Britney Spears amvuruga Justin Timberlake

Muktasari:

  • Hatua hiyo inakuja miezi kadhaa baada ya Spears kutoa kitabu chake "The Woman in Me" - "Mwanamke Ndani Yangu" na kueleza jinsi uhusiano wake na Timberlake ulimvyomuacha na majereha moyoni kufuatia kulazimishwa kutoa mimba.

Mwimbaji na mtayarishaji muziki nchini Marekani, Justin Timberlake amefuta machapisho yote katika ukurasa wake wa Instagram kufuatia kuandamwa na tuhuma nzito kutoka kwa mpenzi wake wa zamani, Britney Spears.

Hatua hiyo inakuja miezi kadhaa baada ya Spears kutoa kitabu chake "The Woman in Me" - "Mwanamke Ndani Yangu" na kueleza jinsi uhusiano wake na Timberlake ulimvyomuacha na majereha moyoni kufuatia kulazimishwa kutoa mimba.

Wawili hao walianzisha uhusiano rasmi mwaka 1999 na walikuja kuachana Machi 2002, ukaribu wao ulianza wakiwa wadogo tangu enzi za utayarishaji wa kipindi cha televisheni cha ‘The Mickey Mouse Club’.

Tangu Spears, 41, kuibua tuhuma hizo, Timberlake, 42, alikuwa anafunga sehemu ya kutoa maoni kwenye kila chapisho lake jipya Instagram na sasa ameamua kufuta machapisho yote katika ukurasa huo wenye wafuasi milioni 72.1.

Vilevile Timberlake alikimbilia Mexico kwa ajili ya mapumziko na mkewe Jessica Biel ambaye walifunga ndoa Oktoba 19, 2012 katika hoteli ya Borgo Egnazia huko Fasano, Italia. Pia waliambatana na watoto wao wawili, Silas, 8, na Phineas, 3.

Hata hivyo, habari nyingine za ndani zinadai kuwa mwimbaji huyo wa wimbo maarufu, ‘Cry Me a River’ (2002) amechukua uamuzi huo kwa sababu anajiandaa kuachia albamu mwaka huu pamoja na ziara kubwa ya kimuziki Marekani.

Katika kitabu chake Britney Spears alidai kuwa Timberlake alimwambia atoe ujauzito huo kwa sababu hakuwa tayari kuwa baba kwa wakati huo.

"Tulihakikisha hakuna mtu atakayejua kuhusu ujauzito au utoaji mimba, hatukuiambia familia yangu, mtu pekee ambaye alijua zaidi ya Timberlake na mimi, alikuwa Felicia Culotta (msaidizi wa zamani wa Spears) ambaye alikuwa kila wakati ananisaidia," ameandika Spears kwenye kitabu hicho chenye historia ya maisha yake ndani ya muziki na nje, ambapo pia alieleza kuachana kabisa na muziki. 

"Siku iliyopangwa, nikiwa na Felicia na Timberlake, nilichukua vidonge vidogo na kumeza, punde tu nilianza kusikia tumbo likiuma, niliingia bafuni na kukaa humo kwa saa nyingi, nikiwa nimelala sakafuni, nikilia na kulia pamoja na kupiga kelele," ameandika Spears.

Staa huyo baada ya kutengana na Timberlake mwaka 2002, alipata watoto wawili, Sean Preston (2005) na Jayden James (2006) pamoja na aliyekuwa mume wake Kevin Federline, ambaye waliachana kwa talaka Julai 2007.