa kuwa wanahitaji wanachama wa kupiga kura, kisha wanaambatanisha na fomu ya maswali ambayo anayehitaji kuingia katika hiyo akademi atayajibu kwa ufasaha.
Maswali yanalenga kupima uelewa wa mwombaji kuhusu burudani na wale atakaowajibu vizuri ndio wanaingia katika akademi hiyo ambayo inakuwa na kazi ya kumpata mshindi sahihi wa tuzo ya BET, hivyo akademi ndio inapiga kura ya nani awe mshindi.
Hata hivyo, kuna kipengele kimoja ambacho kinatoa nafasi kwa mashabiki kupiga kura nacho ni kile cha 'Viewer’s Choice' ambacho upigaji kura utaanza Juni 6, 2024 hadi Juni 30, 2024.
Ikumbukwe hadi sasa Beyonce ndiye msanii aliyeshinda tuzo nyingi za BET kwa muda wote akiwa nazo 32 ukichanganya na alizoshinda akiwa na Destiny's Child na The Carters (Beyonce & Jay Z). Anafuatiwa na Chris Brown (19), Drake (17), Nicki Minaj (12) na Lil Wayne (11).