Dida salio la kizazi cha CNN
Muktasari:
- ‘Taimu’ ile Amina Chifupa yuko juu kuliko ofisi yake. Alipendwa haswa. Alihusudiwa mno. Alifuatiliwa sana. Na aliuza gazeti za udaku kinoma. Wakati huo kama taifa ‘tukiwishi’ Ikulu akaishi Jakaya na Salma wake
Dar es Salaam, Benja na Anna wakiishi Magogoni. ‘Bigi Bosi’ wa Dar es Salaam akiwa Baba January. Usalama wa Bunju, Kiluvya, Pugu, Vikindu ukiwa chini ya Tibaigana. Sauti ya Pius ikishika hatamu pale Bungeni.
‘Taimu’ ile Amina Chifupa yuko juu kuliko ofisi yake. Alipendwa haswa. Alihusudiwa mno. Alifuatiliwa sana. Na aliuza gazeti za udaku kinoma. Wakati huo kama taifa ‘tukiwishi’ Ikulu akaishi Jakaya na Salma wake.
Club Bilcanas ‘site senta’, Mambo Club ‘Obei’, Kwa Macheni Mapipa, Blue Palms Mikocheni, Ambiance Sinzani. Maeneo hayo kwa kiasi kikubwa yalichelewesha maisha ya vijana wengi. Sikia kwa watu.
Wapo waliochelewa kujenga ama kuoa. Wapo walioshindwa kumaliza ‘digrii’ au ‘mastazi’. Kwa sababu ya maeneo hayo mtambuka. Siyo poa, bata lililiwa kikatili na ‘masela wa mjini, ‘mabraza kwa maduu’.
Nyakati hizo Bongo Fleva, Maigizo runingani, Umiss na utangazaji wa radio vilishika hatamu. Tasnia hizi zilibebana na kutengeneza vijana wenye majina makubwa. Na muziki wa dansi pia ulikuwa juu.
Banza Stone wa Moto. Ally Choki hakamatiki. Mwinjuma Muumini anakimbiza. Fm Academia huwezi kuwagusa. Kuna Chuchu Sound na Wazee wazima Sikinde na Msondo. Wote wapo kileleni.
Ni wakati ambao kuliibuka kundi la Al Qaeda. Achana na lile la Osama. Hili lilikuwa la Bongo hapa hapa na liliundwa na pisi kali mjini. Kiongozi mkuu wao akiwa Amina Chifupa. Ni kama kituko lakini ni hali halisi kwa wakati ule.
Akiwepo ‘Sintah’, ‘Nora’, Maimartha Jesse na Dida Shaibu. Ajenda kuu yao ikiwa ni kupambana na wezi wa waume za watu. Lakini katika wote ni Amina Chifupa pekee aliyekuwa na ndoa kwa wakati ule.
Walifanya kazi kubwa zilizowapa majina makubwa. Dida akiwa binti mdogo akisoma na kutangaza pale Times Fm. Aliyefanya mapinduzi ya taarabu na kufuta utawala wote wa Bongo Fleva, kwa vipindi vya muda ya mchana.
Kila radio ilikuwa na kipindi cha muziki wa kizazi kipya mchana. Lakini Didah akaja na Mitikisiko ya Pwani yenye taarabu. Mtoto huyu alijaaliwa maneno ya shombo na vijembe vingi. Ikawa sumu kali kwa mtaa.
Akaishika Dar na Pwani yote. Mtaa gani usiotaka sauti Didah? Kimbiza sana, katisha sana nyonga watoto wa uswazi. Aliwapa wanachokiishi, akawa kipenzi chao na kuuamrisha mtaa ufanye vile atakavyo. Ulimtii.
Mitikisiko ya Pwani ikawa taasisi ndani ya taasisi ya Times Fm. Dida akawa maarufu sawa ama zaidi ya taasisi yake. Hii haikuja kwa bahati mbaya, alifanya kazi kubwa sana iliyomjenga yeye na ofisi yake.
Dida ndio mastaa wa tangu utotoni. Yupo juu toka wakati wa Benja, JK, Magu na Samia. Wakati huo watoto wa mjini kila J’pili ni Leaders Club. Na Twanga Pepeta wakituimbuiza na kutuchezesha. Dida yupo.
Ni mwendo wa ‘hagi’ nyingi, maana wengi tulijuana. Jakaya yupo Ikulu, pesa kitaa zipo tu. Hakuna mikeka wala ujambazi. Washikaji wanapiga pombe nyingi na hawaishiwi. Ndoa nyakati hizo pia Dida anakimbiza.
Wakati huo kuna Banza na Choki. Na kuna Aisha Madinda na Lilian Internet. Wanakupa burudani hadi unawashangaa wanaenda kanisani badala batani. Dida naye alikuwa na dunia yake ya taarabu.
Pisi za mjini Khadija Kiuno, Ester Mshepu, Halima Mchunaji, Mboni wa Mchina, Tele Midollar, Diana Vipedo na Mariam wa Ilala mtaa wa Arusha. Huwakosi viwanjani hao, hii leo sijui wamezeekea wapi?
Dida hatunaye. Ametangulia kule ambako wote tutaenda. Sauti yake kali, yenye mamlaka ya mtoto wa kitaa. Haitasikika tena katika spika za redio zetu mitaani. Kipaji halisi kimeondoka kikiacha alama kuu isiyofutika.
Jina lake linajaza kurasa za kitabu cha vipaji halisi. Ambavyo vinasepa katika wakati ambao vinahitajika zaidi. Kizazi cha dhahabu ndani ya Bongo hii kinapukutika siku hadi siku. Kwenye kila tasnia.
Amina, Ruge, Complex, Vivi, Ngwea, Fredwaa, Cpwaa, Langa, Kanumba, Mez B, Adam Kuambiana, Mr Ebbo, Banza Stone, Aisha Madinda. Dah! Ukurasa hautoshi huu. Siku mbili hizi pia tunaondokewa na Dida wa Mchops, Dida Shaibu.
Dida Shaibu. Mwenye utajiri wake wa maneno. Alikuwa moja kati ya vijana wa kile kizazi cha dhahabu. Kizazi ambacho kilizaliwa baada ya 80 na kabla ya 90. Papa John Paul 11, aliita kizazi cha CCN.
Fuatilia kwa makini. Waliozaliwa baada ya 1980 na kabla ya 1990. Ni kizazi mtambuka kwa kila nyanja. Dida ni sehemu ya kizazi hiki cha dhahabu. Kizazi cha CCN kwa kauli ya Papa Mtakatifu Joh Paul 11.