Huu hapa ukurasa mpya wa Mbosso nje ya WCB
Muktasari:
- Hii inakuwa kazi ya kwanza kwa Khan kuachia tangu alipotangaza kuachana na lebo iliyokuwa ikimsimamia, Wasafi mwezi Februari, 2025.
Dar es Salaam. Baada ya mashabiki kusubiri kwa hamu kazi mpya kutoka kwa msanii wa Bongo Fleva, Mbwana Kilungi maarufu Mbosso hatimaye msanii huyo ametangaza tarehe ya kuachia Ep yake mpya ya Room Number 3 itakayotoka Juni 12, 2025.
Hii inakuwa kazi ya kwanza kwa Khan kuachia tangu alipotangaza kuachana na lebo iliyokuwa ikimsimamia, Wasafi mwezi Februari, 2025.
Awali Mbosso alitangaza kuachia Ep hiyo leo Juni 9, lakini amehairisha bila kutoa sababu za kufanya hivyo baadala yake kutangaza kuachia kazi hiyo siku ya Juni 12, 2025
Mbosso ambaye amekuwa kimya kwa takribani miezi minne bila kuachia muziki mpya, hivi karibuni ameingia kwenye vichwa vya habari baada ya kutangaza kurudi na kazi mpya aliyokuwa amepanga kuachia leo Juni 9, 2025.
“Najua umenimisi sana na unastahili kunipata kwa asilimia mia, karibu kwenye Room Number 3 Ep, tuonane Juni 12, 2025,” ameandika Mbosso kupita akaunti yake ya Instagram.
Muitikio wa mashabiki
Kupitia chapisho hilo lililowekwa leo Juni 9, 2025 majira ya saa 4 asubuhi, mashabiki mbalimbali wametoa komenti zao huku wakimuhusisha aliyekuwa bosi wake, Diamond kuwa chanzo cha msanii huyo kubadili tarehe ya kutoa Ep hiyo ambapo awali alitangaza kuiachia leo.
“Kaka umeshatukaribisha sana inatosha sasa, embu tupe EP yetu wewe uendelee na mambo yako," aliandika shabiki mmoja huku mwingine akiongeza kuwa: "Double release ya Diamond imekutisha ungetoa bana ushakuwa mkubwa wewe."
Komenti nyingine ilisomeka hivi: "We Mbosso tumechoka kusubiri bana weka.”
Wengine wameandika hivi: “Bora ulivyompisha Simba mana leo lengo uachie ila alivyoachia Simba ukaona usogeze mbele, kweli una respect sana brother Mbosso.”
“Unaakili nyingi sana wewe jamaa🙌🙌 wakubwa tumekuelewa kwa nini umesogeza mbele.. Diamond tunamjua mzee wa bato la chinichini, inshalla see u 12 June.”
“Najua Mbosso una heshima sana, umeshindwa kutoa nyimbo kwasababu ya Mondi katoa nyimbo zake, safi sana bro, najua unafahamu kuwa ukitoa wataanza kusema mnashindana, busara sana umetumia, me niko nawe japo nasubiri sana vyuma hivo.”
Hata hivyo hivi karibuni msanii hyo alishirikishwa kwenye kazi za wasanii wengine kama 'Boda' ya Billnass na 'Look for Love' ya Darassa.
Wimbo wake wa mwisho kuachia chini ya lebo hiyo unaitwa 'Kupenda' uliotayarishwa na Laizer Classic, ambao ulitoka Januari 10, 2025 na tayari huko YouTube umetazamwa zaidi ya mara milioni 5.9
Hadi anaondoka WCB Wasafi, Mbosso alikuwa ametoa albamu moja, Definition of Love (2021), EP moja, Khan (2022) ambapo Room Number 3 (2025) itakuwa Ep yake ya pili.
Mbali na kutoa ngoma hizo, lakini pia Mbosso amefanya kolabo na wasanii wa kimataifa akiwemo Mr. Flavour, Reekado Banks na Liya (Nigeria), Costa Titch na Chley (Afrika Kusini), Bahati (Kenya), Spice Diana (Uganda) na Innoss'B (DR Congo) ambaye pia kashirikiana na Diamond, Rayvanny na Zuchu.
Katika muda aliokuwa ndani ya WCB kuanzia Januari 2018 hadi Februari 2025, Mbosso amewahi kushinda tuzo moja ya muziki Tanzania (TMA) kama Msanii Bora wa Kiume wa Bongofleva 2022.