Diamond aweka historia mpya kwenye Bongo Fleva
Muktasari:
- Kupitia mafanikio ya shoo hiyo, pia Diamond ametunukiwa cheti na uongozi wa Royal Albert nchini humo ikiwa ni sehemu ya utaratibu wa kumbi kubwa duniani kufanya hivyo kama ishara ya kumpongeza msanii kwa mafanikio ya kuuza tiketi zote na kujaza ukumbi kwenye show yake.
Msanii wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz ameandika historia mpya kwenye muziki huo usiku wa kuamkia leo Juni 14, 2025, baada ya kuujaza ukumbi wa Royal Albert uliopo jijini London kwa kuingiza mashabiki zaidi ya 5000.
Kupitia mafanikio ya shoo hiyo, pia Diamond ametunukiwa cheti na uongozi wa Royal Albert nchini humo ikiwa ni sehemu ya utaratibu wa kumbi kubwa duniani kufanya hivyo kama ishara ya kumpongeza msanii kwa mafanikio ya kuuza tiketi zote na kujaza ukumbi kwenye show yake.
Katika shoo hiyo ambayo Diamond aliambatana na familia yake akiwemo Mama Dangote, msanii huyo alifanya sapraizi ya kuwapandisha wasanii kama Tiwa Savage, Mr Flavour, Patoranking, Jux, na wengineo.
Diamond alipafomu nyimbo zake hit ikiwemo Komasava, Marry You, Fire, Jeje, Enjoy, Waah, bila kusau My Darling aliyoshirikishwa na Chella Boi.
Kupitia mafanikio ya shoo hiyo, Diamond amepongezwa na wengi akiwemo mke wake ambaye ni msanii wa Bongo Fleva, Bi Zuhura 'Zuchu'.
Kupitia akaunti yake ya Instagram, Zuchu aliandika: "Mume wangu kijana wa kimasikini tokea Tandale M/Mungu akutunze kwaajili yetu, aisee maana halisi ya mpambanaji unanifundisha sana, najifunza mnoo, hakuna kukata tamaa, hakuna kisichowezekana."
Nae mtayarishaji wa muziki nchini, S2kizzy ‘Zombie’ kupitia ukurasa wake wa instagram amechapisha video ya shoo hiyo huku akiandika "UK London History made" Pia G Nako kupitia ukurasa wake wa Instagram ameandika "Bendera ya Tanzania inapepea London"
Ukumbi wa Royal Albert ulianza kujengwa mwaka 1867 na ukakamilika na kuanza kutumiwa mwaka 1871 kisha ukafanyiwa marekebisho mwaka 1996 mpaka mwaka 2004, una uwezo wa kuingiza Watu 5,272.
Utakumbuka ukumbi huo pia umewahi kutumiwa na wasanii wakubwa wakiwemo Psquare Septemba 21, 2022, ambapo waliungana na wasanii wengine kama Dbanj, Awilo Longomba, na Weird MC, wasanii wengine ni pamoja na Wagner, Verdi, Rachmaninov, The Beatles, Frank Sinatra, na Adele.
Hatahivyo, baada ya tamasha lake kubwa kwenye ukumbi wa Royal Albert Hall, London lilofanyika Juni 13, 2025, msanii huyo nyota wa Bongo Fleva ameendelea kuonesha ukubwa wake kupitia tukio la kukutana na kusalimiana na mashabiki zake 'Meet and Greet'.
Tukio hilo linatoa nafasi kwa mashabiki kukutana, kusalimiana na kupiga picha na Diamond kwa tozo ya dola 55 sawa na sh 165,000, bila kujumuisha tiketi ya tamasha.
Tukio hilo limepangwa kuanza leo Juni 14 hadi 17, na tiketi zinapatikana hadi Juni 16 saa 2:00 asubuhi.
Kwa ujumla, tukio hili linaonesha hadhi mpya ya Diamond kimataifa na kuimarisha nafasi ya Bongo Fleva kwenye muziki wa duniani