I see! Amber Rose kapenda tena! 

Muktasari:

  • Amber, 40 na Rock, 58, wanadaiwa kuwa katika uhusiano mpya ambao bado hawajauthibitisha, katika matembezi yao Rock alionekana kumsimulia Amber hadithi ya kuchekesha waliposimama pembezoni mwa barabara.

Mwanamitindo maarufu duniani, Amber Rose na mchekeshaji Chris Rock wana lao jambo baada ya kuonekana pamoja katika matembezi huko New York, Marekani siku moja baada ya sikukuu ya Krismasi.

Amber, 40 na Rock, 58, wanadaiwa kuwa katika uhusiano mpya ambao bado hawajauthibitisha, katika matembezi yao Rock alionekana kumsimulia Amber hadithi ya kuchekesha waliposimama pembezoni mwa barabara.

Wawili hao ambao walivalia miwazi ya giza, huku nyuso zao zikipambwa na tabasamu, wanarejea tena katika vichwa vya habari baada ya wote hapo awali kwa nyakati tofauti kueleza hawapo tena kwenye uhusiano wowote.

Amber Rose amewahi kuwa na uhusiano na mastaa kadhaa wa Hollywood, alipata umaarufu alipoanza kutoka na Kanye West mwaka 2008.

Kufuatia kutengana na Rapa huyo wa ngoma 'Heartless' mnamo 2010, Amber alihusishwa na wanaume wengine maarufu kama Machine Gun Kelly, 21 Savage, Odell Beckham Jr. na Wiz Khalifa ambaye aliolewa naye na kupata mtoto, Sebastian, 9.

Uhusiano wake wa hivi karibuni aliouweka wazi kwa umma ulikuwa kati yake na Alexander 'AE' Edwards ambaye walikuwa pamoja kutoka mwaka 2018 hadi 2021 na kupata mtoto mmoja, Slash, 4.

Sababu ya kuachana kwao, Amber alidai kuwa mwenzake hakuwa mwaminifu hata kidogo, Januari mwaka huu aliapa kutokuwa tena katika uhusiano baada ya kile alichoita historia mbaya dhidi ya wanaume.

"Nataka kuwa peke yangu maisha yangu yote, sitaki kushirikiana nyumba yangu au maisha yangu na mtu yeyote, sitaki mtu yeyote awe karibu na watoto wangu. Sitaki kufanya ngono tena.

"Niko sawa kuwa peke yangu, nina furaha sana kutoshiriki kitanda changu na mtu yeyote,” alisema Amber Rose katika mahojiano na Podcast ya Sofia With F.

Kwa upande wake, Chris Rock alifunga ndoa na Malaak Compton mwaka 1996 hadi 2016, kuanzia Juni 2022 alikuwa na Lake Bell na baadaye akawa na mtangazaji wa Uingereza, Sharon Carpenter ingawa urafiki wao ulikuwa wa muda mfupi.

"Sina mtu, nimekuwa peke yangu kwa muda mrefu. Nilikuwa kwenye ndoa kwa muda mrefu na nilikuwa na uhusiano na mtu kwa muda fulani ila sasa niko ‘single’," alisema Chris Rock katika mahojiano yake na Netflix hapo Machi mwaka huu.