King aliyeondoka na kutuachia majuto...

Muktasari:

  • Alipoanza hakufahamu kama sanaa hii ingeweza kumpa pesa, nyumba, gari na utajiri chekwa. Vyote hivyo vilikuta yeye akiwa tayari yuko juu kwenye sanaa. Navyo vikaungana naye kuikuza sanaa yake

‘Yeah! Hii ni rimembaringi satadei’Aliyefanya tucheke mpaka mashavu yameremete kwa machozi. Ndiye huyohuyo aliyefanya tulie mpaka mashavu yetu yameremete kwa machozi. Hakika kifo hakijawahi kuwa rafiki na nyoyo za binadamu daima dumu.

Alikuwa alama sahihi ya mswahili. Alikuwa ngao ya utamaduni wetu. Alikuwa mhimili wa utu wetu. Alikuwa binadamu aliyetuongezea siku za kuishi. Kwa vicheko na furaha kwenye sebule za nyumba zetu.

King aliondoka akatuachia Majuto. Amri Athuman, kiumbe mwenye kila kitu cha kumliwaza mgonjwa, mfiwa, mfungwa ama mnyonge yeyote katika uso wa dunia hii. Aliondoka na hatutomuona tena zaidi ya kumbukizi za kazi zake.

Baada ya muda mrefu wa utumishi wake kwenye sanaa. King akatuachia Majuto katika uso wa dunia. Baada ya miaka mingi ya furaha, vicheko na tabasamu kila tumuonapo. Runingani, majukwaani mpaka mitaa ya Chumbageni na Sahare.

Hakutulazimisha kucheka. Tulilazimika kucheka kila tumuonapo. Gwiji la sanaa kuwahi kutokea Tanzania hii. Aliifanya sanaa ya kuchekesha watu ionekane kitu rahisi mno kupitia yeye. Mwamba kweli kweli aliyejaaliwa na Allah.

Kuna mambo aliyafanya watu wakaumia mbavu kwa kicheko, ambayo mwingine angeyafanya yakageuka kero kwa watu. Majuto alikuwa katili wa mbavu za watu. Kupitia kazi yake ya ‘komedi’ iliyompatia pesa uzeeni.

Jambo lolote ukifanya kwa kuzidisha sana ni sehemu ya ukatili. Sasa Majuto alipitiliza kuchekesha watu, sasa akawa katili zaidi wa mbavu za watu.

Tatizo siyo kuchekesha. Tatizo hata yeye akichekeshwa kicheko chake kilikuwa kichekesho zaidi. Kuliko hata kichekesho cha mchekeshaji. Hakujitengeneza ila aliumbwa hivyo. Sanaa ya kuchekesha ilijenga undugu na mwili wake.

Watu tunaishi mara moja duniani, kibaya zaidi tukiondoka hatuzaliwi tena kupitia mwili wa binadamu wengine waliobaki.

Wengi wamekuta sanaa ina pesa tayari. Wakaamua kuungana nayo wapate pesa. Uhalisia haupo. Kipindi ambacho furaha inahitajika sana. Majuto anaamua kutuacha. Miaka ya karibuni, kuna mengi yanafanya furaha kiwe kitu adimu kwenye mioyo ya watu.

Jamii imekuwa na mifarakano kuanzia ngazi ya familia kaya mpaka taifa. Watu aina ya King hawakupaswa kipindi hiki kutuachia Majuto. Sanaa na vipawa vyao vilifaa kutuweka sehemu moja. Katika wakati ambao tunahitaji furaha ili kujenga uzalendo. Ni wakati ambao tulimhitaji sana.

Ukitazama sinema zake kwenye basi unasahau kama kuna ajali duniani. Kama ni kibarazani usingekumbuka kelele za mwenye nyumba. Kama ni chumbani mawazo ya kishetani ya usaliti wa ndoa ungeyapuuza.

King Majuto ni sehemu ya binadamu walioletwa ili tusahau shida zetu. Mungu alitupa rafiki wa maisha yetu ya shida na raha. Mungu huyo huyo katuondolea chanzo cha furaha katika maisha ya kila siku. Ila kazi ya Mola ‘hainaga’ kwere.

Kama ambavyo huwezi kuipata Tanzania mpya. Pia huwezi kumpata King Majuto mwingine. Kuna vitu vya kipekee kamwe havijirudii kwenye uso wa dunia. Nyerere hatozaliwa tena, kama ilivyo Magufuli, Lowassa na Sokoine.

Firauni anaweza kuzaliwa tena katika mwili wa Aldof Hitler. Lakini Nabii Mussa mwingine hajawahi kuwepo hata mfano wake tu. Ikiwa na maana kuwa mtu mwema au mwema sana, hutokea mara moja tu. Na Majuto alikuwa miongoni mwa watu wema.

Siyo kwa kukosa dhambi katika maisha yake. Hapana, bali kwa kujaza upendo na furaha kwenye akili na mioyo ya watu, hata wakawa pamoja kwenye kicheko. Mtu mwema huwaweka watu pamoja. Aliwafanya watu wengi wawe na furaha.

Kila mtu kwa nafasi yake atengeneze furaha. Kadiri unavyokaza shingo yako na kuwa ngumu kwa sababu tu ya chuki zisizo na mbele wala nyuma. Tambua kuwa unayakaribisha jirani mno mauti ya nafsi yako. Wenye furaha huishi muda mrefu.

Furaha ndo kila kitu kwa maisha ya mwanadamu. Tunatafuta pesa ili kujenga furaha. Tunataka uongozi bora ili tuwe na furaha. Tunaoa na kuolewa na wapenzi sahihi, ili tuishi kwa furaha. Kila kitu kinafanyika ili kuleta furaha.

Kazi ya kutengeneza furaha kwenye mioyo na nyuso za binadamu. Majuto alifanya kwa miaka mingi sana. Tena bila kutuangusha hata mara moja.

Msanii mmoja nyota na mwenye jina kubwa, aliwahi kuniambia kuwa Majuto amefanya naye kazi nyingi sana, lakini ndiye msanii ambaye huwa anapata tabu sana kufanya naye kazi. Tabu yenyewe ni kuvumilia kumaliza ‘sini’ moja baada ya nyingine.

‘Sini’ moja wangeweza kurudia mara kumi. Kwa sababu ya kushindwa kuzuia kicheko kwa jambo ‘siriazi’. Wanaweza kuigiza wapo msibani waonekane wana majonzi. Hapo ndo penye mtihani hapo.

 Majuto kwa hali yoyote alikuwa anakupa ‘konteti’.
Mzee Majuto angeweza kuigiza kweli mtu mwenye majonzi makubwa. Lakini yule anayeigiza naye atagalagala kwa kicheko. Kila alichofanya kilikuwa ni kichekesho kwa wengine.