Changamoto za kiafya zilivyokatisha safari ya Bitchuka
Muktasari:
- Taarifa zinaeleza kuwa Bitchuka amekuwa akisumbuliwa na tatizo la presha ya macho. Hali iliyowalazimu madaktari wanaomfuatilia kumshauri kupunguza shughuli zinazoweza kuathiri afya yake, ikiwemo kuimba na kufanya maonyesho ya muziki.
Dar es Salaam. Mwanamuziki mkongwe wa muziki wa dansi nchini, Hassan Rehani maarufu Bitchuka 'Stereo', ameendelea kuishi mbali na jukwaa la muziki kutokana na changamoto za kiafya.
Taarifa zinaeleza kuwa Bitchuka amekuwa akisumbuliwa na tatizo la presha ya macho. Hali iliyowalazimu madaktari wanaomfuatilia kumshauri kupunguza shughuli zinazoweza kuathiri afya yake, ikiwemo kuimba na kufanya maonyesho ya muziki.
Hatahivyo anaendelea kuwa miongoni mwa wanamuziki wa dansi waliofanya vizuri nchini. Anaendelea kusikilizwa kupitia kanda, CD na majukwaa mbalimbali ya kidijitali ambako mashabiki wanapata kufurahia nyimbo zake.
Amewahi kufanya kazi na bendi kongwe zikiwemo Nuta Jazz Band (sasa Msondo Ngoma), DDC Mlimani Park Orchestra pamoja na Orchestra Safari Sound (OSS).
Katika kipindi chake cha ubora, Bitchuka alijizolea umaarufu kutokana na sauti yake ya kipekee. Uwezo wa kutunga nyimbo zenye ujumbe mzito na umahiri wa kuwasilisha kazi zake jukwaani.
Wengi wanampenda kupitia nyimbo zake za uzalendo, maendeleo na maisha ya jamii ambazo zilipata umaarufu mkubwa ndani na nje ya Tanzania.
Mbali na uimbaji, Bitchuka alishiriki kutunga na kuimba nyimbo zilizohamasisha mshikamano wa kitaifa. Maendeleo na harakati za ukombozi wa baadhi ya nchi za Afrika wakati wa enzi za chama cha TANU na baadaye CCM.
Wadau wengi wa muziki wa dansi wanamtaja Bitchuka kama mmoja wa waimbaji walioacha alama kubwa katika historia ya muziki wa Tanzania.
Ushirikiano wake wa muda mrefu na marehemu Muhidin Maalim Gurumo pia unaendelea kukumbukwa kama moja ya pacha zilizotikisa zaidi muziki wa dansi nchini.
Licha ya kutokuwa jukwaani kwa sasa, mchango wake katika muziki wa Tanzania unaendelea kuishi kupitia nyimbo mbalimbali zilizowahi kufanya vizuri kama.
Nani Kama Mama, Sina Deni, Mkulima wa Kijijini na kazi nyingine zilizobeba mafunzo na burudani. Ambazo bado zinasikika katika vyombo vya habari na miongoni mwa wapenzi wa muziki