Christian Bella atangaza vita ya burudani
Muktasari:
- Bella anatarajiwa kutumbuiza katika tamasha maalumu la The VIP Experience, litakalofanyika Julai 31 mwaka huu kwenye ukumbi wa The Voice, uliopo Tabata Kinyerezi, Dar es Salaam. Tamasha hilo, linaloandaliwa na The Voice, litakuwa la kwanza kufanyika tangu kuzinduliwa kwa ukumbi huo, huku waandaaji wakieleza kuwa maandalizi yote yamekamilika.
Dar es Salaam. Mwanamuziki wa muziki wa dansi, Christian Bella, ameendelea kuwashukuru Watanzania kwa sapoti kubwa wanayoendelea kumpa katika safari yake ya muziki, huku akiahidi kuwapa burudani ya kiwango cha juu katika tamasha lake lijalo.
Bella anatarajiwa kutumbuiza katika tamasha maalumu la The VIP Experience, litakalofanyika Julai 31 mwaka huu kwenye ukumbi wa The Voice, uliopo Tabata Kinyerezi, Dar es Salaam. Tamasha hilo, linaloandaliwa na The Voice, litakuwa la kwanza kufanyika tangu kuzinduliwa kwa ukumbi huo, huku waandaaji wakieleza kuwa maandalizi yote yamekamilika.
Mbali na maandalizi ya jukwaa na mfumo wa viingilio, waandaaji wamesema pia wameimarisha ulinzi na usalama ili kuhakikisha mashabiki wanapata burudani katika mazingira salama.
Akizungumzia tamasha hilo, Christian Bella amesema anathamini upendo mkubwa anaopata kutoka kwa mashabiki wake nchini na kuahidi kuwapa onyesho litakalobaki kwenye kumbukumbu zao.
"Ninaendelea kuwashukuru Watanzania kwa upendo na sapoti kubwa ambayo wamekuwa wakinionyesha kwa miaka yote. Nimejipanga vizuri kuhakikisha kila atakayefika anapata burudani ya kweli," amesema Bella.
Tamasha la The VIP Experience linatarajiwa kuwakutanisha mashabiki wa muziki wa dansi kutoka maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam na nje ya jiji hilo, huku Bella akitarajiwa kuimba nyimbo zake maarufu zilizoendelea kutamba kwa miaka mingi.