Ilipo tofauti ya Tiffah Dangote na Blue Ivy Carter

Miaka minane iliyopitia Zari The Bosslady na Diamond Platnumz walimleta duniani Latiffah Naseeb ‘Tiffah Dangote’ akiwa ni mtoto wa nne kwa Zari ila wa kwanza kwa ‘staa’ huyo wa Bongo Fleva kutoka WCB.

Januari 2015 ndipo Diamond alithibitisha Zari ni mjamzito baada ya kufanyika vipimo katika hospitali ya Dr. Makhubela nchini Afrika Kusini na kufika Agosti 6, 2015 saa 10:40 alfajiri ndipo Tiffah akazaliwa. 

Tiffah ni mtoto pekee wa kike kwa Zari kati ya watoto watano alionao, vilevile ni mtoto pekee wa kike kwa Diamond kati ya watoto wanne aliojaliwa kwa wanawake watatu tofauti ambao ni Zari, Hamisa Mobetto na Tanasha Donna.

Uhusiano wa Diamond na Zari ulioanza mwaka 2014 na kutamatika 2018 ulikuwa wenye ushawishi mkubwa katika kiwanda cha burudani Afrika Mashariki hasa katika kundi kubwa la vijana, huku wakijaliwa watoto wawili, Tiffah na Nillan.

Hilo lilifanya Tiffah alipozaliwa kuwa mtoto maarufu katika mitandao ya kijamii, ndani ya mwaka mmoja tayari alikuwa ni wafuasi zaidi ya milioni 1 katika mtandao wa Instagram na sasa amefikisha milioni 3.9.

Ni mtoto wa kwanza nchini na Afrika Mashariki kuwa na wafuasi wengi tena katika ukurasa ambao umeidhinishwa (verified) na Instagram mwenyewe. Ukimtoa mdogo wake, Nillan, hakuna mtoto mwingine wa staa Bongo ambaye amefikisha walau wafuasi milioni 1 huko Instagram.

Hata hivyo, licha ya ushawishi huo bado Diamond na Zari hawajataka kumuhusisha mmoja kwa moja na kazi yao ya muziki, na hapa ndipo unaanza kuonekana tofauti ya Tiffah Dangote na Blue Ivy Carter, ambaye ni mtoto wa Beyonce na Jay Z.

Diamond ambaye kwa mara ya kwanza alimtaja na kumuonesha Tiffah katika video ya wimbo wake, ‘Utanipenda’ (2015) akiwa na Zari, aliwahi kueleza hofu yake kama mtoto huyo ataingia kwenye muziki kwa madai kuna mambo yasiyofaa hasa kwa wasanii wa kike. Utakumbuka Diamond ni msanii mkubwa Afrika akiwa ameanzisha lebo ya WCB Wasafi, ametoa albamu tatu na EP moja, ameshinda tuzo za ndani na nje zaidi ya 40 na amewekeza katika miradi mingi ya kibiashara.

Naye Zari kutokea Uganda kabla ya kukutana na Diamond aliwahi kufanya muziki hapo awali na kutoa nyimbo kama Oliwange, Jukila, Kangume, Kikooma, Hotter Than Them, In Love With The Dance Floor, Falling In Love n.k.

Lakini, hilo halijatosha kwa Diamond na Zari kumpa mtoto wao nafasi katika muziki licha ya kuonyesha anaweza kwa mujibu wa baadhi ya video zake katika mitandao anazoonekana akiimba na kucheza.

Hata hivyo, kwa Blue Ivy aliyezaliwa Januari 7, 2012 wazazi wake, Beyonce na Jay Z walimpa nafasi mapema katika muziki, akiwa na umri wa miaka tisa tu, Blue Ivy alishinda tuzo ya Grammy 2021 kupitia wimbo ‘Brown Skin Girl’ alioshirikishwa na mama yake.

Huyu ni mtoto mdogo wa pili duniani kushinda Grammy baada ya Leah Peasall anayeshikilia rekodi ya kuwa mtoto mdogo zaidi kushinda tuzo hizo ambapo mwaka 2002 alishinda akiwa na umri wa miaka minane, umri ambao ni sawa na Tiffah kwa sasa. 

Ikumbukwe muda mfupi baada ya kuzaliwa Blue Ivy sauti yake ilisikika kwenye wimbo ‘Glory’ wa baba yake Jay Z ambao uliingia chati za Billboard na kumfanya Blue Ivy kuandika rekodi nyingine ya dunia kama mtu mdogo zaidi kuingia katika chati hizo.

Hadi sasa Blue Ivy ameshinda tuzo za Grammy, MTV VMAs, Shorty, The Daily Califonian, Soul Train (2), NAACP Image (2), Voice Art na BET katika kipengele cha BET HER na kuandika rekodi kama mtu mwenye umri mdogo zaidi kuwahi kushinda BET.

Tuzo ya BET Her ni maalumu kwa nyimbo zinazotia moyo na kuwawezesha wanawake, kwa mara ya kwanza ilitolewa mwaka 2006 ikitambulika kama BET J Cool Like That, na hadi sasa Beyonce na Mary J. Blige ndiyo wasanii walioshinda mara nyingi kwenye kipengele hicho.

“Ninapomwambia Blue Ivy ninajivunia yeye, ananiambia anajivunia mimi na ninafanya kazi nzuri, ni tamu sana,” Beyonce aliliambia jarida la Vogue la Uingereza.

Pia Blue Ivy amewahi kutumbuiza mara kadhaa, katika tuzo za Oscar 2022 akiwa na umri wa miaka 10 aliungana na mama yake, Beyonce kutumbuiza wimbo wake ‘Be Alive’ uliotumika katika filamu ya ‘King Richard’.

Januari 2023 aliungana tena na Beyonce jukwaani kutumbuiza huko Dubai katika ufunguzi wa Hoteli ya Atlantis The Royal Resort ambapo walilipwa Dola 24 milioni (zaidi ya Sh60 bilioni) kwa shoo iliyodumu kwa saa moja na nusu tu.

“Unajua kuhisi kupendwa ndilo jambo muhimu zaidi ambalo mtoto anahitaji, sijali ikiwa mtoto wangu hataki kuwa katika muziki au michezo, lakini ilimradi anahisi kuungwa mkono na kupendwa, lolote linaweza kutokea,” alisema Jay Z.

Katika video za Beyonce zilizoandaliwa na Disney kutoka kwenye filamu, ‘The Lion King’ (2019), Blue Ivy ameonekana katika video za nyimbo mbili ‘Spirit’ na ‘Bigger’ na kumfanya kuwa ‘staa’ wa video za muziki duniani.

Hata hivyo, licha ya umaarufu na mafanikio hayo kimuziki, Blue Ivy hayupo Instagram wala mtandao mwingine wowote wa kijamii, Beyonce na Jay Z hawajataka hilo kwa sasa kama ambavyo Zari na Diamond hawajataka Tiffah kufanya muziki mapema.

Na hii ni tofauti ya pili kubwa kati ya Tiffah Dangote na Blue Ivy Carter ambao wote ni watoto wa kwanza wa kike wa ‘mastaa’ Afrika na Marekani, wazazi wao wakiwa maarufu katika muziki, mitindo na filamu huku akitengeneza fedha nyingi katika biashara nje ya sanaa yao.