Hamisa Mobetto kafunga kazi na Alikiba!
Muktasari:
- Ni pale Hamisa alipotokea katika video ya wimbo wa Alikiba, Dodo (2020) ambao umetayarishwa na Yogo Beats. Huku video yake iliyoteka mazungumzo mtandaoni ikisimamiwa na kampuni ya Rockshot
Dar es Salaam. Miaka mitano iliyopita, mwanamuziki wa Bongofleva, Alikiba na mwanamitindo Hamisa Mobetto walikutana Zanzibar na kufanya kazi ambayo ilikuwa na matokeo mazuri katika ukuaji wa shughuli zao za sanaa.
Ni pale Hamisa alipotokea katika video ya wimbo wa Alikiba, Dodo (2020) ambao umetayarishwa na Yogo Beats. Huku video yake iliyoteka mazungumzo mtandaoni ikisimamiwa na kampuni ya Rockshot.
Hata hivyo, Alikiba katika moja ya mahojiano yake alisema hakujua kama Hamisa atatokea kwenye video hiyo. Ni jambo lililopangwa na uongozi wa Kings Music, hivyo ilikuwa kama sapraizi kwake kukutana na Hamisa Zanzibar.
Video ya wimbo huo ulioandikwa na Alikiba na Tommy Flavour, mwimbaji wa zamani wa Kings Music, katika mtandao wa YouTube tayari imeshatazamwa (views) zaidi ya mara milioni 25.
Hadi kufikia sasa, Dodo (2020) inashikilia nafasi ya nne katika orodha ya nyimbo za Alikiba zilizofanya vizuri zaidi YouTube ikiwa imetanguliwa na nyimbo kama Mahaba (2023), Mwana (2014) na Utu (2022).
Kingine cha kufurahishwa ni kwamba Alikiba ndiye msanii wa mwisho kwa Hamisa kufanya naye kazi upande huo. Yaani tangu kichupa cha 'Dodo' kiachiwe, mrembo huyo hajaonekana tena katika video ya msanii mwingine.
Uamuzi huo wa Hamisa umekuja baada ya hapo awali kufanya kazi na waimbaji wengine kama Abdukiba, Barnaba, Quick Rocka na Diamond Platnumz, mwanzilishi wa WCB Wasafi.
Kwa mujibu Hamisa, ili aweze kutokea kwenye video ya msanii yeyote ni lazima yeye ndiye awe mhusika mkuu (main character), kitu ambacho kimefanyika pia katika video yake na Alikiba iliyofanyika Zanzibar.