Chuck Norris wa 'The Delta Force' afariki dunia
Gwiji wa mapigano na filamu za kivita, Chuck Norris, ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 86 huko Hawaii, Marekani.
Taarifa ya kifo chake imetangazwa na familia yake ambayo imesema mazingira ya umauti wake wangependa yabaki kuwa faragha, japo kuna wanaodai alikuwa akiumwa kwa kipindi fulani.
"Kwa huzuni kubwa mioyoni mwetu, familia yetu inatangaza kifo cha ghafla cha mpendwa wetu Chuck Norris kilichotokea jana asubuhi (Alhamisi)."
Taarifa hiyo ya familia iliendelea kwa kusema; " Ingawa tungependa kubaki faragha kuhusu mazingira ya kifo chake, tafadhali fahamuni kwamba alikuwa amezungukwa na familia yake na alikuwa katika hali ya amani."
Katika miaka ya 1980, mwigizaji huyo alijizolea umaarufu kupitia filamu kama The Delta Force na Missing in Action, akijijengea jina kama shujaa asiyeogopa chochote.
Baadaye, alizidi kung’ara kupitia kipindi maarufu cha televisheni Walker, Texas Ranger, ambapo alicheza kama askari.
Nyuma ya kamera, Norris alikuwa alikuwa mtaalamu wa mapigano, akiwa na mikanda myeusi kadhaa.
Umahiri wake ulimfanya aheshimiwe duniani kote na mwaka 1989 alitunukiwa nyota kwenye Hollywood Walk of Fame heshima kubwa kwa mchango wake.
Maisha yake pia yaligusa historia ya sanaa ya mapigano kupitia urafiki wake wa karibu na Bruce Lee.
Wawili hawa walifanya mazoezi pamoja na baadaye wakaonekana katika filamu ya The Way of the Dragon, pambano lao likibaki kuwa moja ya matukio ya kukumbukwa zaidi katika historia ya filamu.
Hata baada ya kupunguza uigizaji, Chuck Norris hakuwahi kupotea mioyoni mwa watu. Alibaki kuwa gumzo mitandaoni kupitia hadithi za utani kuhusu nguvu.
Siku chache kabla ya kifo chake, alionekana mwenye furaha akisherehekea siku yake ya kuzaliwa ya miaka 86, akionesha kuwa bado alikuwa na nguvu na roho ile ile ya ushindi.
Alizaliwa mwaka 1940 huko Oklahoma na kabla ya umaarufu, alilitumikia jeshi la anga la Marekani.
Katika maisha yake, alijenga familia na kuacha watoto watano. Leo, dunia inaaga shujaa wa kweli aliyewahamasisha wengi kuishi kwa ujasiri.
Pumzika kwa amani, Chuck Norris aliyoyafanya yataendelea kuishi.