Filamu ya Children of Honey yashinda tuzo Uingereza
Picha kushoto ni muongozaji wa filamu Emanuel Musa Marco, katikati ni mtayarishaji wa filamu Simona Nickmanova, na kulia ni muongozaji wa filamu Jigar Ganatra.
Muktasari:
- Katika tuzo hizo zaidi ya miradi 600 kutoka nchi mbalimbali iliwasilishwa kuwania tuzo hiyo. Lakini miradi mitano pekee ilifanikiwa kufika hatua ya mwisho. Na baada ya ushindani mkali, Children of Honey ilitangazwa mshindi.
Uingereza. Filamu ya Children of Honey imeshinda tuzo maarufu ya Whickers Film & TV Funding Award 2026, katika tamasha la kimataifa la filamu Sheffield DocFest nchini Uingereza.
Ushindi huo umeiwezesha filamu hiyo kupata ufadhili wa Pauni 120,000 za Uingereza, zaidi ya Sh400 milioni kwa ajili ya kukamilisha uzalishaji wake
Katika tuzo hizo zaidi ya miradi 600 kutoka nchi mbalimbali iliwasilishwa kuwania tuzo hiyo. Lakini miradi mitano pekee ilifanikiwa kufika hatua ya mwisho. Na baada ya ushindani mkali, Children of Honey ilitangazwa mshindi.
Kupitia filamu hiyo iliyoongozwa na Jigar Ganatra pamoja na Emanuel Musa Marco, kijana kutoka jamii ya Wahadzabe, imemuwesha Emanuel kuweka historia kuwa mmoja wa watu wa jamii hiyo kushiriki kuongoza filamu inayosimulia maisha ya watu wake.
Children of Honey inaeleza maisha ya vijana watatu wa Kihadzabe, wanaokabiliana na changamoto za kukua na kuwa watu wazima katika kipindi ambacho jamii yao inapitia mabadiliko makubwa ya kijamii na kiutamaduni.
Filamu hiyo inaonesha mapambano ya kuhifadhi utamaduni, lugha na utambulisho wao huku wakikabiliana na dunia inayobadilika kwa kasi. Kilichowavutia majaji ni namna filamu hiyo ilivyowapa Wahadzabe nafasi ya kuwa wasimulizi wa hadithi zao.
Picha kushoto ni muongozaji wa filamu Emanuel Musa Marco, katikati ni mtayarishaji wa filamu Simona Nickmanova, na kulia ni muongozaji wa filamu Jigar Ganatra.
Watayarishaji wa filamu hiyo walisema ushindi huo una maana kubwa zaidi ya fedha walizopata. Walisema ni uthibitisho kuwa jamii za asili zina uwezo wa kusimulia hadithi zao kwa sauti zao wenyewe na kusikika katika majukwaa makubwa duniani.